Prime
Wizara nne kupambania bajeti zao

Muktasari:
- Wabunge wa Tanzania wanaendelea kujadili bajeti za wizara mbalimbali kwa mwaka 2025/26 na wiki ijayo kutakuwa na wizara nne ambazo mawaziri wake watakuwa na jukumu la kuhakikisha wanazipigania ili kuwashawishi wabunge wazipitishe.
Dodoma. Wizara nne zitaingia kwenye mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/26, huku utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Toleo la mwaka 2023 ukitarajiwa kuteka mjadala wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Watakaoanza kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara zao kwa wiki inayoanza kesho, Jumatatu, Mei 12, 2025, watakuwa ni Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inayoongozwa na Profesa Adolf Mkenda, na Wizara ya Viwanda na Biashara, inayoongozwa na Dk Selemani Jafo.

Nyingine zitakazowasilisha makadirio yao ni Wizara ya Uchukuzi inayoongozwa na Profesa Makame Mbarawa, na Jeshi la Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linalosimamiwa na Dk Stergomena Tax.
Kati ya bajeti hizo, ni ya wizara ya elimu pekee ambayo itajadiliwa kwa siku mbili, huku nyingine zikiwa siku moja moja.
Hoja nyingine katika mijadala hiyo ni uwepo wa wafanyabiashara wa kigeni wanaofanya biashara zinazoweza kufanywa na wazawa, uboreshaji wa utendaji kazi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), na ujenzi pamoja na ufanyaji kazi wa usafiri wa Reli ya Kisasa nchini (SGR), migogoro ya ardhi kati ya wananchi na maeneo ya jeshi.

Katika Bunge hilo lililoanza vikao vyake Aprili 8, 2025, limeshajadili na kupitisha bajeti ya wizara sita ambazo ni za Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Rais, Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Nishati, Katiba na Sheria na ile ya Madini.
Wizara nyingine ambazo zimeshawasilisha makadirio yake na kupitishwa na wabunge ni Wizara ya Ujenzi, Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, na Wizara ya Maji.
Tayari Serikali imeshazindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya mwaka 2014, Toleo la mwaka 2024 ambayo inakwenda kuleta mageuzi makubwa katika elimu nchini.
Utekelezaji wa sera hiyo, ambao umeanza kwa awamu kuanzia mwaka jana, umeanzia katika elimu ya awali, darasa la kwanza, la tatu, kidato cha kwanza, kidato cha tano na mwaka wa kwanza wa elimu ya juu.
Jumla ya shule 98 za sekondari teule, 28 kati yake za Serikali, zilipangwa kuanza utekelezaji wa mafunzo ya awali ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera iliyoboreshwa.
Hata hivyo, zipo changamoto katika utekelezaji wa sera hiyo ikiwemo uhaba wa walimu wa amali na weledi, pamoja na ukosefu wa vyuo maalumu kwa mafunzo ya ualimu wa amali.
Februari 11, 2025, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za kamati yake kwa mwaka 2024, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Saiboko, alisema walimu wa amali wanaohitajika ni 620, waliopo ni 62 na upungufu ni 558.
Hata hivyo, Februari 14, 2025, Bunge lilipitisha nyongeza ya bajeti ya Sh945.7 bilioni, huku likieleza kuwa kati ya fedha hizo, Sh131.4 bilioni zitakuwa kwa ajili ya kugharamia maeneo mbalimbali ya elimu nchini.
Miongoni mwa shughuli hizo ni mahitaji ya mtaala mpya wa sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari za amali, upatikanaji wa vifaa na walimu.
Hata hivyo, kelele za wadau wa elimu wakiwemo Taasisi ya HakiElimu, zimeendelea kutaka bajeti ya elimu iongezeke kutoka asilimia 12.5 ya bajeti kuu ya Serikali kufikia angalau asilimia 15 ili ipunguze changamoto katika sekta hiyo, ikiwemo ya walimu.
Akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2025/26, Aprili 10, 2025, Mbunge wa Kuteuliwa, Shamsi Vuai Nahodha, alisema bado mfumo wa elimu hautengenezi wahitimu wenye weledi na umahiri mkubwa kwa sababu hauzingatii shauku ya kujifunza kwa wanafunzi, lakini pia vipaji vyao.
Akapendekeza Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) kuandaa walimu kwa mafunzo, hasa katika mbinu za kisasa za kufundishia na kutumia teknolojia ya kisasa katika elimu, na pia walimu kutumia kompyuta kwa njia ya mtandao kuwaonyesha watoto majaribio ya kisayansi.
Mbali na maoni ya wadau wa sekta ya elimu, bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeongezeka kutoka Sh1.68 trilioni kwa mwaka 2023/24 hadi Sh1.97 trilioni katika mwaka 2024/25.
Akizungumza na Mwananchi, Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu, amesema ni vyema elimu ya amali ikafundishwa kulingana na shughuli zinazofanyika katika kila eneo nchini, ili kuleta manufaa kwenye jamii inayozunguka shule husika.
"Kama kule kwetu watekeleze amali katika utalii na kilimo, kwenye jamii za kifugaji pia wafundishwe masuala ya ufugaji," amesema Jesca ambaye pia ni mdau katika sekta ya elimu nchini.
Naye mmoja wa wazazi, Justina Mbilinyi, amesema ni vyema Serikali kuhakikisha inawekeza kwa walimu wa kutosha wenye weledi na ujuzi katika kufundisha masomo ya amali ili kufanya utekelezaji wa sera hiyo kuzaa matunda yaliyotarajiwa.
“Tunaweza kuwa na sera nzuri, mitaala mizuri lakini bila kuwekeza kikamilifu, itakuwa ni ngumu kupata matokeo yanayokusudiwa na wimbo ukawa ule ule wa kutaka uboreshaji wa elimu yetu,” amesema.
Wageni kuvamia biashara
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Severine Mushi, aliwasilisha kilio cha ongezeko la raia wa kigeni wanaofanya biashara rejareja (machinga), hali inayowaathiri wafanyabiashara wazawa katika Soko la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Mushi alitoa kilio hicho Januari 30, 2025, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya chakula cha mchana alichokiandaa Rais Samia kwa ajili ya washiriki wa shughuli ya uokoaji wa kuporomoka kwa jengo la Kariakoo lililosababisha vifo vya watu 31 na wengine 80 kujeruhiwa.
Kutokana na kilio hicho, Rais Samia alimuagiza Waziri Jafo kuangalia biashara zinazofanywa na wenyeji, hali iliyomfanya waziri huyo Februari 2, 2025, kutangaza kamati ya watu 15 iliyoongozwa na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Profesa Edda Lwoga.
Kwa mujibu wa ripoti ya Lwoga iliyokabidhiwa kwa Waziri Jafo, katika eneo la Kariakoo pekee, maduka 75 yalikutwa na raia wa kigeni 152 walioajiriwa, huku asilimia 97 wakijihusisha na biashara za rejareja.
Aprili 24, 2025, Idara ya Uhamiaji ilitangaza kuwakamata raia 7,069 wanaofanya shughuli hizo.
Hatua ya kukamatwa kwao, kwa mujibu wa idara hiyo, imetokana na uchunguzi wa miezi minne kuanzia Januari hadi Aprili 2025 katika mikoa yote nchini.
Kwa mujibu wa taarifa ya uhamiaji iliyotolewa na Msemaji wa Uhamiaji, Paul Msele, kati ya waliokamatwa, 1,008 wamefikishwa mahakamani, huku 703 wamehukumiwa kifungo gerezani na 257 wamehalalisha ukazi wao.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa wengine 4,796 wameondolewa nchini na watuhumiwa 305 uchunguzi bado unaendelea.
Katika mwaka 2024, wizara hiyo iliidhinishiwa na Bunge Sh110.89 bilioni, ikiwa imeongezeka kutoka Sh92.34 bilioni iliyoidhinishwa mwaka 2023/24.
Mbunge wa Viti Maalumu, Grace Tendega, ameshauri Serikali kuhakikisha wafanyabiashara wanaotoka nje ya nchi wanafuata utaratibu unaotakiwa katika shughuli zao na kuwa makini kwa vibali wanavyovitoa kwa ajili ya wageni hao.
“Kama walichoombea kuja hapa nchini ndicho wanakifanya na Serikali imeridhia, ni sawa lakini kama ni tofauti na hapo, Serikali iangalie suala hili kwa sababu ni kuwanyima fursa Watanzania kwa biashara ambazo wangeweza kuzifanya,” amesema.
Amesema ni vyema wageni waje kusaidia Watanzania kwenye masuala ya teknolojia za viwanda ambazo Watanzania hawana ili waweze kuwainua kiuchumi.
Utendaji wa ATCL
Katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, alisema mwaka wa fedha 2023/24, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lilipata hasara ya Sh91.8 bilioni, ikiwa ni ongezeko la asilimia 62 kutoka Sh56.6 bilioni mwaka 2022/23.
Hasara hiyo inatokana na gharama kubwa ya matengenezo ya ndege na hitilafu za injini, ambapo ndege za Airbus zilikaa muda mrefu bila kufanya kazi.
Lakini si mara ya kwanza kwa CAG kuzungumzia hasara hizo katika ripoti ya utekelezaji wa shughuli zake kwa mwaka 2021/22 ilieleza kuwa ATCL ilipata hasara jumuishi ya Sh152.96 bilioni tangu mwaka 2015/17.
Februari 23, 2022, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi (sekta ya Uchukuzi), Dk Ally Possi, alisema kuwa sababu ya hasara ya Sh60.24 bilioni ni athari ya ugonjwa wa Uviko-19.

Katika mwaka 2023/24, Wizara ya Uchukuzi ilitengewa bajeti ya Sh2.08 trilioni, huku mwaka 2024/25 ikiongezewa fedha kufikia Sh2.72 trilioni.
Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest, amesema ukisoma ripoti za CAG, inaelezwa juu ya hasara zinazopatikana kutokana na ucheleweshaji wa ujenzi wa viwanja vya ndege.
“Unakuta walipanga hivi, lakini wakiingia katika utekelezaji inakuwa tofauti, hivyo kusababisha kuongezeka kwa fedha ambazo hazikuwa katika mpango. Tunajua bajeti ya Wizara ya Uchukuzi inachukua eneo kubwa la bajeti, lakini tukitoa fedha kwa wakati, itatufanya kuondoa riba,” amesema Anatropia.
Amesema hali hiyo inafanya sehemu kubwa ya bajeti hiyo kwenda katika riba, fidia na mambo mengine, kinyume na malengo, hivyo utekelezaji wa bajeti kuwa chini kwa miaka mingi.
Kuhusu utendaji wa ATCL, Anatropia amesema changamoto ya shirika hilo inatokana na matatizo katika mikataba, kwa sababu wanakodi ndege kutoka kwa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA).
“Kwa hiyo changamoto ya kukodi ndege, unakuta hata isipotembea, isipotengeneza fedha, wao wanaendelea kulipa. Kwa hiyo ukiangalia actual running cost (gharama halisi za uendeshaji) yao na wanachokipata, unakuta wanapata hasara,” amesema.
Amesema hata hivyo, unaporudi katika mikataba ya ukodishaji, unakuta shirika hilo linapata hasara na akashauri Serikali kubadilisha muundo wa uendeshaji wa ATCL ili kubadili vitabu vyake.
Wizara ya Ulinzi
Kwa upande wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), hoja ya hali ilivyo hadi sasa kuhusiana na migogoro ya ardhi kati ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni miongoni mwa mambo yatakayozungumzwa katika bajeti hiyo.
Katika bajeti ya mwaka 2024/25, Waziri wa Ulinzi na JKT, Dk Stergomena Tax, alisema kupitia Mpango wa Kutatua Migogoro ya Ardhi wa Mwaka 2021/22 - 2023/24, wizara hiyo imeendelea kutatua migogoro ya ardhi.
Alisema mpaka sasa, asilimia 89.7 ya migogoro yote iliyotambuliwa imetatuliwa kwa kuhuisha mipaka, kupima na kulipa fidia kwa wananchi wanaostahili.
Katika mwaka 2024/25, wizara hiyo ilipitishiwa na Bunge Sh3.23 trilioni, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh2.98 trilioni kwa mwaka 2023/24.