Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hizi hapa sababu Mtanzania kushindwa kumiliki nyumba

Muktasari:

  • Changamoto zinazomfanya Mtanzania kushindwa kuwa na nyumba au amiliki kwa gharama kubwa zamulikwa.

Dar es Salaam. Kukosekana kwa sera ya nyumba, mikakati na gharama kubwa za ujenzi ni miongoni mwa sababu zinazowafanya Watanzania wengi wakiwemo vijana kushindwa kumiliki nyumba bora na salama.

Hayo yamebainishwa kwenye utafiti wa ‘Ukuaji wa Nyumba katika miji ya Afrika jinsi ya kujenga makazi kunavyoendesha ukuaji wa miji na uchumi’ uliofanywa nchini Tanzania na Ghana na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF).

Akizungumza na Mwananchi katika warsha iliyowakutanisha watafiti na wadau na Serikali Aprili 24, 2025 Mkurugenzi wa ESRF, Profesa Fortunata Makene amesema dhumuni la utafiiti ni kuwafanya hasa vijana wamiliki nyumba bora hivyo changamoto zote zilizoibuliwa zinawasilishwa serikalini.

“Nikweli hakuna sera ya nyumba na bila sera maana yake masuala mazima yanayohusiana na nyumba, ujenzi, ubora na gharama inakuwa ngumu,” amesema.

Amesema utafiti huo wa miaka mitatu ulioanza mwaka 2021 uliofanyika Dar es Salaam na Morogoro umebaini nyumba bora inahitaji gharama kubwa kiasi cha Mtanzania wa hali ya kawaida hawezi kununua kuimiliki.

“Sasa hivi mambo yamebadilika kuna maendeleo katika ujenzi kuna matumizi ya aluminiamu, jipsum, vigae, vioo ambapo vitu hivi vinafanya gharama kuwa kubwa mno. Vijana hawana nyumba nzuri za kisasa,” amesema Profesa Makene.

Aidha amesema changamoto nyingine hata ujenzi holela, gharama za maeneo ya ujenzi vilevile inachangia. Katika kutatua changamoto hizo, Profesa Makene amesema kupitia utafiti huo zitatengenezwa ripoti kisha kupelekwa taasisi mbalimbali za Serikali.

“Ndiyo maana tunashiriki na washiriki kutoka wizarani, halmashauri katika warsha kama hizi ili wasikie kwanza changamoto kisha kuzitatua ili Watanzania wenye mpango wa kumiliki nyumba za ndoto zao wazifikie,” amesema.

Kingine amesema takwimu katika utafiti huo zinaonesha umiliki wa nyumba kwa wanawake uko chini ukilinganisha na wanaume akisema katika watu kumi wanawake ni wawili wanaomiliki.

Profesa Lusugga Kironde mmoja ya washiriki wa utafiti huo amesema vilevile utafiti umeangazia namna ya ujenzi wa nyumba ambapo umebaini watu wanajenga kiholela bila ya kuwa na mwongozo.

“Tunataka kuwe na sera ya nyumba ili Serikali iwepo kuwasaidia changamoto zao katika mchakato mzima. Kitaifa tunataka kila Mtanzania afikie kigezo fulani mfano ilivyo katika elimu.

“Tumegundua pia watu waliowengi wanaishi katika nyumba ambazo hazijakamilika unakuta mtu kapaua tu anahamia sasa hatuwezi kuishia hapohapo lazima kuwe na mwongozo,” amesema.

Amesema sera ieleze nyumba anayotaka kuishi au kupangisha mtu iwe na ubora gani, iseme mtu afikie hatua fulani, yote katika kuboresha eneo hili muhimu la ustawi wa watu.

Profesa wa Idara ya Jiografia ya Binadamu na Mazingira, Claire Mercer amesema kwa ujumla wamefanya utafiti huo Ghana na Tanzania kujua umuhimu wa nyumba unavyojenga ukuaji wa uchumi wa miji na watu.

Katika hilo ndipo wamegundua watu wengi wanashindwa kujenga nyumba kutokana na sababu tajwa hivyo kuminya uchumi wa nyumba ambao ni sehemu ya kupata kipato kuanzia ujenzi hadi matumizi ikiwemo upangishaji.

Ofisa Mipango Miji kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Makao Makuu, Paul Kitosi amesema kwanza nyumba ni moja ya mahitaji muhimu ya mwanadamu, hivyo mtu anapokuwa hana nyumba anapata changamoto zinazoathiri hata kipato.

Kunapokuwa na nyumba za gharama za chini wananchi wanarahisishiwa hata shughuli zao za kiuchumi.

“Sisi kama Serikali tumechukuwa yote haya na ambayo yamejadiliwa tumepokea tunafanyia kazi,” ameahidi.