Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hizi hapa sababu viongozi Mataifa makubwa kupishana Afrika

Rais wa Ujerumani Frenk-Walter Steinmeier akipokea ua baada ya kuwasili Tanzania.

Dar es Salaam. Bara la Afrika limeonywa kuhusu kushamiri kwa ziara za viongozi wa mataifa makubwa kuja barani Afrika ikielezwa kuwa zinalenga kuwa wanalenga kujinufaisha.

Kwa nyakati tofauti, viongozi wa mataifa ya Ulaya na Marekani wamekuwa wakizunguka nchi mbalimbali barani Afrika kwa ziara zenye lengo la kuimarisha ushirikiano na mataifa husika, ikiwemo kwenye biashara.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa wamebainisha kwamba licha ya kuwa ziara hizo zina manufaa kwa Afrika, viongozi wake wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa kuwa ujio wa viongozi hao unalenga kutafuta fursa zitakazowanufaisha wao.

Oktoba 30, Rais wa Ujerumani, Dk Frank-Walter Steinmeier alianza ziara nchini ambapo alikutana na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan kwa mazungumzo na kukubaliana juu ya masuala mbalimbali.

Wakati akiendelea na ziara hapa nchini, Mfalme Charles III wa Uingereza naye alikuwa kwenye ziara ya siku nne nchini Kenya, lengo likiwa ni kuendeleza ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili.

Machi mwaka huu, Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris alifanya ziara yake hapa nchini yenye lengo la kuimaisha ushirikiano baina ya Tanzania na Marekani. Mbali na Tanzania, Kamala alitembelea pia mataifa ya Ghana na Zambia.

Julai 17, mwaka huu, Rais wa Hungary, Katalin Novak, alifanya ziara ya siku nne nchini.

Mbali na viongozi hao wa Ulaya na Marekani, baadhi ya viongozi wa Asia pia wanafanya ziara zao kona mbalimbali za Afrika wakitafuta ushawishi katika bara hili, kama wanavyofanya wenzao wa Magharibi. Agosti 21, 2023 Tanzania ilipokea ugeni wa Rais wa Indonesia, Joko Widodo aliyefanya ziara ya siku mbili kabla ya kuelekea Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa mataifa yanayokua kiuchumi (Brics).

Rais wa China, Xi Jinping naye Agosti 23, mwaka huu alitembelea Afrika Kusini kwa ziara ya kiserikali sambamba na kuhudhuria mkutano wa Brics uliowakutanisha na viongozi mbalimbali wa Afrika.

Kadhalika, Rais wa Ureno, Marcelo Rebelo de Sousa alifanya ziara Afrika Kusini Juni 15, mwaka huu.

Septemba, 2023, Waziri Mkuu mstaafu wa Sweden, Stefan Löfven naye aliitembelea Rwanda kwa ziara ya siku tatu.

Ziara kama hiyo, ilifanywa Oktoba 5, mwaka huu na Naibu Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohamed bin Abdulrahman Al Thani kwa siku mbili.

Japan nayo haiko nyuma, kati ya Aprili 19 hadi Mei 5, 2023, Waziri Mkuu wake, Kishinda Fumio alitembelea Misri, Ghana, Kenya, Msumbiji na Singapore.

Machi, mwaka huu, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alifanya ziara katika mataifa ya Gabon, Angola kisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akizungumzia ziara za viongozi wa Ulaya, Marekani na Asia, mhadhiri wa uhusiano wa kimataifa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Muhidin Shangwe alisema ziara za viongozi hao ni fursa kwa bara la Afrika.

Fursa hizo zinatokana na kile alichokieleza kuwa ni Afrika kuwa na machaguo mengi ya washirika wa mambo yake, tofauti na zamani ambapo haikuwa na nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa Dk Shangwe, viongozi hao wanaitembelea Afrika kutokana na wingi wa fursa, rasilimali na umuhimu wa bara hilo kwa ujumla.

“Bara la Afrika linatambulika kama bara la vijana maana idadi kubwa ya watu wake ni vijana, hivyo hakuna eneo unaloweza kupata nguvu kazi ya kutosha kama Afrika, ndiyo maana wanakuja,” alisema.

Dk Shangwe alisema zipo pia sababu za kisiasa zinazowashawishi viongozi hao wapishane kufanya ziara katika mataifa ya Afrika, kwa kuwa bara hilo ni mtaji wa kura kwenye vyombo vya uamuzi hasa wanapohitaji kushinikiza jambo katika jumuiya ya kimataifa, akisisitiza kuna kura 54 za mataifa ya bara hili.

“Utakumbuka hivi karibuni,

kulikuwa na ushawishi kwa nchi za Afrika kupiga kura za kuikataa Urusi hili lilikuwepo, kwa hiyo sababu kama hizi zinawafanya viongozi hao wazuru Afrika kujenga mtaji wa kisiasa katika jumuiya za kimataifa,” alisema.

Hata hivyo, alisema ujio wa viongozi hao ni ishara kwamba Tanzania imerejesha hadhi yake kutoka enzi zile za ukoloni.

Kwa kiasi kikubwa, alisema baada ya ukoloni kulikuwa kama kuna vita baridi kati ya Afrika na mataifa hayo, kwani hayakuona tena haja ya kuendelea kushirikiana na bara hilo.

“Baada ya ukoloni, kulikuwa ni kama kuna vita baridi hivi, mataifa mengi ya nje ya Afrika hasa yale yaliyoitawala hayakuona umuhimu wa kurudi. “Kwa sababu walikuwa wanaitumia Afrika kwa masilahi yao binafsi, wengi waliona kwa nini waendelee kuwepo ilhali hawana cha kufuata. Tunapoona ziara zao maana yake wameanza kuona umuhimu wa bara hili,” alisema.

Dk Shangwe alisema wingi wa ziara hizo hasa katika miaka ya hivi karibuni, unachagizwa na ushindani wa mataifa tajiri duniani.

Kwa kawaida, alisema viongozi wa nchi zilizoendelea hasa zile zilizowahi kuitawala Afrika ndiyo wanaofanya ziara zaidi, lakini kwa sasa kumezuka ushindani dhidi yao kutoka mataifa ya Asia.

Dk Shangwe alisema kuna nchi kama Falme za Kiarabu, China na nyingine zinatembelea Afrika kujenga ushirika zikishindana na zile zilizowahi kuitawala.

“Na kuna dalili kwamba zile nchi zilizowahi kuitawala Afrika zinaona kama zinapoteza ushawishi, ndiyo maana unaona kuna ushindani wa ziara za kujenga uhusiano.

“Kwa sababu hawa wapya nao wana fedha na wanataka kilekile ambacho wale wengine wanataka, kwa hiyo ushindani unafanya viongozi hawa wapishane,” alisema

Kwa upande wa Mhadhiri wa Sayansi ya siasa kutoka UDSM, Dk Kelvin Munisi alisema Afrika inapaswa kuchukua tahadhari kwa kuona namna itakavyonufaika na ziara hizo.



“Ipo haja ya kujipanga vizuri na kuangalia namna ya kutumia mahusiano haya kupiga hatua, tusifurahi tu kwa kuwa wanakuja ipo haja ya kujipanga vizuri kuhakikisha tunaweza kupata fursa ili kuwepo na faida kwa pande zote,” alisema.

Lakini kinachoshawishi ziara hizo, alisema ni masilahi yanayotokana na ukweli kwamba, Afrika ina rasilimali nyingi.

“Baada ya ukoloni wakaja na njia mpya ya kuhakikisha wanaendelea kuvuna rasilimali zilizopo. Wenzetu wanajua namna ya kujiweka vizuri kwa kukamata rasilimali na soko,” alisema.

Ujio wao, alisema unalenga kuimarisha diplomasia, lakini ndani yake kuna fursa lukuki wanazozitarajia.

“Wanataka kuimarisha uchumi wa nchi zao na wanapambana kwa kuwa wanajua ni ushindani na uwepo wa mchina aliyeikamata Afrika kwa nguvu umewatisha,” alisema.

Naye Mhadhiri kutoka Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Godwin Amani alisema siasa za ulimwengu zimebadilika.

Alisema hilo linafanya Afrika iliyoonekana haina uwezo wa kuamua kuhusu mambo yake, sasa inaonekana muhimu na tegemeo la wengi.

Lakini, alisema bado Afrika haijaathiriwa na mambo mengine kwani ina ardhi nzuri ya kilimo, hivyo inahitajika na wengi.

Kutokana na hayo, alieleza ujio wa viongozi hao ni kutaka ushirikiano na Afrika wakitambua umuhimu wake.

Hata hivyo, alisema si vibaya kuridhia ushirikiano huo, isipokuwa ni vema kuwa waangalifu.

"Na hilo hatuna shaka nalo kwa kuwa tumeshajifunza tangu zamani, sasa hivi hatutahitaji tena kujifunza tuwe makini ili ushirikiano usituathiri, lakini tusikatae kushirikiana," alisema.