Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hospitali ya Mawenzi yapewa vifaa vyaSh217 milioni kuwanusuru watoto wachanga

Wakati Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi ikikabiliwa na ongezeko kubwa la watoto wachanga, hasa wale wanaozaliwa kabla ya kufikia muda kamili wa ujauzito (njiti), Mpango wa NEST360 kwa kushirikiana na Wizara ya Afya umekabidhi vifaa tiba na wodi maalumu zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 217.

Takwimu zinaonyesha ongezeko kubwa la watoto wachanga wanaopokelewa hospitalini hapo, kutoka 393 mwaka 2022 hadi kufikia 823 mwaka 2024, wengi wao wakiwa na changamoto mbalimbali za kiafya.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo, yaliyofanyika Julai 3, 2025, Kiongozi wa Mpango wa NEST360 nchini, Dk Honarati Masanja, amesema vifaa vilivyotolewa ni pamoja na chumba cha watoto njiti (Kangaroo Mother Care – KMC), chumba cha kutenga watoto wenye magonjwa ya kuambukiza (Isolation Room), pamoja na vifaa tiba vya kisasa vyenye teknolojia muhimu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto wachanga.

Amesema, NEST360 inaendelea kushirikiana na hospitali za mikoa na wilaya ili kuhakikisha huduma hizo zinawafikia watoto wachanga zaidi ya 483,000 wanaohitaji matibabu ya hospitali kila mwaka.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto katika hospitali hiyo, Dk Jonas Kessy, amesema awali hospitali hiyo ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya msongamano mkubwa wa watoto wachanga kutoka wilaya mbalimbali za mkoa huo.

"Watoto wengi wanaopokelewa ni njiti au huzaliwa wakiwa na matatizo ya kiafya, ikiwemo kushindwa kupumua pindi tu wanapozaliwa," amesema Dk Kessy.

Amebainisha kuwa ongezeko la watoto kutoka 393 mwaka 2022 hadi 823 mwaka 2024 linaonyesha hali bado ni changamoto, na akaishukuru NEST360 kwa msaada walioutoa unaolenga kuboresha huduma za watoto wachanga.

Naye, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Kilimanjaro, Fatina Rashid, amesema vifaa na ukarabati wa wodi hiyo utasaidia kupunguza msongamano uliokuwepo awali katika hospitali hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amesema kupitia programu hiyo, mkoa huo unatarajia kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto wachanga.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu akiwa ameambatana na wataalam mbalimbali wa afya wakati walipokuwa  wakikagua chumba maalumu cha watoto wachanga katika  hospitali ya Rufaa ya Mkoa,  Mawenzi.

"Ni matumaini yangu kuwa mkoa huu utaongoza kwa kupunguza vifo vya watoto kupitia mradi huu wa NEST360," amesema Babu.