Ecobank yajivunia faida Sh3.5 bilioni

Muktasari:
- Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo anasema ufanisi huo ulichangiwa na kupungua kwa gharama mbalimbali pamoja na uwiano wa mikopo chechefu (NPL) kuwa chini ya asilimia 3 kwa miaka miwili iliyopita.
Dar es Salaam. Katika kipindi cha robo mwaka wa 2024, Benki ya Ecobank Tanzania imefanikiwa kupata faida ya Sh3.5 bilioni ambayo ni mara tano zaidi ya ile iliyopatikana katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Juni 10, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Ecobank Tanzania, Dk Charles Asiedu amesema matokeo ya robo ya kwanza ya mwaka ni mwendelezo wa utendaji mzuri ambao benki iliupata mwaka 2023.
"Katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka, mapato yaliongezeka kwa asilimia 66 hadi karibu Sh10 bilioni, ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka 2023. Hii inatokana na kuongezeka kwa mikopo iliyotolewa kusaidia shughuli za kiuchumi nchini na ongezeko la kasi ya biashara ilioimarishwa na kukubalika kwa huduma mbalimbali za benki kwa wateja," amesema.
Mkurugenzi huyo amesema ufanisi huo pia ulichangiwa na kupungua kwa gharama mbalimbali pamoja na uwiano wa mikopo chechefu (NPL) kuwa chini ya asilimia tatu kwa miaka miwili iliyopita.
Dk Asiedu amesema amana za benki hiyo ziliongezeka kwa asilimia 68 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja hadi Sh313 bilioni, jambo ambalo lilichochea ukuaji wa mali kwa asilimia 27 hadi kufikia Sh415 bilioni.
“Kutokana na ukuaji mkubwa wa amana, tuliweza kusaidia biashara za wateja wetu, kwani tuliongeza mikopo yetu kwa zaidi ya Sh65 bilioni hadi Sh157 bilioni kutoka Sh90 bilioni,” amesema Dk Asiedu.
Kadhalika, Dk Asiedu amesema Ecobank Tanzania katika mwaka 2023 mapato yake yalifikia Sh31.26 bilioni, kutoka Sh21.11 bilioni mwaka 2022 huku uwiano wa gharama kwa mapato ya benki ukipungua kutoka asilimia 90.56 mwaka 2022 hadi asilimia 65.1 mwaka 2023.
Katika mkutano huo, mkuu wa kitengo cha wafanyabiashara wadogo na kati, Joyce Ndetabura amesema kama benki imewapa kipaumbele wateja wa chini na kati na mara zote wamekuwa wakiangalia namna ya kuwasaidia.
“Katika kuangalia hilo tunajua moja ya tatizo linalowakumba wafanyabiashara ni kupata mikopo, wengi wanakuwa hawana elimu ya kujua mkopo gani utamsaidia katika biashara yake, wengi wanadhani benki tunahitaji kujua mapato yake, ili kumpa mkopo. tunachokifanya sisi ni kuhakikisha tunamweka mtu ambaye atakuwa anawaangalia kwa ukaribu,” amesema Joyce.