Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dereva bodaboda auawa Arusha akituhumiwa kuiba pikipiki

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Salvas Makweli

Muktasari:

  • Pikipiki hiyo iliibwa jana Aprili 10, 2025 saa mbili usiku katika eneo la mjini wakati mmiliki wake akitizama mpira kati ya Azam na Yanga, kabla ya kudaiwa kukutwa na kijana huyo leo asubuhi Aprili 11, 2025 kwa fundi akibadilisha baadhi ya vifaa.

Arusha. Kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Salim, dereva bodaboda na mkazi wa Sinoni, ameuawa kwa kuchomwa moto na wananchi wenye hasira, baada ya kudaiwa kukutwa na pikipiki ya wizi.

Tukio hilo limetokea leo Aprili 11, 2025, majira ya saa nne asubuhi katika eneo la Olmokea, ambapo marehemu alikutwa kwa fundi akibadilisha baadhi ya vifaa vya pikipiki hiyo, ambayo inabia jana usiku katika eneo la Mjini Kati.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Salvas Makweli amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa bado linafanyiwa uchunguzi.

“Ngoja na mimi nifuatilie nijue undani wa tukio hilo ndipo nitaweza kuongelea zaidi,” amesema kwa njia ya simu.

Kwa mujibu wa mashuhuda, pikipiki hiyo iliibwa wakati mmiliki wake akiwa ameiacha nje ya banda moja, akitazama mechi kati ya Azam na Yanga.

Mhina Sefu, mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, amesema:

“Inadaiwa huyu kijana aliyeuawa naye ni dereva bodaboda. Alienda eneo la tukio na kuchukua bodaboda hiyo kana kwamba ni yake, hivyo watu hawakumtilia shaka. Baada ya mechi kuisha ndipo mmiliki wa pikipiki aligundua imeibwa na kuanza kulalamika.”

Sefu amesema kazi ya msako haikuwa ngumu kwani pikipiki hiyo ilikuwa imefungwa mfumo wa GPS, uliosaidia kufuatilia hadi ilipoonekana leo asubuhi.

“Walipomkuta kijana huyo kwa fundi, wakashuhudia akiwa anafungua baadhi ya vifaa vya pikipiki, ikiwemo taa. Fundi amesema pikipiki ni ya huyo kijana. Hapo ndipo watu walipoanza kumpiga na baadaye kumchoma moto,” alieleza.

Diana Awile, mkazi wa eneo hilo, ameeleza kusikitishwa na ongezeko la matukio ya wizi jijini Arusha na kutoa wito kwa vijana kufanya kazi halali.

“Vijana fanyeni kazi, msiibe. Angalieni mwenzenu leo hata chai hajanywa tayari amepoteza maisha. Wakati alikuwa na kazi nzuri ya kuendesha bodaboda, angeweza kupata riziki ya halali,” amesema.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Olmokea, Abdallah Mgongo, amesema alipokea taarifa za tukio hilo kwa njia ya simu kutoka kwa mwananchi ndipo alipoamua kuwasiliana na Polisi.

“Nilipopata simu, nilitoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao waliahidi kufika. Kwa bahati mbaya walichelewa kidogo, walipofika tayari kijana alikuwa amepigwa na kuchomwa moto,” alisema Mgongo.

Tukio hilo limeibua taharuki kubwa miongoni mwa wakazi wa Arusha, huku wengi wakitaka kuimarishwa kwa ulinzi na kuhimiza vijana kuepuka vitendo vya kihalifu vinavyohatarisha maisha yao.