Gharama za kuwaona madaktari kero kwa wabunge
Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Waitara amesema utaratibu wa kumuona daktari umetengenezwa bila kuangalia hali za maisha ya watu wa vijijini na umechukuliwa katika baadhi ya maeneo kama kizuizi cha kuwafikia wataalamu.
Dodoma. Wabunge wamehoji gharama za malipo kabla ya kumuona daktari kwamba ni miongoni mwa kero zinazotakiwa kuondolewa kwani zinaumiza wagonjwa.
Wakichangia hotuba ya Wizara ya Afya leo Jumanne Mei 12, 2025, wabunge wamesema gharama hizo zinaongeza mzigo kwa wananchi bila sababu za msingi wakati madaktari ni watumishi wanaolipwa na Serikali.
Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara amesema suala la kumuona daktari ni kero kubwa na kwamba linaongeza mzigo usio na ulazima kwa watu wenye kipato cha chini, lakini akahoji iweje mtumishi aliyeajiriwa alipiwe gharama za kumuona.
Waitara amesema utaratibu wa kumuona daktari umetengenezwa bila kuangalia hali za maisha ya watu wa vijijini na umechukuliwa katika baadhi ya maeneo kama kizuizi cha kuwafikia wataalamu.
“Huu mpango siyo mzuri, gharama za matibabu kwa wagonjwa zinakuwa kubwa pasipo sababu za msingi. Siku hizi hadi vijijini mtu anaambiwa alipie Sh5,000 ili amuone nesi. Mheshimiwa Mwenyekiti, hii siyo sawa kabisa. Jambo hili likomeshwe,” amesema Waitara.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, kitendo hicho kingeweza kuzuilika ikiwa Serikali ingekuwa na mfumo wa pamoja badala ya kuweka mambo tofauti tofauti, kwani kinaweka matabaka kwenye matibabu.
Akizungumzia suala la bima ya wabunge, amesema nalo limekuwa na ubaguzi kwani limewatenga watu wanaosaidiwa na wabunge, wakiwemo wazazi, badala yake linaangalia wabunge pekee, jambo alilotaka libadilishwe haraka.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bunda Vijijini (CCM), Mwita Getere amesema kulipia kumuona daktari ni kitanzi kinachoweza kusababisha vifo kwa wagonjwa kwani mtu anapokwenda hospitali anawaza gharama za kuanzia kwa daktari, na akiona ni shida anaamua kuacha.
Hata hivyo, Getere ametaja alichokiita ajabu inayoshangaza kwamba gharama za kumuona daktari zinatofautiana kutoka hospitali moja kwenda nyingine hata kama hospitali hizo zina hadhi inayolingana. Pia amehoji kwa nini kila siku ina gharama zake.
“Mfano mzuri ni hapa Hospitali ya Benjamin Mkapa. Ukienda kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, gharama za kumuona daktari utatozwa Sh25,000, lakini ukienda Jumamosi na Jumapili huwezi kumuona daktari hadi umelipia Sh70,000. Hii ni nini?” amesema Getere.
Mbunge huyo amesema malipo hayo ni maumivu kwa mgonjwa kabla ya kufikia hatua ya kutibiwa. Pia amehoji kwa nini yawekwe malipo wakati wahusika wanalipwa mishahara na Serikali kama ilivyo kwa watumishi wengine wote kwenye vitengo na idara tofauti.
Katika hatua nyingine, wabunge wa mikoa ya Kigoma na Tabora wamejikuta kwenye mvutano kuhusu wapi ijengwe Hospitali ya Rufaa ya Kanda kwani kila mkoa umetengewa eneo na Serikali imewapa mkanganyiko.
Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta amesema hadi sasa wanashindwa kuelewa kwa nini hospitali hiyo isijengwe Tabora mahali walipotenga eneo kubwa tangu muda mrefu, na kwamba haipendezi kupokea taarifa tofauti kuhusu ujenzi wa hospitali mkoani humo.
Hoja ya Sitta ilikuja baada ya wabunge wengine kutoka Tabora, akiwemo Mbunge wa Nzega Vijijini, Neto Kapalata, kutaka Serikali isihamishe ujenzi wa hospitali hiyo na kuipeleka mkoa mwingine.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Clayton Chipando pamoja na wabunge wa Viti Maalum wamesema hospitali hiyo inapaswa kujengwa Kigoma kwani ni mkoa wa mpakani utakaosaidia kuhudumia hata nchi jirani, hivyo kukamilisha wazo la kufanya utalii wa tiba.