Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais wa Ujerumani awasili Tanzania

Rais wa Ujerumani Frenk-Walter Steinmeier akipokea ua baada ya kuwasili Tanzania.

Muktasari:

  • Rais Frenk-Walter Steinmeier atafanya ziara ya siku tatu nchini kusafiri kwenda Songea kuangalia kumbukumbu ya vita vya Majimaji na kutembelea Shule ya Msingi Majimaji.

Dar es Salaam. Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, amewasili nchini tayari kwa kuanza ziara yake inayotarajiwa kufanyika kwa siku tatu.

Steinmeier amewasili nchini usiku wa leo Jumatatu Oktoba 30, 2023 na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Serikali, Rais Steinmeier anatarajia kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan kesho kabla ya kuendelea na shughuli nyingine.

Kwa mujibu wa kituo Cha televisheni cha UTV, kupitia ziara hiyo, wafanyabiashara wa Ujerumani na Tanzania wanatarajia kukutana kupitia kongamano maalumu ili kujadiliana kuhusu fursa za kibiashara zilizopo hapa nchini baina ya nchi hizo mbili.

Akizungumzia ziara hiyo Mkuu wa mawasiliano Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Mindi Kasiga amesema Rais huyo ameambatana na wafanyabiashara 12 waliojikita katika sekta mbalimbali ambazo mataifa hayo yanahusiana.

"Atapokelewa rasmi na Rais Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Dar es Salaam na baadaye atashiriki kongamano la wafanyabiashara kwa ajili ya kukuza na kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na Ujerumani," amesema Kasiga.

Amesema kongamano hilo linatarajiwa kuibua fursa mbalimbali na maeneo mapya ya ushirikiano.

Aidha ameongeza kuwa Rais huyo atatembelea kiwanda cha simenti cha Twiga ambacho kina ubia na kampuni ya Ujerumani.

"Siku ya tatu ya ziara atasafiri kwenda Songea kuangalia kumbukumbu ya vita vya Majimaji na kutembelea Shule ya Msingi Majimaji," amesema.

Pia amesema ziara hiyo ni ishara ya diplomasia ya uchumi kukua kwani huo ni muendelezo wa viongozi mbalimbali kuja hapa nchini kwa ajili ya kuimarisha mahusiano.