Prime
Jaji Warioba ataka mambo manne yazingatiwe Katiba Mpya

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba akijibu maswali ya waandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) wakati wa mahojiano yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam.Picha na Sunday George
Muktasari:
- Asema viongozi wasiosikiliza wananchi ni hatari, aonya wanaoita Serikali ya awamu, akimkumbuka Mwalimu Nyerere
Dar es Salaam. Ni dhahiri kwamba harakati za kudai Katiba mpya hazijapoa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba ametia mguu akisisitiza mjadala huo unapaswa kuendelea hadi 2025.
Jaji Warioba amebainisha maeneo makuu manne yanayopaswa kupata mwafaka wa kitaifa kabla ya kwenda kwenye kura ya maoni ya Katiba Pendekezwa ni suala la maadili, madaraka ya Rais, mambo ya uchaguzi na muundo wa Muungano.
Amesema mambo hayo yasipopata mwafaka itakuwa vigumu kwa Katiba Pendekezwa kuridhiwa na wananchi.
Jaji Warioba amesisitiza: “Katiba ni ya wananchi si ya viongozi, wananchi wanapaswa kusikilizwa wanachokitaka.”
Warioba amesema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi Aprili 5, 2024 yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam, yakihusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kisiasa, kijamii, kiuchumi, kielimu na utawala bora.
Jaji Warioba ameeleza suala la Katiba ikiwa ni siku chache tangu Rais Samia Suluhu Hassan kugusia kwa mara nyingine juu ya mchakato uliokwama mwaka 2014.
Mchakato huo uliokwama ulikuwa umefikia hatua ya kupatikana kwa Katiba Pendekezwa, licha ya kutumia mabilioni ya fedha za walipakodi, haukuendelea na tangu wakati huo kumekuwa na danadana za kuuhitimisha.
Aprili 4, 2024 Rais Samia alitumia sehemu ya hotuba yake akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua akiwemo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini aliyemtaka kwenda kushirikiana na waziri wake, Dk Pindi Chana kushughulikia suala hilo.
Katika maelekezo yake kwa Sagini, aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Rais Samia alimtaka kutumia uzoefu wake serikalini kumsaidia waziri, Dk Chana kuiendesha wizara hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na madai ya Katiba mpya.
“Wewe ni mzoefu sana serikalini, umefanya kazi maeneo mengi, nenda kasaidie kwenye Katiba na Sheria. Katika kipindi hiki watu wanadai Katiba yao kwa hiyo nenda kasaidiane na waziri naamini utafanya vizuri,” alisema Rais Samia.
Moja ya swali aliloulizwa Jaji Warioba katika mahojiano hayo ni mwendelezo wa Rais Samia kuzungumzia uhitaji wa Watanzania kupata Katiba mpya akisema, mijadala na mashauriano inapaswa kuendelea hadi 2025.
Amesema katikati ya mijadala hiyo, mambo manne ni machache lakini yana uzito wake kutokana na wananchi wengi kuyatolea maoni.
Mambo makuu manne
Jaji Warioba amesema kabla ya kuamua kuhusu Katiba mpya, kuwe na majadiliano kwenye masuala manne, yaliyozungumziwa kwa uzito na wananchi wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilipokuwa inakusanya maoni.
Akichambua mambo hayo, alianza na maadili, akisema wananchi walisema yameporomoka kwa jamii na viongozi.
"Wakataka liwekwe kwenye Katiba, halikuwa suala rahisi kuona Katiba inakuwa na vifungu vya kushughulikia maadili, Tume iliweka vifungu kwa kuwa ili kujenga maadili lazima tuwe na misingi imara.
"Kikawekwa kitu kinaitwa tunu za Taifa, ambayo inajenga utamaduni wa maadili kwa kuzingatia utu, usawa, uzalendo, uadilifu, uaminifu na kuenzi lugha yetu ambayo inatuunganisha,” amesema na kuongeza:
"Tukasema ili tuwe na msingi huu, inabidi kuwepo utaratibu wa kuzisimamia, tuwe na misingi ya uongozi, ukiingia kwenye uongozi lazima uifuate misingi hiyo na miiko ya uongozi, kuwe na chombo ambacho kitasimamia misingi hiyo kwa sababu hivi sasa katika Katiba hakipo."
Jambo la pili lililozungumzwa zaidi na wananchi kwa mujibu wa Jaji Warioba ni mamlaka ya utawala, akisema namna wananchi walivyolizungumzia hilo kwa uzito na kueleza ni muhimu kuimarisha mihimili ya dola.
"Walitaka kuwe na Serikali ambayo ina uwezo wa kutekeleza mambo ya nchi, kuwe na Bunge huru ambalo linaweza kuisimamia Serikali na Mahakama yenye kutoa haki,” amesema.
Amesema wananchi walisema ili kila chombo kitekeleze wajibu wake pasi na kuingilia kingine: "Bunge liwe ni Bunge, Serikali isiwe sehemu ya Bunge na wakasema ni vizuri mawaziri wasiwe wabunge, kila mhimili ufanye kazi yake kwa uhuru.”
"Mahakama iwe huru na ipewe uwezo na tukasema hata muundo wake uongezewe iwe na Mahakama ya Juu ya Mahakama ya Rufani na pia ipate uwezo, madaraka kamili ya kusimamia fedha zake,” amesema.
Kuhusu Serikali, amesema walitaka Katiba mpya kuangalia madaraka na mamlaka.
Ametoa mfano baada ya Uhuru, Desemba 9, 1961, ilipobadilishwa Katiba ikawa Jamhuri, wakati huo Rais alikuwa na madaraka makubwa.
"Kulikuwa na sheria zinampa madaraka ya kuwatia watu kizuizini bila kupitia utaratibu wa Mahakama, alikuwa na uwezo wa kuwahamisha watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine.”
"Alikuwa na madaraka ya kuteua maofisa wengi sana. Hata baadhi ya wakurugenzi mwanzoni waliteuliwa na Rais, jinsi ilivyoenda ilionekana utaratibu huu unahitaji kuangaliwa,” amesema.
Amesema Rais wa wakati ule, Mwalimu Julius Nyerere alianza kuangalia utaratibu mpya, Serikali ilijenga taasisi zake, jeshi, polisi, idara ya usalama zikawa imara na baada ya hapo ikaonekana hakuna haja ya Rais kuwa na madaraka ya kuweka watu kizuizini kwa sababu unakuwa na taasisi zinazofanya kazi hiyo.
"Hivyo, kama una taasisi hizo, maana yake Polisi au Jeshi, au Usalama kama kuna dalili zozote mtu anataka kuhatarisha amani wao wanashughulikia, polepole Rais akaacha kuwaweka watu kizuizini," amesema Jaji Warioba ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Amesema Mwalimu Nyerere mwishoni alipokaribia kutoka madarakani (alitoka mwaka 1985) hakuwatia watu kizuizini, na hadi alipoondoka hakukuwa na mtu kizuizini. Waliofuata hawakutumia madaraka hayo.
"Kwenye upande wa uteuzi, Rais mwenyewe alisema ameteua watu wengi ambao hawafahamu, wala hawasimamii, nidhamu yao pia haisimamii, akaona kwa utaratibu huu kulikuwa na hatari ya kuteua watu ambao hawana sifa au uwezo wao hata kuingia dalili za rushwa.”
"Kwa kuwa ni Rais anayeteua mapendekezo na watu wengi, inawezekana mtu akamhonga kiongozi fulani ili ampigie debe au ana jamaa yake anaenda kumpigia debe. Rais akasema hapana, yeye atateua watu ambao atakuwa anafanya nao kazi, anawafahamu, ikaamuliwa atakuwa anateua watu wa juu," amesema.
Katika hilo, Jaji Warioba amesema Mwalimu Nyerere alisema atakuwa anateua waweka sera kwa tafsiri ni mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya: “Hawa ndio wanasimamia sera.”
Wengine ni maofisa wakuu wanaosimamia utendaji na hao ni makatibu wakuu, naibu wao, wakuu wa mashirika, mabalozi na viongozi wa juu wa ulinzi na usalama: “Wengine wote, watakuwa chini ya taasisi zao.”
Amesema tangu wakati huo huwezi kusikia Rais ameteua kamanda wa Polisi wa mkoa (RPC) bali kwa sasa Rais akishamteua Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Mkuu wa Majeshi (CDF) na wengine nao wanapanga safu zao.
“Madaraka yale ya Rais yakapunguzwa lakini baadaye madaraka hayo yakarudishwa, sasa katika mjadala ilikuwa ni kupunguza madaraka haya ya Rais,” amesema.
Jaji Warioba aligusia Baraza la Mawaziri, akisema wakati huo kulikuwa na mjadala ambao uliongozwa na Rais mwenyewe.
"Nakumbuka hili vizuri, miaka ile ya mwisho alitutuma mimi na (Pius) Msekwa kwenda nje kujifunza uzoefu wa nchi nyingine, alisema hasa mwende Ufaransa, akasema (Mwalimu Nyerere) tumesikia kule Rais ana madaraka na waziri mkuu ana madaraka.”
"Tulienda wakatueleza wao Rais ndiye mkuu wa nchi na sera zake ndizo zinatekelezwa, uamuzi wa sera ni wake, pia anashughulikia na mambo ya ulinzi,” amesema.
Amesema mambo ya maendeleo, uchumi na jamii yalikuwa mikononi mwa waziri mkuu kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo wakati huo, na Rais wao ndiye aliunda baraza la mawaziri kwa kushauriwa na waziri mkuu.
"Lakini maana yake ilikuwa waziri mkuu ndiye anayeunda baraza kisha Rais anaenda kuidhinisha, hivyo tuliona tusingeweza kuchukua mfumo huo.”
"Hapa kwetu wakati ule, waziri mkuu haikuwa awe mbunge wa kuchaguliwa, kwani mawaziri wakuu nikiwamo mimi (Warioba) hatukuwa wabunge, Rais aliteua na kukufanya waziri mkuu,” amesema na kuongeza:
“Tuliona haitatusaidia kwamba waziri mkuu ndiye aunde Serikali, Rais ataendelea kuunda baraza la mawaziri ila ashauriane na waziri mkuu kwa kuwa ndiye atakuja kuwasimamia kiutendaji,”amesema Jaji Warioba.
Amesema wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba inakusanya maoni: “Madaraka yale yalikuwa yamepanulia kwamba Rais anateua watu wengi sana mpaka kufika wilayani, atateua mkuu wa wilaya, katibu tawala wa wilaya, mkurugenzi wa halmashauri.”
“Hili nalo bado ni suala. Je, Rais abaki na madaraka haya ama tuwe na utaratibu unaosambaza mamlaka kwa baadhi ya taasisi? Hilo nalo ni eneo jingine ambalo majadiliano ya Katiba mpya yakianza lazima lijadiliwe," amesema.
Amesema lililozungumzwa zaidi na wadau wa siasa ni mambo ya uchaguzi, juu ya mazingira yanayowezesha uwepo wa uchaguzi akisema licha ya sheria tatu zilizopitishwa na Bunge hivi karibuni, lakini ni miongoni mwa mambo yanayohitaji mjadala mpana.
Jaji Warioba amesema la nne ambalo limezungumzwa kwa zaidi ya miaka 30 ni la Muungano, ambalo lilizungumzwa na Tume ya Nyalali, G55, Tume ya Kisanga na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Kwa kipindi chote, mazungumzo ni juu ya muundo wa Serikali na baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukabidhi taarifa, suala kubwa lililozungumzwa na ambalo liligawa watu ni Muungano; bado Muungano ni imara, lakini tatizo na hili linabidi liangaliwe na kuzungumzwa kufikia uamuzi,” amesema.
Amesema Katiba mpya ikishapitishwa kuna suala la kura ya maoni, hivyo uamuzi wa pamoja na masuala hayo manne ni muhimu.
“Mambo kama haya mashauriano yaendelee ili tukimaliza uchaguzi 2025 tuwe kwenye hatua ya kuikamilisha tufikie uamuzi kwani kwenye Rasimu maeneo hayo manne ndiyo makubwa katika suala la Katiba mpya, ni machache lakini yana uzito wa pekee," amesema.
Katiba ni ya wananchi
Alipoulizwa suala la Katiba mpya linaweza kuamuliwa na utashi wa kisiasa kwa viongozi, hususani chama tawala na wale wa upinzani kuongoza mchakato huo, Jaji Warioba amesema wananchi ndio wenye kuamua na wanapaswa kusikilizwa.
“Suala la Katiba ni la wananchi, hawa viongozi wa Serikali na vyama vya upinzani, hawa ni viongozi wazingatie maoni ya wananchi si utashi wa viongozi bali wanapaswa kuona hali halisi wananchi wanataka nini,” amesema.
Amesema kwa hali ya sasa mambo yanafanyika kwa kuona kiongozi anataka nini kifanyike na si wananchi wanataka nini.
Amesisitiza viongozi wanaoongoza wananchi wana kila sababu kuwasikiliza na kufanyia kazi kile wanachokitaka.
“Ukiwa kiongozi unapopanga maendeleo ni kwa ajili ya wananchi si kwa sababu ya viongozi, kama unataka kuwe na umoja, amani na mshikamano lazima ufanye uamuzi unaotokana na matakwa yao, usipofanya hivyo wananchi hawataithamini sana Serikali,” amesema.
Akerwa kutaja maendeleo kwa awamu
Jaji Warioba ameonyesha kukerwa na watu wanaochukulia masuala ya utendaji wa Serikali na kuyaweka kwenye awamu za uongozi, akisema zamani walizoea kusikia Serikali imefanya hivi, kuanzia wakati Mwalimu Nyerere ilikuwa ni Serikali.
Amesema hilo liliendelea hata baada ya Mwalimu kung’atuka na kuingia Ali Hassan Mwinyi (1985-1995), Benjamin Mkapa (1995-2005)
“Lakini hapa katikati tukaanza kusema si Serikali ya nchi ni Serikali ya awamu, yaani inaonekana Serikali si ya nchi ni ya watu.”
“Serikali hii iliyopo mambo inayofanya yataenda kwenye Serikali inayokuja, kila kitu awamu ya tano, awamu ya sita na tatizo lake kama kila kitu unazungumzia Serikali iliyopo, madhara yake ikitoka, Serikali inayokuja ili ipate sifa inaanza kuua yale yaliyopita na hii haisaidii,” amesema.
Amesema ukiona maendeleo yaliyopatikana msingi wake ni huko nyuma.
“Serikali ipo wakati wote, iliyopo inayofanya itaunganishwa na inayofuata.
"Mfano tuchukulie hali yetu ya umoja na amani ilijengwa na Serikali wakati ule lakini ni ya msingi kwa nchi, kwa hiyo kila Serikali inayokuja inalinda umoja na amani, lakini wakati wote tungekuwa tunasema umoja na amani ni Serikali ya awamu ya kwanza,” amesema.
Amesema, "viongozi wanaweka legacy kwa masilahi ya nchi, yanayofanyika ni ya nchi si ya awamu, ni jukumu la viongozi wakati wote kwamba mambo tunayoyafanya ni ya wananchi, hata ukipanga maendeleo unapanga kwa ajili ya wananchi si kwa sababu ya viongozi," amesema.
Itaendelea kesho Jumanne ambapo Jaji Warioba anagusia uchaguzi ujao, nini kifanyike ili yasijirudie ya 2019, 2020 na angalizo kwa Serikali na vyama vya upinzani.