Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hii hapa ajira inayoongoza kwa kutafutwa ‘Google’

Muktasari:

  • Ajira, teknolojia ya akili unde (AI), mikopo na huduma za kifedha, Kamari pamoja na elimu ni miongoni mwa maeneo matano yaliyotafutwa zaidi mtandaoni na Watanzania katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka 2026.



Dar es Salaam. Ajira, teknolojia ya akili unde (AI), mikopo na huduma za kifedha, Kamari pamoja na elimu ni miongoni mwa maeneo matano yaliyotafutwa zaidi mtandaoni na Watanzania katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka 2026.

Mwelekeo huo unaashiria mabadiliko katika vipaumbele vya Watanzania, katika kipindi ambacho gharama za maisha zimeendelea kuongezeka, ushindani katika soko la ajira umeongezeka, na matumizi ya teknolojia za kidijitali yamekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku.

Wakati maelfu ya vijana wakitafuta nafasi za ajira kupitia Google kila siku, wengine wameelekeza umakini wao kwenye zana za akili bandia (AI) kama ChatGPT na Gemini, wakitafuta njia mpya za kujifunza, kuongeza ufanisi kazini au kujiongezea kipato.


Nini maana yake

Akizungumzia suala hili leo Alhamisi Julai 16, 2026, Mtaalamu wa Uchumi,  Dk Goodhope Mkaro amesema kama wengi wakiingia wanatafuta ajira kuna changamoto ya ajira, wengine wanataka wabadili ajira.

Amesema teknolojia ndiyo njia ya mawasiliano na njia ya kazi; inaweza kuwa kitu kizuri kuonesha mafanikio ya kuhamishia kazi nyingi kufanyika kidijitali

“Ndiyo dunia inapokwenda na kama nchi tunakwenda na kasi hiyo, namna ya kufanya kazi imekuwa kidijitali, hii imefanya wengine kuamua kujifunza AI kwa sababu zipo hadi za kusoma bure na watu wengi, karibu kila kitu wanataka kusaidiwa na AI ndiyo maana hata matumizi yake yanaonekana kuwa yako juu,” amesema.

Mtaalamu wa masuala ya kidijitali, Baraka Mafole amesema hali ngumu ya maisha imebadili namna Watanzania wanavyotumia mtandao badala ya kutumia zaidi kwa burudani kama ilivyokuwa miaka michache iliyopita sasa wengi sasa wanatafuta fursa za ajira za mtandaoni.

Hilo limeenda sambamba na kutafuta maarifa yanayoweza kuwasaidia kujiongezea kipato huku miongoni mwa maswali yanayotafutwa kwa wingi ni kuhusu kazi zinazoweza kufanywa kwa njia ya mtandao na jinsi AI inavyoweza kuwasaidia kupata ajira au kuongeza kipato.

“Pamoja na mabadiliko hayo, Tanzania bado haijafikia kiwango kinachotarajiwa katika matumizi ya teknolojia za kidijitali kutokana na idadi kubwa ya wananchi kukosa ujuzi unaohitajika,” amesema.

Amesema juhudi zinaendelea lakini bado zinahitaji kuongezewa nguvu kwa kushirikiana Serikali na wadau wengine ili kuwajengea wananchi ujuzi wa kidijitali utakaowawezesha kunufaika na fursa zinazotokana na teknolojia.


Maeneo mengine

Ongezeko la utafutaji kuhusu mikopo linatajwa katika pande mbili; ya kwanza ni kulinganisha viwango vya riba kati ya taasisi na taarifa sahihi huku wengine wakitafuta namna ya kujikwamua kiuchumi huku.

Upande wa kamari imeendelea kutawala miongoni mwa mada zinazotafutwa zaidi jambo linaloonesha jinsi michezo ilivyoendelea kuwa kivutio kwa Watanzania lakini pia kuibua maswali kuhusu utegemezi wa kamari kama chanzo cha matumaini ya kipato.

Elimu nayo haijaachwa nyuma. Vipindi vya matokeo ya mitihani, udahili wa vyuo na fursa za masomo vimeendelea kuongeza utafutaji wa taarifa mtandaoni, zikionesha kwamba; pamoja na changamoto za kiuchumi, Watanzania bado wanaiona elimu kuwa njia muhimu ya kuboresha maisha yao.

Katika upande wa mikopo, Mtaalamu wa Elimu ya Fedha, Magesse Mazingeamesema ni ishara kuwa Watanzania wengi wanatafuta njia za kukabiliana na changamoto za kifedha zinazotokana na kupanda kwa gharama za maisha na mahitaji ya mitaji kwa ajili ya biashara.

Amesema tofauti na miaka ya nyuma, watu wengi walikopa kwa ajili ya matumizi makubwa au ununuzi wa mali; sasa sehemu kubwa ya wananchi wanatafuta mikopo ya kuanzisha au kuendeleza biashara ndogo, kulipia ada za shule, kugharamia matibabu au kuziba pengo la matumizi ya kila siku.

"Kuongezeka kwa utafutaji wa taarifa za mikopo si lazima kuwe na maana kwamba, watu wote wanakopa bali kunaonesha mahitaji makubwa ya kupata suluhisho la kifedha. Lakini muhimu wananchi wakakopa kwa malengo yenye tija na kuhakikisha wana uwezo wa kurejesha mikopo hiyo ili kuepuka kuingia kwenye mzunguko wa madeni," amesema.

Mtaalamu wa Huduma za Kifedha, Letisia Masuana amesema wakati mwingine ongezeko la utafutaji wa mikopo linaonesha wananchi wamekuwa wakitumia mtandao kulinganisha bidhaa za kifedha kabla ya kufanya uamuzi.

“Elimu ya fedha imeongezeka na watu wengi wanataka kujua viwango vya riba, masharti ya mikopo na taasisi zinazotoa huduma nafuu kabla ya kuomba mkopo, ikiwa hivi ni jambo zuri na kinyume chake kama ni mikopo ya simu, runinga na vitu vingine vidogo inabidi iangaliwe,” amesema.


Watoa onyo

Hata hivyo, uwepo wa michezo ya kubahatisha kama miongoni mwa vitu vilivyotafutwa sana vinatajwa kuwa na matokeo hasi katika kuathiri namna vijana wanavyofikiri.

Dk Goodhope amesema hiyo ni ishara kuwa vijana sasa hawapendi kufanya kazi na wanabaki wakiiamini kamari kama njia ya mkato ili waweze kupata fedha.

“Ni mbaya mtu akiamini kuwa, naweza kupata Sh100 milioni kwa ajili ya kucheza kamari inafanya ashindwe kutumia fedha aliyonayo; kuwekeza katika mambo mengine na kuendelea kuizungusha kwenye michezo ya kubahatisha hii inamfanya anapata uraibu,” amesema.

Mtaalamu wa Saikolojia, Naiman Mussa amesema kupunguza tatizo la kamari kunahitaji mchanganyiko wa elimu ya fedha, ajira na ushauri wa afya ya akili badala ya kutegemea sheria pekee.

Amesema watu wengi wanaoingia kwenye kamari hufanya hivyo, wakiamini ni njia ya haraka ya kubadilisha maisha, hasa wanapokabiliwa na ukosefu wa ajira au kipato kidogo.

“Ni muhimu Serikali, taasisi za elimu na wadau wengine kuwekeza katika utoaji wa elimu ya fedha na ujuzi wa kujiongezea kipato ili kuwapa vijana mbadala wa kutafuta fedha kupitia kamari,” amesema.

“Pia, ni lazima kuimarisha huduma za ushauri nasaha kwa watu wanaopata uraibu wa kamari kwa kuwa wengi wao huhitaji msaada wa kitaalamu ili kuondokana na tabia hiyo.”