Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kupandikiza mimba Muhimbili Sh14 milioni, wadau wakosoa gharama

Muktasari:

  • Jumla ya wenza 2000 wamejitokeza kuhitaji usaidizi wa kupata watoto katika kitengo IVF Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Dar es Salaam. Wakati Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ikitimiza miezi minane tangu kuanzishwa rasmi wa kitengo cha upandikizaji mimba Vitro Fertilization (IVF), gharama za huduma hiyo zimetajwa ni Sh14 milioni, huku wadau wakishauri Serikali isaidie kwa wasiojiweza.

Kwa mujibu wa Muhimbili, gharama hizo ni tofauti na vipimo vya awali na wamejaribu kuwapa nafasi watu ambao wana bima zao katika kipengele cha kufanya vipimo.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa kitengo cha IVF Muhimbili, Dk Matilda Ngarina alipofanya mahojiano maalumu na Mwananchi mapema wiki hii.

Amesema waliamua kuvunjavunja kwa kuona ni wapi ambako bima inalipia na kama hailipii, waliweka bei inayohusika kwa kuwa,  kuna mwingine anaweza kutibiwa kwa bei ndogo sababu ana bima na mwingine ikawa kubwa sababu hana bima.

Pia, amesema inatofautiana na aina ya matatizo aliyonayo, hivyo bei zinatofautina mgonjwa mmoja na mwingine.

"Wanaweza kuja wanandoa baba na mama wanataka mtoto, lakini wameshakuwa watu wazima hawana mbegu, watakuwa na kazi ya kumuandaa mama na kuandaa kijana wa kumpa baba mbegu, gharama ya wale haitafanana na mtu anayekuja kijana mdogo ana nguvu zake ambaye labda pia ana bima, isipokuwa kwa wenye gold kadi za NHIF," amesema Dk Ngarina.

"Kuna kile kipengele cha kuanzia sindano za utoaji mayai mpaka kuja kuhifadhi kwa ajili ya kupandikiza, hicho kipengel e wote wanalipa sawa ambayo ni Sh14 milioni sasa vitu vingine vinakuja kuongezea kutokana na una shida ipi na unatakiwa ufanye nini."

Hata hivyo, gharama hizo zimepokewa tofauti na wadau mbalimbali wakitaka Muhimbili ifikirie upya kupunguza gharama, huku wengine wakiitaka serikali kusaudia wasiojiweza.

Neema Athanas (37) anashauri gharama ipunguzwe ili wanaotafuta watoto wasaidiwe, akisema si wote wana uwezo.

Neema aliyepata mtoto kwa njia ya upandikizaji miaka miwili iliyopita, amesema gharama ni kubwa hospitali zingine na matumaini yake angeongeza mtoto wa pili Muhimbili.

"Sasa ukiangalia gharama hazitofautiani sana, tulidhani Muhimbili kungekuwa na nafuu. Nawafikiria wale wasio na uwezo kabisa ina maana watakufa bila watoto? Serikali ifikirie kuweka ruzuku pale IVF," amesema Neema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wagumba Tanzania, Shamila Makwenjula amesema gharama hizo zipo juu hata anayetibiwa matatizo ya uzazi. 

Amesema wadau wanapodhamini au kusaidia mambo mengine nao iwe hivyohivyo, wengi wanapata sonona, ukatili na unyanyapaa mpaka kuiba watoto bila kujua madhara.

"Sio kwamba wote wagumba, wengine wakipata matibabu wanazaa kawaida, lakini inashindikana kutokana na gharama kuwa juu.

"Wengi kutoka kijijini kuja Muhimbili wanashindwa, kama hauwezi usafiri wa kawaida milioni 14 ataweza? Nashauri wagumba tuangaliwe, kama Serikali wanavyolipia kwenye mambo mengine watusapoti na sisi tupate watoto tuwe na furaha," amesema Shamila.

Hata hivyo, Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema:"Huduma za uzazi saidizi ni ghali, sio kwa kila mtu, ni kwa wale wenye shida tu, gharama za uwekezaji ni kubwa, na uendeshaji ni kubwa."



Upandikizaji kuanza Mei

Akizungumzia hatua za upandikizaji, Dk Ngarina amesema mpaka sasa jumla ya wenza 11 wamefanikiwa kuvuka katika hatua za awali.

Idadi hiyo ni kati ya wenza 31 walioanza hatua za awali za uvunaji wa mayai na mbegu za kiume, kisha kuunganishwa maabara na kufanikiwa kutengeneza kijusi, kabla ya upandikizaji vijusi hivyo katika tumbo la mama.

Amesema mpaka sasa wametoa huduma kwa makundi matatu, walianza kundi la kwanza lenye wenza watano Desemba mwaka jana, kundi la pili lenye wenza 13 Februari mwaka huu na kundi la tatu lenye wenza 13 mapema mwezi huu.

"Kundi la kwanza lilikuwa na wagonjwa watano, kati yao watatu ndiyo waliweza kukidhi vigezo mpaka hatua ya mwisho ya kunyonywa mayai na kutengenezwa embryo 'kijusi' baada ya muunganiko ya yai la mama na mbegu ya baba na kutengeneza kijusi ambacho tumekifreeze (kugandisha) maabara.

"Kundi la pili tulikuwa na kinamama 13 kati ya hao, wanane ndiyo walikwenda vizuri mpaka mwisho na kuweza kutengeneza vijusi ambavyo vipo frozen.

"Sasa hivi tuna wamama 13 ambao wameanza matibabu ya kuja kunyonywa mayai na katika kundi hili ndiyo kwa mara ya kwanza kumeanza kutumia mbegu kutoka kwa donors ‘wachangiaji’ huko nyuma tulikuwa tunatumia wenza wao," amesema Dk Ngarina.

Amesema kwa sasa katika upandikizaji, wanasayansi wanashauri kitu kinaitwa ‘freeze all’ alimaanisha kugandisha kwanza 'kijusi', akisema zamani baada ya mbegu na yai kurutubishwa maabara baada ya siku tatu mama alipandikizwa.

Lakini sasa wakabaini ukimpandikiza hapohapo, kunakuwa hakuna matokeo mazuri ikilinganishwa na kuhifadhiwa kwa muda, mwili wa mama ukapumzika.

Amesema shughuli ya kupandikiza ni kazi kubwa, tofauti na wengi hudhani mama atafika na kuvunwa mayai na kupandikizwa.

"Ni shughuli ndefu ya maandalizi, lazima mwili ukae sawa ijulikane shida ni nini, tuamue kwamba utapewa huduma namna gani ya kuuandaa mwili, tuanze kukuchoma zile sindano, twende chumba cha upasuaji tuvune yale mayai, tuyarutubishe na kuyaunganisha na mbegu, halafu yaachwe yaatamie yatengeneze kijusi.

"Vijusi navyo vinakuwa na hatua au ubora mbalimbali, tunavipa ubora kusema hiki bora, bora kidogo na hiki hakifai, kwa hiyo unaweza ukaanza vizuri mpaka unafika mwisho kuja kutengeneza kijusi unakuta kijusi hakifai kabisa," amesema Dk Ngarina.

"Ndiyo maana unaona tunaanza na wengi, lakini wengine wanatengeneza kijusi ambacho hakina mfumo mzuri, kwa hiyo ile hatua ya ya kumwandaa mama mpaka aje atengeneze kijusi huwa tunataka atengeneze mayai mengi, ili usije ukarudia tena kuja kumchoma yale masindano huwa yana stress sana, hiyo huwa inafanya mwili wake unabadilika."

Dk Ngarina amesema mama akivunwa mayai hata kizazi huwa kikubwa kule anakolala mtoto, kwa hiyo hushauriwa mama akishanyonywa mayai kumuacha mwili wake kwanza urudi kawaida, kabla ya kumwandaa kwa ajili ya kumpandikiza.

Amesema kwa makundi ya awali yenye wanawake 31, 11 kati yao vijusi vipo vizuri kwa sasa wanawaandaa kupandikiza baada ya kuacha miili yao ikae vizuri na pia kulikuwa kuna hatua za kuangalia nyumba ya uzazi kwa ndani.

Amesema baada ya kunyonya mayai kabla ya kuja kupandikiza, lazima kuangalia nyumba ya uzazi ina hali gani kuhakikisha hakuna uvimbe, ghasia yoyote itakayozuia mimba isishike, kwa hiyo wameshawafanyia vipimo na vizazi vyao vimeshatulia vizuri na wao wenyewe wako tayari kubeba mimba.

"Tutapandikiza wiki ya kwanza ya Mei ndiyo hatua ambayo tuko sasa hivi."

Dk Ngarina amesema hawajaenda haraka sana kwa sababu baada ya watu kusikia Muhimbili wanapandikiza na walipata wagonjwa ambao ni wagumu kimatibabu.

"Wengi waliokuja wameshapita mahali kadhaa wameshindikana huku na kule, kwa hiyo wanakuja wagonjwa wagumu sana na maandalizi yao wengi wanahitaji msaada ya mayai ya mtu mwingine au mbegu ya mtu mwingine.

"Sasa maandalizi ya kupata mbegu ya mtu mwingine ambayo ni nzuri nayo siyo kitu cha siku moja, huwezi kwenda barabarani tu ukasema jamani naomba mbegu hapana ni kazi tunafanya kama ya kikachero kutafuta watu katika hali ya chini."


Alipoulizwa iwapo mama asipofanikiwa kupata mtoto licha ya kulipia Sh14 milioni, gharama zitakuwaje amejibu, "inategemea ameishia wapi na ameshatumia kiasi gani kulingana na ile fedha aliyoiweka na anaweza kurudia mara kadhaa, kama tukiona ana changamoto  tunaweza kumshauri kurudia au vinginevyo wagonjwa hawafanani."

Amesema Muhimbili wanaendelea kupata uzoefu walishirikiana na waliowafungia mashine.

Sayansi ya kugandisha vijusi

Unaweza kujiuliza inakuwaje kijusi kinapohifadhiwa kwenye barafu kwa miezi kadhaa kabla ya kupandikizwa, hii ni sayansi na hapa Dk Ngarina anafafanua,"kinachotokea siyo unamchukua tu na kumweka kwenye friji kama nyama hapana, kile kijusi kinawekwa katikati ya 'media' ni kama kuna maji ambayo yanasaidia uhai wake, yapo kwenye tube inawekwa kule ndani anakaa, anakuwa kama yuko hai ile media inamzunguka.

"Ni kama wale wanyama anaokaa kwenye barafu hawafi na barafu ikiisha anakuwa yuko sawa, vijusi hawa wanawekwa kwenye baridi kubwa ya 290 Degrees Celsius baridi hii haipatikani kwenye friji wakiwa humo wanatulia.”

Dk Ngarina amesema  kuna namna ya kumrudisha katika hali ya kawaida kwa kujiyeyusha yeye mwenyewe akitoka pale anaendelea na maisha ya kawaida.

"Kumtoa mpaka kumpandikiza ni masaa manne, kuna hatua za kufanya awe amepoa yuko vizuri na hai na ndipo unamwekea mama, ukimuweka tu kwenye nyumba ya uzazi anajua cha kufanya, anakwenda kujishikiza sababu ni kiumbe anajua kwa kukaa, ni sawa na mtoto akizaliwa hafundishwi kunyonya anajua nini anatakiwa kufanya ili ashibe ni kitu cha asili," amesisitiza.


Mbegu

Alipoulizwa kuhusu uhifadhi wa mayai na mbegu, Dk Ngarina amesema wanaohitaji huduma hiyo wanawashauri wahifadhi katika hali ya kijusi kwa maana wakija kuhifadhi mbegu peke yake au mayai peke yake ubora wake unapungua hasa kwa wanawake.

Hata hivyo, amesema bado hawajaanza kuhifadhi mbegu, isipokuwa wamehifadhi vijusi kwa raia wa kigeni.

Dk Ngarina amesema mpaka mwishoni mwa Mei waliofika kuhitaji upandikizaji  na walioonekana hawawezi kusaidika zaidi ya kupandikiza wamefika 120 kati ya 2000 waliofika katika kituo cha IVF.

"Wamekuja mpaka watu wazima wana miaka 50 mpaka 60, lakini sasa unakuta tayari ana magonjwa, presha, kisukari unamwelekeza tu kwamba kwa afya yako nini unafaa kufanya."