Jaji Chande aipa kongole AKU ikitimiza miaka 40

Muktasari:
- Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 40 ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande amesema, kimekuwa na kiwango kizuri katika utoaji wa elimu, ndio maana wahitimu wake wamefanikiwa kushika madaraka ndani na nje ya nchi.
Dar es Salaam. Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande amesema ndani ya miaka 40 ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), taasisi hiyo kimekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha na kuendeleza za sekta ya afya na elimu katika mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda.
Jaji Chande ameeleza hayo jana Machi 16, 2023 wakati wa maadhimisho ya kusheherekea miaka 40 ya AKU ambacho kipo pia katika mataifa ya sita ya Afrika Mashariki ikiwemo Kenya na Uganda.
Amesema AKU imekuwa na kiwango kizuri katika utoaji wa elimu, ndio maana wahitimu wake wamefanikiwa kushika madaraka katika taasisi mbalimbali ikiwemo nje ya Tanzania.
"Wanafunzi wake wana uwezo kwa mfano hapa taasisi ya elimu ya maendeleo iliyopo ndani ya AKU wanafunzi wake wenye shahada ya umahiri wa elimu ni viongozi katika sekta ya elimu katika mataifa ya Tanzania, Kenya na Uganda.
"Hii moja ya dira ya AKU ambapo inatoa wanafunzi watakaofundisha na kushika madaraka ili kusaidia sera za elimu na afya.Ni michango mizuri iliyofanywa AKU kwa miaka 40 ya uhai wake," amesema Chande.
Kwa mujibu wa Chande, AKU kipo katika mataifa sita ya Afrika Mashariki, pia kipo nchi za Uingereza, Pakistan na viwango vya elimu yake vipo juu ili mhitimu ili kuondoa dhana ya kwenda nje ya nchi kusoma.
Mkuu wa AKU, nchini Dk Eunice Pallangyo amesema miaka 40 ya taasisi hiyo ina maana kubwa na inawapa nafasi ya kutafakari yale yaliyofanyika ndani ya muda huo wakati wa utoaji huduma kwa wananchi.
"Tumefundisha wanafunzi wengi zaidi ambao wameshika nafasi za uongozi katika maeneo mbalimbali nchini.Elimu tunayoitoa ni zaidi ya kuweka wanafunzi darasani, uwezo wa kufundisha mwanafunzi na kuleta mapinduzi sehemu alipo ni msingi wetu pia," amesema Dk Pallangyo.
Chuo Kikuu cha Aga Khan inajishughulisha na utoaji wa elimu ya shahada ya uzamili ya elimu, udaktari bingwa na elimu ya ukunga na uuguzi.