Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mchengerwa: Watakaokwamisha viwanda vya dawa kushughulikiwa

Waziri wa Afya Mohamed Mchengelwa akiwasilisha  Makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027 katika Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo bungeni leo asubuhi, Mbunge wa Gairo (CCM) Ahmed Shabiby  aliibua hoja nzito kuhusu kile alichodai kuwa ni mtandao wa watu wenye maslahi binafsi wanaokwamisha uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini ili kuendelea kufaidika na biashara ya uagizaji wa dawa kutoka nje.

Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali haitarudi nyuma katika mpango wa ujenzi wa viwanda vya dawa nchini, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaojaribu kukwamisha mchakato huo.

Akihitimisha mjadala wa bajeti ya Wizara ya Afya bungeni leo Mei 12, 2026, Mchengerwa ameyasema hayo leo Mei 12, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge 59 kuhusu mjadala wa bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Mchengerwa amesema Serikali imejipanga kuhakikisha Tanzania inaongeza uwezo wa kuzalisha dawa ndani ya nchi ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.

Katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo bungeni leo asubuhi, Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby  aliibua hoja nzito kuhusu kile alichodai kuwa ni mtandao wa watu wenye maslahi binafsi wanaokwamisha uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini ili kuendelea kufaidika na biashara ya uagizaji wa dawa kutoka nje.

Mbunge huyo alisema yupo tayari hata kupelekwa Kamati ya Maadili ili kuwataja watu anaodai wanahusika katika kuchelewesha uwekezaji huo.

Akijibu hoja hiyo, Mchengerwa amesema Serikali tayari ina orodha ya watu wanaodaiwa kuzuia jitihada za uwekezaji katika sekta ya dawa na kwamba hatua zitachukuliwa dhidi yao.

“Mchakato wa ujenzi wa viwanda vya dawa si maamuzi ya Mchengerwa wala Wizara ya Afya pekee, ni maamuzi ya Taifa. Yeyote atakayejaribu kukwamisha mchakato huu tutashughulika naye, hatutamuacha,” amesema.

Amesema Tanzania haiwezi kuendelea kutegemea uagizaji wa dawa kutoka nje wakati ikiwa imepita zaidi ya miaka 60 tangu kupata uhuru huku uzalishaji wa ndani ukiwa chini ya asilimia 16.

“Kipindi cha Uviko-19 kilituonyesha umuhimu wa kujitegemea katika uzalishaji wa dawa. Ni lazima sasa tuzalishe dawa sisi wenyewe kama Taifa,” amesema.

Waziri huyo amesema Rais Samia Suluhu Hassan alimpa jukumu maalumu la kusimamia maendeleo ya viwanda vya dawa mara baada ya kumteua kuongoza Wizara ya Afya.

Amesema ndani ya miezi mitatu iliyopita Serikali imezindua eneo maalumu la uwekezaji wa viwanda vya dawa Mloganzila na tayari imesaini hati ya makubaliano na Uingereza kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa dawa nchini.

“Juzi tumezindua hub ya Mloganzila ya uzalishaji wa dawa na tayari tumekabidhi eneo hilo pamoja na kusaini makubaliano na Uingereza. Kwa mara ya kwanza sasa tutaanza kuzalisha dawa sisi wenyewe,” amesema.

Mbali na hilo, Mchengerwa amesema wabunge 59 wamechangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Afya huku zaidi ya wabunge 19 wakizungumzia suala la bima ya afya kwa wote.

Amesema michango hiyo inaonyesha namna ambavyo viongozi wanapaswa kujitolea kwa ajili ya wananchi na kuhakikisha huduma muhimu za afya zinapatikana.

“Watanzania watamkumbuka Rais Samia kwa kazi kubwa anayofanya. Nchi hii ni ya kijamaa, kusaidiana na kujitegemea, hivyo viongozi lazima tufanye kazi kwa bidii na kukusanya kodi ili kusaidia maendeleo ya nchi,” amesema.


Maagizo Mkoa wa Shinyanga

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amewataka viongozi wa Mkoa wa Shinyanga kutafuta suluhisho la haraka la ujenzi wa chumba cha huduma ya dialysis badala ya kusubiri fedha za bajeti ya mwaka ujao.

Amesema haikubaliki kwa mkoa wenye shughuli kubwa za kiuchumi na wadau wa maendeleo kushindwa kupata Sh200 milioni za kuanzisha huduma hiyo muhimu kwa wagonjwa wa figo.

“Tunalia tunahitaji milioni 200 kutengeneza chumba cha dialysis wakati kuna viongozi wa mkoa, wadau wa maendeleo na taasisi za kifedha. Hii haikubaliki hata kidogo,” amesema.

Mchengerwa amesema ametoa mwezi mmoja kwa viongozi wa afya wa mkoa huo kuhakikisha wanapata fedha hizo, akionya kuwa atachukua hatua iwapo watashindwa.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kutoa huduma za afya kwa wananchi hata pale wagonjwa wanaposhindwa kumudu gharama za matibabu.

Amesema zaidi ya Watanzania milioni 40 walipata huduma katika vituo vya afya nchini katika mwaka wa fedha uliopita huku hospitali mbalimbali zikitoa misamaha ya mabilioni ya fedha kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ilitoa misamaha yenye thamani ya Sh1.9 bilioni kwa wagonjwa wa moyo, Ocean Road Cancer Institute ikatoa zaidi ya Sh12 bilioni, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) zaidi ya Sh7 bilioni huku Hospitali ya Taifa Muhimbili ikitoa misamaha ya Sh19 bilioni.

Hospitali nyingine zilizotajwa ni KCMC iliyotoa zaidi ya Sh6 bilioni na Bugando iliyotoa zaidi ya Sh4 bilioni kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kulipia huduma.