Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

GPS ilivyomfichua muuaji wa bodaboda, auhukumiwa kifo

Muktasari:

  • Baada ya kumuua bodaboda huyo wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, mtuhumiwa alikimbilia Manyoni, mkoani Singida, ambako aliuza pikipiki kwa Sh1.4 milioni, lakini akakamatwa kufuatia pikipiki hiyo kuwa na mfumo wa ufuatiliaji wa GPS (Global Positioning System).

Arusha. Licha ya Aivan Jackson, kuiba pikipiki wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani na kuisafirisha hadi mkoani Singida alikoiuza, hakuepuka mkono wa sheria baada ya kutiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kumuua dereva bodaboda, Frank Antony, na kisha kuiba pikipiki yake.

Mauaji hayo yalitokea Mei 5, 2023, katika Kijiji cha Kalabaka, eneo la Fukatosi Bayagomo, mkoani Pwani, ambapo Aivan alimuua Frank kwa kumkata na panga kichwani, kisha akaiba pikipiki yake na kuisafirisha hadi Manyoni, alikoenda kuiuza.

Kutokana na pikipiki hiyo kuwa na mfumo wa ufuatiliaji wa GPS (Global Positioning System), polisi walimfuatilia na kumkamata mtuhumiwa baada ya mtu aliyenunua pikipiki hiyo kukamatwa.

Aivan alishtakiwa kwa kosa la mauaji katika kesi iliyosikilizwa na Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, mbele ya Jaji Butamo Philip.

Hukumu ya kesi hiyo ilitolewa Mei 2, 2025, ambapo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama iliridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa hilo bila kuacha shaka yoyote.


Ilivyokuwa

Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi 10, akiwemo Inspekta Ulinyambusya (PW1), G 6012 Koplo Isaya (PW2), Juma Mtolo (PW3), G 7671 PC Okombo (PW4), na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Mwanzo Manyoni, Masatu Magesa (PW5).

Mashahidi wengine ni D 8831 Sajenti (PW6), Rashid Galawa (PW7), Hamisi Rashidi (PW8), G 1918 Koplo Emmanuel (PW9), na Dk Edna Deogratias Buberwa (PW10).

Mbali na mashahidi hao, upande wa mashtaka pia uliwasilisha vielelezo vinne, ikiwemo pikipiki yenye namba za usajili MC 272 DRE iliyotumika kama kielelezo muhimu katika kesi hiyo.

PW1 aliieleza Mahakama kuwa akiwa katika kituo chake cha kazi alipokea taarifa kuhusu pikipiki iliyoibiwa kutoka Bagamoyo hadi Manyoni, katika tukio ambalo mtu mmoja aliuawa.

Alifafanua kuwa alielekezwa kuhusu mfumo wa GPS uliowekwa kwenye pikipiki hiyo, uliomsaidia kuifuatilia hadi Kijiji cha Makuru, ambako aliwakamata watu wawili waliokuwa nayo, Shango Shani na Rashid Juma.

Baada ya kuwahoji, walieleza kuwa waliipata pikipiki hiyo kutoka kwa PW7, ambaye naye alikamatwa katika Kijiji cha Mbwekoo.

Alipofanyiwa mahojiano, PW7 alikiri kuwa alinunua pikipiki hiyo kutoka kwa mshtakiwa.

PW3 aliieleza mahakama kuwa marehemu alikuwa mpwa wake, na kwamba Mei 6, 2023, kaka yake alimjulisha kuhusu kifo cha Frank na kupotea kwa pikipiki aliyokuwa akiitumia.

Walipofika eneo la tukio, walikuta mwili wa marehemu ukiwa na jeraha kichwani na usoni.

Ushahidi huo ulithibitishwa na PW9, aliyekuwa mpelelezi wa kesi hiyo. Alieleza mahakama kuwa alifika eneo la tukio akiwa na askari wenzake, na walikuta marehemu akiwa na majeraha usoni, kichwani na mgongoni.

Alieleza pia kuwa alipohoji ndugu wa marehemu, aligundua kuwa marehemu alikuwa dereva wa bodaboda yenye namba za usajili MC 272 DRE, iliyokuwa imeibiwa wakati huo.

Shahidi alieleza mahakama kuwa katika uchunguzi wake, aligundua kuwa pikipiki hiyo ilikuwa imewekwa na mfumo wa GPS, ambapo aliunganishwa na mtu aliyeweka mfumo huo.

Kupitia GPS, waligundua kuwa pikipiki hiyo ilielekea Singida.

Shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa walizungumza na wenzao waliopo Singida, ambao walisaidia katika kufuatilia pikipiki hiyo.

Mei 17, 2023, kupitia mfumo wa GPS, alithibitisha kuwa pikipiki hiyo ilifika Singida, na walifanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa.

Aidha, shahidi alieleza kuwa Mei 20, 2023, alikwenda Manyoni, mkoani Singida, akiwa na wenzake wawili, na walikutana na mshtakiwa pamoja na watuhumiwa wengine.

Alipomhoji Aivan, alikiri kumuua marehemu na kuiba pikipiki hiyo.

PW5 alieleza mahakamani kuwa Mei 22, 2023, alimpokea mshtakiwa katika ofisi yake, baada ya kuletwa na PW4 kwa ajili ya kurekodi ungamo lake.

Alipompa mshtakiwa haki zake za kisheria, ikiwa ni pamoja na kumuita wakili au ndugu yake wakati anahojiwa, Aivan alikataa na kusema hataki mtu yeyote ashuhudie mahojiano hayo.

Shahidi huyo alieleza kuwa Aivan alikiri kumuua marehemu na kuiba pikipiki aliyokuwa akiitumia.

PW6 alieleza kuwa Mei 18, 2023, alirekodi maelezo ya onyo ya mshtakiwa, na kuwa kabla ya kurekodi alimpa haki zake za kisheria, ikiwemo kumuita wakili au ndugu yake, lakini mshtakiwa alikataa na akaendelea kuhojiwa akiwa peke yake, ambapo pia alikiri kutenda kosa hilo.

PW7, mfanyabiashara, alieleza kuwa Mei 17, 2023, alizungumza na PW8 akitaka kwenda soko la Makuru kununua mbuzi, na kwa kuwa alikuwa na Shango, alikodishiwa pikipiki hiyo kwa Sh10,000, ambapo alinunua mbuzi saba.

Walipomaliza, walielekea kwenye mgahawa, ambapo walikamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Makuru.

Walipoulizwa kuhusu mmiliki wa pikipiki hiyo, walimtaja PW8, ambaye aliwaambia kuwa pikipiki hiyo aliuziwa na Aivan.

PW8 alieleza kuwa alinunua pikipiki hiyo kwa mshtakiwa kwa Sh1.4 milioni, ambapo alilipa Sh600,000, na walikubaliana kuwa baada ya kumaliza malipo yote, angempa kadi ya usajili wa pikipiki.

Alisema kuwa Mei 17, 2023, alimkodishia PW7 pikipiki hiyo, na kabla ya kuirejesha, alimpigia simu kumjulisha kuwa pikipiki hiyo imeharibika.

Walikubaliana kukutana eneo la Msemembo, lakini alikamatwa na polisi na alipoulizwa aliponunua pikipiki, alimtaja mshtakiwa.

PW10, daktari aliyemfanyia uchunguzi marehemu, alieleza kuwa baada ya uchunguzi, alibaini kuwa marehemu alikuwa na majeraha usoni na nyuma ya kichwa chake, na chanzo cha kifo kilikuwa kuvuja damu.


Utetezi wa mshtakiwa

Katika utetezi wake, Aivan alieleza mahakamani kuwa alikuwa akiishi Manyoni kabla ya kukamatwa na alikuwa akijishughulisha na kuuza kuku sokoni.

Alisema kuwa saa 12 alfajiri, mmoja wa wateja wake alimtaka amuuzie kuku 30 kwa Sh300,000.

Alieleza kuwa alipokuwa njiani kurejea nyumbani, alikuta kwenye mgahawa, na alipomlipa Sh10,000 mhudumu, alielezwa kuwa fedha hizo ni bandia.

Alisema kuwa alimuonyesha fedha zote alizokuwa nazo, na baada ya kuziangalia, mhudumu alikiri kuwa fedha ni bandia, na kutokana na kelele zilizozuka, walikusanyika watu wengi na polisi walifika.

Alisema kuwa mmiliki wa mgahawa alieleza polisi kuwa Aivan alikuwa amempa fedha bandia, na walipochukua fedha hizo, alieleza walikozitoa.

Hata hivyo, polisi walimuuliza alikozitoa fedha hizo na walikataa kumwamini, hivyo wakamkamata hadi kituo cha polisi.

Aivan alisema aliteswa na polisi, na alihojiwa kuhusu mashine inayotengeneza fedha bandia.

Aliendelea kusema kuwa alikataa kutoa rushwa kwa polisi, na alikaa kituoni hapo kwa siku nne kabla ya kupelekwa Kituo cha Polisi Bagamoyo akiwa na watu wanne wasiowafahamu.

Aivan alieleza zaidi kuwa alikaa kituoni hapo kwa siku sita, lakini hakuwa na ufahamu wa sababu ya kukamatwa kwake.

Alisema alifikishwa mahakamani kwa kesi ya mauaji lakini hakujua jina la marehemu, hakuwa na maelezo yoyote ya kukiri, na hakuwa na taarifa yoyote kuhusu kifo cha marehemu.


Uamuzi wa Jaji

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Jaji alisema kuwa kutokana na ushahidi uliotolewa, hakuna shahidi aliyeshuhudia mauaji ya marehemu, na hakuna shahidi aliyethibitisha kumuona mshtakiwa akimshambulia au kumuua marehemu.

Alisema kuwa kesi ya upande wa mashtaka ilitegemea maelezo ya onyo ya mshtakiwa, ungamo la mshtakiwa, na ushahidi wa kimazingira.

Baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, Jaji alihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.