IGP Wambura aanza kwa kupokea kilio

Muktasari:
- Mikakati ya kulisuka upya Jeshi la Polisi imepata msukumo zaidi baada ya mkuu wa taasisi hiyo kuweka bayana kuwa miongoni mwa vipaumbele vyake ni kulinda na kuheshimu haki.
Dar es Salaam. Wakati famili tano zilizopotelewa na watoto wao maeneo ya Kariakoo katika mazingira ya kutatanisha, wametoka tena hadharani safari hii wakimuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura kuwasaidia kuwapata vijana wao, kamanda huyo amekiri kulipokea jambo hilo na kuahidi kuwasilikiza.
Akizungumza na Mwananchi juzi, IGP Wambura alisema; “nimesikia kilio chao na wakija nitawasikiliza na kulifanyia kazi suala lao kwa kuwa dhamira yetu ni kuhakikisha haki ya kila mmoja inalindwa.”
Wambura ameshika wadhifa huo, Julai 20 mwaka huu, baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, akichukua nafasi ya Simon Sirro aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe.
Hadi jana Jumatatu ni siku 211 zimepita tangu vijana hao walipotoweka katika mazingira ya kutatanisha Desemba 26 mwaka jana eneo la Kamata, Kariakoo jijini Dar es Salaam wakati wakiwa njiani na gari yao wakienda ufukweni Kigamboni kusherekea sikukuu ya Krismas.
Vijana hao waliopotea ni Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe.
Mashuhuda walidai tukio la kutekwa kwao lilitokea majira ya 11 jioni ambapo watu watatu waliokuwa wamevalia nguo zinazodaiwa za askari wakiwa katika Bodaboda waliisimamisha gari waliyokuwa wamekaa kisha kubadili muelekeo wa safari na kuondoka nao.
Wakizungumza juzi na Mwananchi miongoni mwa wazazi hao akiwemo mzazi wa Edwin Kunambi alisema ndoto za kuwapata vijana hao zilishapotea kwani waliangaika sehemu zote lakini hawakupata ushirikiano kutoka kwa taasisi hiyo huku wakieleza ujio wa Mkuu mpya wa Polisi unaweza kurudisha tabasa kwao kwa kuwasaidia kupatikana.
Walichokisema
“Tangu kupotea kwa vijana wetu tumehangaika kuwatafuta kwenye vituo vya Polisi na kwenda mamlaka zingine na tumefanya vikao na wenzangu lakini bado hatujafanikiwa na Polisi hawatupi ushirikiano tunaamini Mkuu mpya wa Polisi anaweza kutusaidia kupatikana watoto wetu,”alisema Mzazi huyo
Alisema kwa namna watu wanavyozungumzia wasifu wake vizuri na wakizingatia msiamamo wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni muumini wa haki wakati wote wanaamini watapata ushirikiano waliokuwa wameokosa na kujua waliko vijana wao.
Naye Sylvia Quentin ambaye ni Mama mzazi wa Tawfiq Mohamed alisema juhudi zote walizofanya kuzunguka kuwatafuta hazijazaa matunda huku akieleza mara ya mwisho walipoenda Polisi walielezwa kwamba jalada lao limeenda Dodoma.
“Kila tukifuatili kujua kinachoendelea hawatupi majibu, ndipo tulienda hadi Ikulu Dar es Salaam tukaelekezwa kwenda kwa Waziri wa Mambo wa Ndani lakini hadi sasa hatujapata msaada zaidi ya kuzungushwa,” alisema
Alisema wajukuu zake wanamsumbua muda wote kumuulizia aliko baba yao na anakosa majibu ya kuwapa kwa kuzingatia mazingira na namna walivyopotea.
Hata hivyo Kelvin Yohana ambaye ni rafiki wa vijana hao na walikuwa wanafanya kazi pamoja ya kuuza simu Kariakoo hakusita kuonesha masikitiko yake kwa kutokuonekana kwa vijana wenzake huku akiomba mamlaka kusaidia kutegua kitendawili cha kupatikana kwao.
“Bado tuko njia panda kama unavyojua mtu uliyejuana naye anapotea ghafla katika mazingira ya kutatanisha na tulikuwa tunafanya mipango mingi lakini hadi tunazungumza hapa hatuelewi huwezi kuwa na furaha,”alisema
Visa vya Polisi
Januari 26, Mwananchi liliandika taarifa ya maofisa saba wa Jeshi la Polisi, kushikiliwa na jeshi hilo mkoani Mtwara kwa tuhuma za kumpora mfanyabiashara mmoja wa madini Sh70 milioni na kisha kudaiwa kumuua kwa kumchoma kwa sindano ya sumu na kuutupa mwili wake baharini.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Mark Njera alisema jana kuwa tukio la mauaji lilitokea Januari 5 baada ya Hamis (Mussa) kufuatilia fedha zake zilizochukuliwa na maofisa wa polisi.
Oktoba 17, 2021 dereva wa lori Ibrahimu Saidi (35) alifariki dunia mkoani Lindi baada ya kupigwa risasi na askari baada kumgonga askari mmoja na kudaiwa kutaka kupora bunduki mwingine.
Mei 31, 2021 askari polisi wa Wilaya ya Mwanga anadaiwa kumuua askari mwenzake wa kitengo cha upelelezi aliyetambulika kwa jina moja la Linus.