Prime
Gharama kumwona daktari, viwanda vya dawa vyazua jambo bungeni
Muktasari:
- Shabiby asema yupo tayari hata kupelekwa kamati ya maadili ili kuwataja wabunge anaodai wanahusika katika kuchelewesha na kukwamisha uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini.
Dodoma. Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby ameibua mjadala mzito bungeni baada ya kudai kuwepo kwa mtandao wa watu wenye masilahi binafsi wanaokwamisha uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini, ili waendelee kufaidika na biashara ya uagizaji wa dawa kutoka nje.
Shabiby ametoa madai hayo leo Jumanne Mei 12, 2026 wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumzi ya Wizara ya Afya bungeni, akisema yupo tayari hata kupelekwa katika Kamati ya Maadili ya Bunge iwapo atahitajika, ili kuwataja watu anaodai wanahusika na hujuma hizo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, baadhi ya watu wamekuwa wakihujumu juhudi za Serikali za kujenga uwezo wa ndani wa uzalishaji wa dawa, jambo ambalo linaendelea kuiweka Tanzania katika utegemezi mkubwa wa dawa kutoka nje ya nchi.
Amesema hali hiyo ina madhara makubwa kwa wananchi kutokana na gharama za dawa kuwa kubwa pamoja na changamoto za upatikanaji wake.
“Hii ni zaidi ya madawa ya kulevya. Kuna watu wanazuia viwanda vya dawa visiwepo ili wananchi waendelee kununua dawa kwa gharama kubwa huku wao wakinufaika na biashara hiyo,” amesema Shabiby.
Amesema Tanzania haiwezi kuendelea kutegemea uagizaji wa dawa wakati ipo fursa ya kujenga viwanda vya ndani vitakavyosaidia kupunguza gharama na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa dawa muhimu.
Shabiby amesema Serikali tayari imetenga eneo la ekari 400 kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya dawa, lakini utekelezaji wa mradi huo unaendelea kwa kasi ndogo.
Amevitaka vyombo vya usalama kusaidia kulinda masilahi ya taifa kwa kuhakikisha uwekezaji huo unafanikiwa na kuondoa vikwazo vinavyochelewesha maendeleo katika sekta hiyo.
Amemwambia Waziri wa Afya kuwa changamoto zilizopo katika sekta hiyo, zinahitaji usimamizi makini ili kuzuia masilahi binafsi yasivuruge mipango ya Serikali.
Mbunge huyo amesema Tanzania hutumia zaidi ya dola1 bilioni za Marekani sawa na zaidi ya Sh2.7 trilioni, kuagiza dawa kutoka nje kila mwaka.
Kwa mtazamo wake, hali hiyo inaliweka taifa katika hatari endapo kutatokea migogoro ya kimataifa au changamoto za usafirishaji wa bidhaa.
“Leo Iran na Marekani wakipigana na dawa zikazuiwa kuingia, kuna siku tutakosa hata panadol,” amesema.
Pia ameeleza wasiwasi wake kuhusu ubora wa baadhi ya dawa zinazopatikana nchini, akisema aliwahi kupata uzoefu nje ya nchi ambapo alipewa dawa zenye ubora tofauti na zile alizokuwa akitumia Tanzania.
Mbali na suala la viwanda vya dawa, Shabiby ameitaka Serikali kuharakisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, akisema wananchi wa mkoa huo wanahitaji huduma za kibingwa karibu yao huku miundombinu ya hospitali ya sasa ikiwa chakavu.
Wachumi waunga mkono hoja
Kauli za Shabiby zimeungwa mkono na mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo aliyesema uwekezaji wa viwanda ni msingi muhimu wa maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo, Profesa Kinyondo amesema viwanda vina mchango mkubwa katika kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya Serikali kupitia kodi na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Amesema nchi isiyo na viwanda hulazimika kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza bidhaa muhimu, hali inayoweza kuathiri thamani ya fedha ya ndani na kudhoofisha uchumi.
“Unaponunua dawa au bidhaa nyingine kutoka nje, unatumia dola badala ya shilingi. Lakini bidhaa zikizalishwa hapa nchini, fedha hizo hubaki ndani ya uchumi wetu,” amesema Profesa Kinyondo.
Ameongeza kuwa kukwamisha uwekezaji wa viwanda ni sawa na kuhujumu uchumi wa taifa na kupendekeza kuwepo kwa vitengo maalumu vya ujasusi wa kiuchumi ndani ya vyombo vya usalama ili kudhibiti vitendo vya aina hiyo.
Amesema uwepo wa viwanda vya dawa nchini utasaidia kuboresha upatikanaji wa dawa kwa wakati na kuongeza tija ya nguvu kazi kutokana na wananchi kuwa na afya bora.
Gharama kumuona daktari
Wakati huohuo, baadhi ya wabunge wameendelea kuhoji mfumo wa malipo ya kumuona daktari katika hospitali za umma, wakisema unaongeza mzigo kwa wananchi na unaweza kuwafanya baadhi ya wagonjwa kushindwa kupata huduma kwa wakati.
Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara amesema utaratibu wa wagonjwa kulipia kumuona daktari au nesi unawaumiza wananchi wa kipato cha chini, hasa waliopo vijijini.
“Huu mpango si mzuri. Siku hizi hata vijijini mtu anaambiwa alipe Sh5,000 ili amuone nesi. Hii si sawa,” amesema Waitara.
Amesema madaktari na wauguzi tayari ni watumishi wa Serikali wanaolipwa mishahara, hivyo gharama hizo zinaongeza mzigo usio wa lazima kwa wananchi.
Pia amehoji mfumo wa bima ya afya kwa wabunge, akisema haujazingatia watu wanaowategemea wabunge, wakiwamo wazazi na ndugu wengine wanaosaidiwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bunda Vijijini (CCM), Mwita Getere amesema gharama za kumuona daktari zinaweza kuwa kikwazo kwa wagonjwa wenye hali ngumu na kuwafanya waache kutafuta matibabu mapema.
Ametoa mfano wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, kuwa wagonjwa hulipa Sh25,000 kumuona daktari siku za kawaida na hadi Sh70,000 mwishoni mwa wiki.
“Haya ni maumivu kwa mgonjwa hata kabla hajaanza kutibiwa,” amesema Getere.
Hata hivyo, akizungumzia hilo nje ya Bunge, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Mugisha Nkoronko amesema malipo ya kumwona daktari ni sehemu ya gharama za uendeshaji wa hospitali na si fedha zinazokwenda moja kwa moja kwa daktari anayemhudumia mgonjwa.
Amesema fedha hizo husaidia kugharamia huduma mbalimbali ikiwamo vifaa tiba, uendeshaji wa hospitali na kuboresha huduma kwa wagonjwa.
Pamoja na hayo, Dk Nkoronko amesisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kuboresha mfumo wa bima ya afya kwa wote, ili wananchi wengi zaidi waweze kupata huduma bila kuathiriwa na gharama kubwa za matibabu.
Ushauri mitandaoni
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Clayton Chipando maarufu Baba Levo ameishauri Wizara ya Afya kuanzisha kitengo maalumu cha kutoa elimu ya afya kupitia mitandao ya kijamii ili kudhibiti ongezeko la taarifa potofu zinazotolewa na watu wasiokuwa wataalamu wa afya.
Akichangia mjadala wa hotuba ya Wizara ya Afya bungeni, Baba Levo amesema wananchi wengi hupokea ushauri unaokinzana kuhusu afya na lishe kupitia mitandao ya kijamii, hali inayoweza kuathiri ustawi wa jamii.
Amesema baadhi ya maelekezo yanayotolewa mitandaoni hayazingatii mazingira halisi ya maisha ya Watanzania, hususan wananchi wa vijijini ambao hutegemea vyakula vya asili kwa maisha yao ya kila siku.
“Unaweza ukalala ukaamka unaambiwa usile ugali, wakati watu wengi vijijini hicho ndicho chakula chao kikuu,” amesema Baba Levo.
Mbunge huyo pia ameitaka Serikali kuingiza gharama za huduma za magari ya wagonjwa katika mfumo wa bima ya afya kwa wote ili kupunguza changamoto zinazowakabili wagonjwa wanaopewa rufaa kwenda hospitali nyingine.
Amesema wagonjwa wengi hukumbana na mateso makubwa wanapohitaji huduma za usafiri wa matibabu kutokana na gharama kubwa za magari ya wagonjwa.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Micheweni, Hamis Vuai amesema baadhi ya mataifa, ikiwemo China, tayari yameweka mifumo maalumu inayoruhusu ushauri wa afya kutolewa na watu waliothibitishwa na mamlaka husika pekee.
Amesema hatua hiyo imekuwa msaada mkubwa katika kupunguza upotoshaji wa taarifa za afya kwa wananchi kupitia majukwaa ya kidigitali.
Katika mjadala huo huo, wabunge kutoka mikoa ya Tabora na Kigoma waliibua mvutano kuhusu eneo la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda, huku kila upande ukisisitiza hospitali hiyo ijengwe katika mkoa wao.
Mbunge wa Urambo (CCM), Margaret Sitta, amesema Mkoa wa Tabora tayari umetenga eneo kubwa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo na hivyo hauoni sababu ya mradi huo kuhamishiwa mkoa mwingine.
Hata hivyo, wabunge wa Kigoma wakiongozwa na Baba Levo wamesisitiza kuwa hospitali hiyo inapaswa kujengwa Kigoma kutokana na nafasi yake ya kijiografia kama mkoa wa mpakani.
Wamesema ikijengwa huko, inaweza kuhudumia pia wagonjwa kutoka nchi jirani na wakati huohuo kusaidia kukuza utalii wa tiba nchini.