Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ghorofa laporomoka Dar, watu kadhaa wahofiwa kupoteza maisha

Muktasari:

  • Jengo hilo linaelezwa kuporomoka mapema leo Jumamosi Novemba 16, 2024. Taarifa za awali kutoka kwa mashuhuda, zinaeleza ndani ya jengo hilo la kibiashara, kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa wakifanya ununuzi katika maduka ya jengo hilo.

Dar es Salaam. Watu kadhaa wanahofiwa kupoteza maisha baada ya jengo la ghorofa lililopo Kariakoo Mtaa wa Congo na Mchikichi jijini Dar es Salaam kuporomoka.

Jengo hilo linaelezwa kuporomoka mapema leo Jumamosi Novemba 16, 2024. Taarifa za awali kutoka kwa mashuhuda, zinaeleza ndani ya jengo hilo la kibiashara, kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa wakifanya ununuzi katika maduka ya jengo hilo.

Shughuli ya uokoaji inaendelea kwa wananchi wakishirikiana na vyombo vya dola ikiwemo Jeshi la Zimamoto na Ukoaji.

Hadi saa 5 asubuhi bado hakuna taarifa ya moja kwa moja juu ya athari zilizosababishwa na kuporomoka kwa jengo hilo.

Kwa mujibu wa mashuhuda, ghorofa hilo lilianguka ghafla majira ya saa 3:05 asubuhi wakati mafundi wa ujenzi walipokuwa kazini wakitoboa kwa ajili ya kuongeza sehemu ya maduka.

"Tulianza kusikia kelele za mtingishiko, kisha kwa ghafla jengo zima likaanguka, wananchi wameshindwa kujiokoa na kazi ya  ujenzi ilianza tangu jana, hivyo angetaka urahisi angebomoa tu jengo lote," amesema mmoja wa mashuhuda, Harrison Shayo.

Akizungumza mmoja wa waokoaji ambaye ni askari wa jiji,  Ibrahimu Mussa amesema amewasaidia watu zaidi ya 10 ambao aliwaona kwa karibu huku wakibaki wengine katika eneo la korido.

"Nilifika kwenye usawa wa ngazi na kuwasaidia baadhi yao kwa kuwashika mkono na kuwavuta nje waliobaki . Wengi wao wapo chini na nimetoka kwa sababu ya kuzidiwa na hali ya hewa," amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert  Chalamila na kamati ya usalama mkoa huo imekwishafika eneo hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari na wananchi waliopo hapo, Chalamila amesema majeruhi waliookolewa wamefikishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Hata hivyo, amesema hadi sasa idadi ya majeruhi haijafahamika wala waliopoteza maisha,  akisisitiza takwimu rasmi zitatolewa baadaye.

Jengo hilo  linaelezwa kuwa lilianguka  saa tatu asubuhi, huku likiwa na zaidi ya asilimia 90 ya wafanyabiashara katika maduka hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi na Naibu Spika, Mussa Zungu nao wapo eneo la tukio


Kauli ya Muliro kuhusu waliookolewa

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema idadi ya watu waliokolewa ni kubwa na wachache wamepata majeraha.

"Watu wengi wameokolewa na kazi kubwa inaendelea," amesema Muliro akiwa mtaa wa Mchikichi na Congo eneo lilikotokea ajali ya ghorofa kuporomoka leo Novemba 16, 2024.

Jengo hilo la ghorofa tano linaelezwa kuwa liliporomoka saa tatu asubuhi likiwa na wafanyabiashara ndani.

Katika eneo la tukio, umati umejitokeza kufanya kazi ya uokozi, huku Jeshi la Polisi likitahadharisha watu kukaa mbali ili kuliachia kazi Jeshi hilo.

Hata hivyo, wananchi wanaendelea kusogea katika eneo hilo wengine wakilinda mali zilizotapakaa ardhini.

Vilio huibuka pale mtu anapookolewa katika jengo hilo.


Rais Samia atoa pole, maagizo ajali ya jengo kuporomoka Kariakoo

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za pole kufuatia ajali ya jengo la ghorofa nne lililoporomoka Kariakoo mkoani Dar es Salaam.
Jengo hilo limeporomoka asubuhi ya leo Jumamosi Novemba 16, 2024, huku jitihada za kuwanasua walionasa katika vifusi vya jengo hilo zikiendelea.

Kupitia akauti yake ya Instagram, Rais Samia ameandika; “Nimesikitika kupokea taarifa ya ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa katika Kata ya Kariakoo, Wilaya ya Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam.

“Nimeuagiza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, na Idara ya Menejimenti ya Maafa kufanya kila linalowezekana kufanikisha zoezi la uokoaji na tiba kwa majeruhi.”

“Wakati hilo likiendelea na tukimuomba Mwenyezi Mungu awape pona ya haraka majeruhi, tuwaombee pia tulivu na subra ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wenzetu wanaotafuta riziki zao katika eneo hili muhimu kibiashara nchini ambao kwa namna mbalimbali wameathiriwa na ajali hii.,” ameandika Rais Samia.
 

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali