Rais wa Ujerumani kufanya ziara Tanzania

Muktasari:
- Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier atafanya ziara nchini Tanzania na kutembelea makumbusho ya vita vya majimaji.
Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini kuanzia kesho Oktoba 30 hadi Novemba 1, 2023.
Hayo yameelezwa leo Jumapili Oktoba 29, 2023 kupitia taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Kulingana na taarifa hiyo, ziara hiyo mbali na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano wa maendeleo baina ya Tanzania na Ujerumani, pia imelenga kukuza na kuimarisha misingi ya biashara na uwekezaji.
Imeeleza ujumbe wa Rais huyo utakaojumuisha viongozi wa Serikali ya nchi hiyo na wawekezaji wa kampuni 12, utawasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam kesho.
“Ugeni huo utapokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba,” imesema taarifa hiyo
Baada ya kuwasilia, taarifa hiyo inaeleza, Rais Steinmeier atafanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan Oktoba 31, mwaka huu.
“Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao watapata fursa ya kuongea na Waandishi wa habari kuelezea kuhusu masuala muhimu yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo yao,” amesema.
Imeeleza wawili hao watashiriki Jukwaa la Biashara, litakalohusisha wafanyabiashara na wawekezaji wa nchi hizo mbili, lililoandaliwa na Ubalozi wa Ujerumani kwa ushirikiano na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Mazungumzo na vijana wa Tanzania, kutembelea kiwanda cha Twiga Cement na makumbusho ya vita vya majimaji mkoani Songea ni miongoni mwa shughuli zinazotrajiwa kufanywa na ugeni huo.
Uhusiano wa nchi hizo
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na TIC, Tanzania imekuwa ikiuzia Ujerumani bidhaa zenye thamani ya wastani wa Dola za Marekani milioni 42.04 kwa mwaka.
Bidhaa kuu ambazo Tanzania inaiuzia Ujerumani ni Kahawa, Tumbaku, Pamba, Asali, Samaki, Nta na vito vya thamani.
Kadhalika, Tanzania inaagiza bidhaa kutoka Ujerumani zenye wastani wa Dola za Kimarekani milioni 237.43 kwa mwaka na bidhaa kuu ni Dawa, Vifaa Tiba, Mafuta (manukato, vipodozi) Magari, Vifaa na Mashine za Umeme.
Kwa upande wa uwekezaji, Ujerumani ni miongoni mwa nchi kumi zinazoongoza kwa uwekezaji nchini.
Kwa mujibu wa TIC hadi Agosti mwaka huu, miradi 178 ya Ujerumani yenye thamani ya Dola za Marekani 408.11 milioni ilisajiliwa na kutoa fursa za ajira 16,121.
Kwa upande wa Zanzibar, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) imesajili miradi 15 yenye thamani ya Dola za Marekani 300 milioni iliyozalisha ajira 905.