Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ijue historia ya pasaka na maana yake

Askofu mstaafu Method Kilaini

Muktasari:

  • Historia ya Pasaka inatokana na historia ya Wayahudi. Katika Pasaka, Wayahudi waliadhimisha ukombozi wao kutoka utumwa wa Misri. Siku hizo waliadhimisha jinsi walivyotoa sadaka ya mwanakondoo kupaka damu yake milangoni mwao.

Tunaambiwa Pasaka ndicho kilele cha mwaka wa Wakristu kwa sababu waamini wa dini ya Kikristu huadhimisha ukombozi wao. Wanaadhimisha kifo na ufufuo wa Mwokozi na Mungu wao, Yesu Kristu.

Historia ya Pasaka inatokana na historia ya Wayahudi. Katika Pasaka, Wayahudi waliadhimisha ukombozi wao kutoka utumwa wa Misri. Siku hizo waliadhimisha jinsi walivyotoa sadaka ya mwanakondoo kupaka damu yake milangoni mwao.

Malaika wa bwana alipopita akiua wazaliwa wa kwanza wa Wamisri, alipokuta damu mlangoni mwa nyumba aliiruka asiwaue. Baada ya hapo mtawala wa Misri akaona Mungu wa Wayahudi ana nguvu sana akawaachia waende. Siku hiyo Wayahudi waliisherehekea kila mwaka. Wakati huo walisherehekea vilevile muujiza wa kuvuka Bahari ya Sham, maji yalipojitenga wakapita pakavu, lakini Wamisri walipojaribu kuwafuata wawateke upya maji yakarudi yakawaangamiza.

Wakati wanajitayarisha kuadhimisha sherehe hii ndipo walipomshika Yesu na kumuua na siku moja baada ya Pasaka akafufuka katika wafu. Kwa sababu hiyo Pasaka ya Wayahudi na Pasaka ya Wakristu zikaenda sambamba.

Toka mwanzoni baada ya kujitayarisha kwa siku 40 za mafungo (Kwaresma), Wakristu wanaadhimisha pamoja Ijumaa Kuu na Pasaka.

Mwanzoni waliviadhimisha pamoja kwenye siku ileile ya Pasaka ya Wayahudi. Polepole Wakristu walijitofautisha na Wayahudi, wakawa wanaadhimisha Pasaka Jumapili, baada ya Pasaka ya Wayahudi kwa sababu Kristu alifufuka siku moja baada ya Pasaka ya Wayahudi, ni wakati huo ndipo walipogeuza na siku yao ya mapumziko na kusali kutoka Jumamosi (Sabato) na kuwa Jumapili (Domenika au Siku ya Bwana).

Siku ya Ijumaa Kuu ilianza kusherehekewa peke yake kwa nguvu mwaka 325, baada ya Mtakatifu Helena kuchimbua msalaba wa Kristu na Mfalme Kaizari Kostantino kushinda vita akitumia msalaba kama alama yake kwenye ngao na bendera zote.


Huadhimishwa lini?

Wayahudi mpaka mwaka 70 BK (Baada ya Kristu) waliadhimsiha siku ya Pasaka siku ya 14 ya mwezi wa Nisan. Ikimaanisha waliadhimisha baada ya mwezi mpevu wa “Vernal Equinox”, yaani tarehe 21 Machi.

Baada ya nchi ya Wayahudi na Yerusalem kuharibiwa na Roma Wayahudi walipoteza mwelekeo wa Pasaka. Wakristu walijiweka sawa mwaka 325 katika Mtaguso Mkuu wa Nicea (huu ndio mkutano wa maaskofu wote duniani) walipoamua kwamba Pasaka itakuwa kila mwaka Jumapili baada ya mwezi mpevu wa equinox, yaani baada ya tarehe 21 Machi.

Mwezi mpevu huu huweza kutokea kati ya tarehe 21 Machi hadi 18 Aprili, hivyo Pasaka huweza kuadhimishwa kati ya tarehe 22 Machi hadi 25 Aprili. Kwa mfano mwaka 1818 iliadhinishwa tarehe 22 Machi na itatokea tena mwaka 2285; na tarehe ya mwisho yaani 25 Aprili ilikuwa mwaka 1943 na itatokea tena mwaka 2038.


Ishara za Pasaka

Kutokana na historia ya Wayahudi, Kristu hulinganishwa na sadaka ya mwanakondoo aliyechinjwa hivyo ‘mwanakondoo’ huwa ishara ya Pasaka na Kristu huitwa “Mwanakondoo wa Mungu”.

Katika tamaduni za Ulaya na Asia kipindi hiki huwa kipindi cha uhai (Spring), kipindi cha kuzaa hata walikiweka chini ya mungu Estre ndiyo sababu ‘mayai’ huwa ishara ya Pasaka hata na ‘sungura’ kwa sababu huzaa sana.


Matayarisho na ibada

Wakristu hujitayarishia sikukuu hii kwa siku 40 za mafungo wakifuasa mfano wa Bwana wetu Yesu Kristu alifunga kwa siku 40. Hiki ni kipindi cha kusali, kufunga na kufanya matendo mema.

Juma la mwisho ambalo huwa Juma Takatifu, Wakristu wanaanza na sherehe ya matawi, Bwana alipoingia kwa shangwe Yerusalemu. Watu walimpokea wa shangwe wakitandaza mavazi yao na kupeperusha matawi ya mizeituni.

Alhamishi Kuu wanaadhimisha siku alipoweka daraja na sakramenti ya upadri. Siku hiyo mapadri hurudia ahadi zao za ukuhani. Vilevile huadhimisha alipoweka sakramenti ya Ekaristu Takatifu, mwili na damu yake. Huadhimisha upendo na huduma ambapo padri anamuiga kwa kuosha miguu ya waamini 12. Hii inamaanisha kwamba ukubwa ni kuhudumia kwa unyenyekevu na upendo.  Ijumaa Kuu huwa siku ya kumwabudu Kristu aliyesulubiwa msalabani. Siku hiyo hakuna misa au adhimisho lingine, bali kuutukuza msalaba na kushiriki mateso ya Bwana. Siku hiyo hutolewa sala maalumu kuwaombea watu wote hata wale wasioamini, kuiombea Serikali, wagonjwa, wenye shida na waamini wote.

Jumamosi usiku na Jumapili huadhimisha sherehe ya Pasaka. Usiku huwashwa mshumaa wa Pasaka ukimwonyesha Kristu kama mwanga wa kweli wa dunia. Mara nyingi huwa na ubatizo hasa wa watu wazima.


Umuhimu wa Pasaka kwa Wakristu

Katika imani hii ni kumbukumbu kubwa ya Kristu aliyekufa na kufufuka. Wakristu walishinda mapingamizi mengi na kudumu hadi leo katika imani hii.

Kwa mfano kwa nguvu za Kristu mfufuka Wakristu waliishinda dola kubwa ya Warumi iliyokuwa na nguvu sana na ilisambaa katika ulimwengu mzima wa siku hizo katika Bara la Ulaya, Afrika na Asia, ilipiga vita sana dini ya Kikristu, ikawaua watu wengi kwa ukatili mkubwa kwa kuwasulubisha msalabani kama Mtakatifu Petro, kuwatupa katika uwanja wenye wanyama wakali kama simba na chui wenye njaa na kuliwa na wanyama hao kama Mtakatifu Ingatius na Felicita na Perpetua, kuwakata vichwa kama Mtakatifu Paulo, kuwakaanga kama Mtakatifu Yohana nakadhalika.

Walifanya hivyo kwa muda wa karne tatu, lakini wakashindwa kwa sababu kadiri walivyokufa kwa imani wakiimba ndivyo kadiri walivyoongezeka. Dola mwishowe ikamwongokea Mungu kupitia Mfalme Kaizari Kostantino. Imekuwa hivyo hadi nyakati zetu mashahidi wa Uganda na Kongo wakiwa mfano hai. Wanashinda si kwa nguvu za silaha za vita, bali kwa nguvu ya imani yao katika Kristu mfufuka. Kama alivyoiita Mfalme Kaizari Kostantino hii ni dini ya wasiokufa.

Wote tunaomwaini Kristu tunajua kwamba Kristu alishinda kifo na kila anayemwamini ni mshindi kwa sababu hakuna kinachoweza kumbabaisha au kumyumbisha.

Katika ufufuko sote tuko washindi, wadogo kwa wakubwa, wake kwa waume, watoto kwa wazee, matajiri kwa maskini, wazima kwa wagonjwa, walio huru kwa wafungwa bila kujali kabila, rangi, jinsia, kimo, akili au tofauti yoyote ile. Yeyote atakayemwamini Kristu kwamba amekufa na kufufuka, akafuata nyayo zake ataokoka, hatakufa bali hata akifa atafufuka na kuwa hai milele yote.

Kristu mwenyewe anatuasa kwamba: Jn. 12:24-25: “Amin Amin nawaambia, chembe ya ngano isipoanguka chini ikafa, hukaa hali hiyo hiyo peke yake; bali ikifa hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha.”

Kufa na Kristo ni kufa kwa mambo ya ubinafsi, ni kufa kwa dhambi, ni kufa kwa maovu yote, ni kufa kwa tamaa mbaya ili tufufuke naye katika wema, katika upendo na katika utakatifu na mwisho wa siku tuwe naye katika uzima wa milele.

Hivyo tufuate anavyotuelekeza (Lk. 9:23-26}) “Mtu yeyote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku anifuate”. Hii kazi si ya siku moja au mara moja, bali ni kazi ya kila siku katika kumfuasa Kristu.

Ninawatakia kila la heri katika sherehe ya Kristu mfufuka. Kristu amefufuka kweli kweli aleluya aleluya.


(Makala haya yameandaliwa na Askofu Method Kilaini)