Ajali ya basi yaua sita Tabora, 11 wajeruhiwa
Muktasari:
- Polisi Mkoa wa Tabora linaendelea kumtafuta dereva wa basi la Kampuni ya Last Bullet aliyesababisha vifo vya watu sita na majeruhi katika ajali iliyotokea mkoani humo mapema leo Jumanne.
Tabora. Watu sita akiwemo mtoto mdogo wamefariki dunia na wengine zaidi ya 11 kujeruhiwa katika ajali ya basi la Kampuni ya Last Bullet iliyotokea leo Jumanne, Julai 7, 2026 eneo la Chemchem wakati linatoka kituo cha mabasi Tabora kuelekea mkoani Geita.
Kati ya vifo hivyo sita, watano wamefariki papo hapo na mmoja ambaye ni mtoto amefariki dunia akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Twaha Lulengelule akizungumza na waandishi wa habari amesema chanzo cha ajali hiyo bado hakijafahamika na mpaka sasa dereva amekimbia na wanaendelea kumsaka.
"Tunaendelea kumsaka dereva huyu aje kujibu tuhuma zinazomkabili za kusababisha vifo hivyo na majeruhi kama hivi, kwani inaonekana pia hakuwa kwenye mwendo mdogo," amesema.
Amesema gari hiyo kabla ya kutoka kituo cha mabasi imekaguliwa na askari wao na ikaonekana iko salama na inafaa kusafiri, maana yake ajali imetokea kwa sababu nyingine na sio masuala ya kiufundi.
"Kumekuwa na tabia wakati mwingine madereva kukimbia na magari maeneo ya mjini, sasa wakati tunapambana na hawa, huyu anakuja kuvunja sheria na hatuwezi kuvumilia hili liendelee," amesema.
Basi la kampuni ya Last Bullet liliopata ajali leo Tabora mjini.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Loshipay Laizer amesema shughuli ya uokoaji imekwenda vizuri kwa haraka na majeruhi wote wameshafikishwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi.
"Tumefanikiwa kuokoa kwa haraka baada ya ajali kutokea na tayari wako hospitali wanaendelea na matibabu," amesema.
Juma Jesse shuhuda wa ajali hiyo amesema gari hilo likiwa limetoka kituo kikubwa cha mabasi ilikuwa mwendokasi huku dereva akipiga honi nyingi mfululizo akieleza imekuwa tabia ya madereva wa mabasi ya masafa marefu kutoka na mwendo kasi kituoni.
"Tushayazoea mabasi makubwa yakitoka kituo cha mabasi yanakuwa mwendokasi sana na kupiga honi nyingi sana ishara ya kwamba linatoka sasa," amesema.
Maua Salum, shuhuda amesema basi hilo baada ya kuruhusiwa kwenye mataa liliondoka kwa kasi na lilipofika kwenye kona likabinuka na ndio zikaonekana damu zinamwagika kutoka ndani ya basi.
"Yaani damu zimemwagika sana pale chini na kwenye ubavu wa gari na juu kule basi limefumuka kabisa lipo wazi, watu wametolewa wameumia sana kwa kweli," amesema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella ametoa pole kufuatia ajali hiyo huku akiwahimiza madereva kuongeza umakini wawapo kwenye majukumu yao ili kuepusha kugharimu maisha ya watumiaji wa usafiri.
"Hatupendi kuona watu wanapoteza maisha wala wanapata majeraha kwa sababu hiyo inagharimu uchumi na kuathiri wategemezi hivyo umakini unapaswa kuongezeka," amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoani humo, Peter Magayane amesema operesheni na ukaguzi itaendelea ikiwa ni sambamba na kuchukua hatua kwa madereva wanaoshindwa kufanya kazi yao kwa weledi.
"Tutawashughulikia madereva wote wanaovunja sheria kwa sababu pia uzembe wao unagharimu maisha ya watu wasio na hatia," amesema.