Wanasayansi kushiriki ajenda ya nishati safi kwa kufanya tafiti

Kamishna Msaidizi wa Uchambuzi wa Sera kutoka Wizara ya Fedha Dk Remidius Ruhinduka, akizungumza na wadau wa mazingira ambao hawapo pichani leo Aprili 24, 2025 Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam.
Muktasari:
- Tafiti zinalenga kubaini namna Watanzania wanavyopokea mabadiliko ya matumizi ya nishati safi, hasa matumizi ya gesi ya kupikia (LPG) katika maisha ya kila siku.
Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikitekeleza mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia (2024-2034), wanasayansi wameingia kazini kuunga mkono ajenda hiyo kwa kufanya tafiti zenye ushahidi wa kisayansi.
Tafiti hizo zinalenga kubaini namna Watanzania wanavyopokea mabadiliko ya matumizi ya nishati safi, hasa matumizi ya gesi ya kupikia (LPG) katika maisha ya kila siku.
Hilo linaongozwa na Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kupitia Kituo cha Tafiti za Tabia (CBS), ikiwa ni hatua muhimu katika kuelewa mwitikio wa Watanzania kwa wito wa kimataifa wa matumizi ya nishati safi.
Mkakati wa kitaifa wa nishati safi ya kupikia unalenga kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuboresha afya za kaya kwa kuchochea matumizi ya nishati safi kama vile gesi na umeme.
Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kitaifa na kimataifa katika ajenda ya nishati safi ya kupikia.

Licha ya juhudi zinazofanywa na Serikali, ikiwemo usambazaji wa mitungi ya gesi kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), bado matumizi ya LPG ni ya chini, ikitajwa ni chini ya asilimia 15 ya kaya hutumia gesi mara kwa mara.
Mratibu wa CBS, Dk Innocent Pantaleo amesema hayo leo Aprili 24, 2025, akieleza awamu ya mwisho ya mradi wa tafiti itachukua miezi saba na itahusisha zaidi ya kaya 150 katika Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.
“Lengo letu ni kuzalisha ushahidi ambao unaweza kusaidia uamuzi wa kisera na kuisaidia nchi kufikia malengo ya nishati safi. Tunajikita katika kusaidia kaya kuachana na matumizi ya mkaa na kuni na kuelekea kwenye nishati safi kama LPG,” amesema.
Utafiti wa CBS kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Liverpool na taasisi kutoka Rwanda, Uganda, Kenya na Cameroon, umeonyesha ingawa baadhi ya kaya zinamiliki majiko ya gesi na mkaa, wengi bado hutegemea mkaa kwa upishi wa muda mrefu kutokana na mtazamo wa gharama.
“Tumeona kuwa familia nyingi hutumia gesi kupika mlo wa haraka, lakini kwa vyakula vinavyohitaji muda mrefu, wanatumia mkaa au kuni. Watu wanadhani gesi ni ghali, lakini hali halisi ni tofauti,” amesema.
Kupambana na dhana hiyo, CBS imeingia ubia na kampuni ya M-Gas Resources inayotumia mita za kisasa kuruhusu familia kulipia gesi kwa kiasi kidogo, mfumo unaofanana na ununuzi wa mkaa.
“Tatizo si bei ya gesi, bali ni gharama ya awali ya kununua jiko na mtungi,” amesema.
Utafiti huu unaoendelea katika awamu ya tatu na ya mwisho amesema unalenga kutoa takwimu halisi zitakazosaidia Serikali katika kutengeneza sera bora na mikakati ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Kamishna Msaidizi wa Uchambuzi wa Sera kutoka Wizara ya Fedha, Dk Remidius Ruhinduka amesema uongozi wa Rais Samia ni kiashiria cha dhamira ya dhati ya Taifa katika kuhamasisha nishati safi.
“Tunaamini katika sera zinazotokana na ushahidi wa kitaalamu. Tafiti kama hizi zinaongeza uzito wa hoja katika mabadiliko tunayoyataka,” amesema.
Wataalamu wanasema sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuchangia upatikanaji wa nishati safi.
Kwa sasa, M-Gas inafanya kazi katika baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam, lakini wanasayansi wanatarajia matokeo ya utafiti yatasaidia kupanua huduma nchini.
Mabadiliko ya matumizi ya nishati safi si suala la mazingira pekee, bali pia afya na maendeleo ya kiuchumi, hasa kwa wanawake na watoto wanaoathirika zaidi na moshi wa mkaa na kuni.