Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JAB kushusha rungu kwa waandishi waliotia nia wakiendelea na kazi

Muktasari:

  • Pia, imewataka waandishi wote wasiosajiliwa kupitia Mfumo wa Tai Habari kuacha kazi hadi wathibitishwe kisheria.

Dar es Salaam. Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeelekeza waandishi wa habari waliotangaza nia ya kugombea nafasi za kisiasa wasitishe mara moja shughuli zote za kihabari katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.

JAB imetoa maelekezo hayo leo, Julai 5, 2025, kupitia taarifa yake iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Patrick Kipangula, ikieleza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda uaminifu wa vyombo vya habari nchini.

Wakati JAB ikitoa maelekezo hayo, tayari baadhi ya waandishi wa habari wamechukua fomu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuomba ridhaa ya chama kugombea ubunge katika majimbo mbalimbali nchini na sasa wanasubiri mchujo na kura ya maoni.

Kipangula ameeleza katika taarifa yake kuwa bodi, kwa nyakati tofauti, imekuwa ikiwakumbusha waandishi wa habari kuzingatia kikamilifu masharti ya sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya habari.

“Hatua hii inalenga kuepusha mgongano wa kimaslahi, kulinda uaminifu wa vyombo vya habari na kuweka mazingira ya usawa kwa wagombea wote.

“Kuendelea kushiriki katika shughuli za kihabari wakati wa kipindi hiki ni ukiukaji wa Kanuni ya 12(g) ya Kanuni za Utangazaji wa Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa (Tangazo la Serikali Na. 775 la Septemba 18, 2020),” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, JAB imewaelekeza waandishi wote wanaofanya kazi katika vyombo vya habari vya kielektroniki au vya machapisho bila kusajiliwa na Bodi ya Ithibati, kuacha mara moja kufanya kazi hizo hadi watakapokamilisha usajili kupitia Mfumo wa Tai Habari.

“Kuendelea kufanya kazi pasipo kusajiliwa na bodi ni ukiukaji wa Kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023), ambacho kinakataza mtu yeyote kufanya kazi za kihabari bila kupewa ithibati,” imeelekeza taarifa hiyo.

Bodi imeeleza kuwa inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa waandishi wa habari wote nchini, na haitasita kuchukua hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwataja hadharani watakaobainika kukiuka masharti ya sheria, kanuni, na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.

Hata hivyo, Bodi imeeleza kuwa katika siku za hivi karibuni, imechukua hatua kwa baadhi ya waandishi wanaofanya kazi katika vyombo vya habari, ikiwa ni pamoja na kuwaondoa walioonekana au kusikika katika vipindi mbalimbali vya redio na televisheni, ambao wanavunja sheria na kwenda kinyume na maadili ya taaluma.

Kipangula amesema katika taarifa hiyo kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kwa waandishi wa habari wanaoendelea kufanya kazi za kihabari bila kusajiliwa na bodi kupitia Mfumo wa Tai Habari, na wale ambao wamejisajili, lakini wametangaza nia ya kugombea nafasi mbalimbali za kisiasa huku wakiendelea kushiriki katika shughuli za kihabari, kinyume na maadili ya taaluma.

“Katika kutekeleza mamlaka hiyo, na hususan kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, bodi katika nyakati tofauti imekuwa ikiwakumbusha waandishi wa habari kuzingatia kikamilifu masharti ya sheria, kanuni, na maadili ya taaluma ya habari,” amesema.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 13(a) na (b) cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023), JAB imepewa mamlaka ya kutoa ithibati kwa waandishi wa habari pamoja na kusimamia uzingatiaji wa maadili ya taaluma ya uandishi wa habari nchini.

Wakati CCM ikikamilisha hatua ya awali ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu, mchakato huo wa kuomba ridhaa ya kugombea ubunge na udiwani unaendelea katika vyama vingine huku watu wa aina tofauti wakijitokeza.