GMSA yapendekeza kuondolewa tozo za simu kuchochea huduma za fedha mtandao

Mkurugenzi wa Sera za Umma wa Shirikisho la Kampuni za Simu GSMA, Caroline Mbugua
Muktasari:
Wakati huduma za kufedha kupitia simu za mkononi zikiwa bado hazijarejea ikilinganishwa na kabla ya kuanzishwa kwa tozo GSMA imekuja na mapendekezo ya kuboresha sekta hiyo.
Dar es Salaam. Wakati thamani ya miamala ya simu inayofanywa kupitia simu za mkononi ikiwa bado haijarejea kama ilivyokuwa kabla ya kodi, Shirikisho la Kampuni za Simu (GMSA) limekuja na mapendekezo ya kuongeza kiwango hicho.
Miongoni mwa vitu vilivyopendekezwa ni kuondolewa kwa tozo za kielektroniki zilizowekwa, uwepo wa sera wezeshi kwa ajili ya sekta ya mawasiliano na kupunguza ushuru wa sekta.
Hayo yamesemwa katika Mwananchi Jukwaa la Fikra lililofanyika leo Juni 20, 2023 jijini Dar es Salaam, huku likibebwa na mada isemayo Uwekezaji jatika mabadiliko ya kidigitali kwa ajili ya ustawi na ushirikishwaji wa jamii Dira 2025.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa Sera za Umma wa Shirikisho la Kampuni za Simu GSMA, Caroline Mbugua amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na GMSA inapendekeza kuondolewa kwa tozo za simu ili kuruhusu huduma za kifedha kufanyika zaidi kwa njia ya simu.
"Hii itasaidia kurejesha sekta hiyo, kukuza ujumuishaji wa kifedha na ukuaji wa uchumi nchini," amesema.
Pia lazima kuwapo kwa sera zinazotabirika ili kufanya mazingira ya kodi kuwa mazuri na yanayofaa kwa ajili ya uwekezaji katika sekta ya mawasiliano.
Pia amesema ni lazima sera ziwe na afya ya muda mrefu katika sekta ya mawasiliano na dijitali nchini ili maendeleo yake yaweze kuchangia ukuaji wa uchumi.
"Kuweka usawa wa kikodi kwenye sekta ya simu, kupunguza ushuru wa sekta mahususi na kupunguza vikwazo vinavyotokana na kodi ili kuongeza uwezo wa kumudu huduma za simu, kupanua wigo wa kodi ili kuboresha ufanisi, kupata mapato zaidi ," amesema
Serikali kupitia Bunge la Bajeti la mwaka 2021/2022 ilianzisha tozo itakayotozwa katika kila muamala wa kutuma au kupokea fedha na kiwango kati ya Sh10 hadi Sh200 kwa siku kila mteja anapoongeza salio la muda wa maongezi kwenye simu.
Tozo hizo zilianza kutumika Julai 15, 2021 ni tofauti na zile zinazotozwa na kampuni za simu pindi mteja anapotaka kutuma au kupokea fedha kutoka kwa mtu mwingine.
Lakini baadaye Septemba 2022, Serikali ilitangaza kufuta na kupunguza kiwango cha tozo za miamala ya kieletroniki.
Uamuzi huo ulitangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba ulitajwa kuwa umelenga kupunguza wigo wa tozo, kuchochea matumizi ya miamala kwa ajili ya kupunguza fedha taslimu, kurahisisha utozaji na kuzuia kutoza tozo husika mara mbili.