Dk Mpango aguswa na gharama upandikizaji mimba

Muktasari:
- Serikali yaagiza Wizari ya Afya na Wizara ya Fedha kujadiliana kuhusu msamaha wa kodi kwa vifaa vya kupandikiza mimba.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais Dk Philip Mpango amemuagiza Waziri wa Afya, Jenista Mhagama kuzungumza na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba kuhusu msamaha wa kodi wa vifaa vya kupandikiza mimba, ili kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi.
“Nimepata mapendekezo ya msamaha wa kodi kwenye vifaa muhimu katika upandikizaji mimba ili kusaidia kushusha gharama ya huduma. Namwelekeza Waziri wa Afya kukaa na Waziri wa Fedha kuangalia namna ya kutekeleza pendekezo hili na mimi naona ni jambo muhimu,” amesema.
Dk Mpango amesema hayo leo Septemba 12, 2024 alipozindua kituo cha upandikizaji mimba (IVF) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi amesema gharama za upandikizaji mimba hospitalini hapo ni Sh13.12 milioni na tayari watu 10 wanaendelea na utaratibu wa kupata huduma hiyo.
Kwa mujibu wa takwimu za MNH, mwaka 2019 wanandoa 1,200 walikuwa na uhitaji wa watoto, huku takwimu za mwaka 2024 zikionyesha wanawake 3,810 nchini walijitokeza wakihitaji usaidizi wa kupata watoto kati ya Juni na Julai.
Mbali na maagizo hayo, Dk Mpango amesema ili huduma ya upandikizaji mimba iwe endelevu hospitalini hapo, ni muhimu kuondokana na utegemezi wa wataalamu kutoka nje ya nchi.
“Jitihada za makusudi ni lazima zichukuliwe kuwezesha uhamishaji wa teknolojia, Wizara ya Afya andaeni mpango madhubuti wa kuwajengea wataalamu wetu wa ndani uwezo utakaowawezesha si tu kutumia vifaa hivi bali kuvifanyia ukarabati wa kisasa,” amesema.
Profesa Janabi amesema asilimia 35 ya tatizo la kutopata watoto linatoka kwa kina baba na asilimia 65 kwa wanawake.
"Katika wagonjwa 10 wanaofika Muhimbili watatu hadi wanne wana tatizo la kutopata mtoto sawa na asilimia 30 na tatizo hili lipo duniani kwa asilimia 17," amesema.
Profesa Janabi akizungumzia gharama iwapo mtu aliyepandikizwa akashindwa kupata mimba, amesema itategemea na aina ya dawa anazotumia na gharama hubadilika.
Nyumba za NHC
Katika hatua nyingine, Dk Mpango amemuelekeza Waziri Mhagama kufanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi ili majengo mali ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) yaliyopo ndani ya MNH yamilikiwe kwa hospitali hiyo.
Amesema hayo kutokana na ombi lililotolewa awali na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Majengo hayo kwa mujibu wa hospitali hiyo yanatumiwa na wapangaji wengine wasiohusiana na Muhimbili.
Maiti kuzuiwa
Chalamila amemuomba Wazari Mhagama kuwe na sheria inayoelekeza kuhusu utaratibu wa ndugu kuchukua maiti hospitali, kwani amekuwa akipokea malalamiko mengi ya watu kuzuiwa kuchukua miili ya ndugu zao, huku kukiwa na maelekezo kuwa isizuiwe.
Mhagama amewaelekeza wataalamu wa afya kuwahudumia haraka wagonjwa wanaokamilisha utaratibu uliowekwa katika utoaji huduma.
Amesema changamoto zilizopo kwenye sekta ya afya zitatuliwe kupitia utekelezaji wa bima ya afya kwa wote itakapoanza, akiisisitiza hadi Oktoba 15, 2024 mifumo ya huduma ya afya itasomama kuanzia ngazi ya msingi hadi hospitali ya Taifa, lengo likiwa kupunguza gharama wakati wa matibabu.
"Wapo wagonjwa ambao wakifanyiwa vipimo wanapokwenda hospitali nyingine vipimo vinaanza upya, hii inaongeza gharama za matibabu. Kuanzia Oktoba 15 mwaka huu tutahakikisha mifumo yote ya huduma ya afya kuanzia ngazi ya msingi hadi hadi hospitali za rufaa na Taifa mifumo itasomana kuleta unafuu wa gharama kwenye huduma," amesema.
Fahamu haya kuhusu upandikizaji mimba
Kwa mujibu wa wataalamu, yai na mbegu (kiinitete) vyenye umri wa siku mbili hadi nne kimoja au zaidi ya kimoja hupandikizwa ndani ya kizazi kwa kutumia chombo maalumu baada ya kizazi cha mwanamke kuandaliwa.
Mafanikio ya upandikizaji mimba kupata ujauzito au mtoto ni kuanzia asilimia 32 kushuka, inategemea na umri na tatizo alilokuwa nalo mwanamke, huku gharama yake ikitajwa kuwa kati ya Sh10 milioni hadi Sh17 milioni kutegemea na hospitali inayotoa huduma hiyo.
Katika mazungumzo yake aliyowahi kufanya na Mwananchi kuhusu upandikizaji wa mimba, mtaalamu wa magonjwa ya uzazi Hospitali ya Aga Khan, Dk Munawar Kaguta alisema uzazi wa kupandikiza hufanyika baada ya mwanamume na mwanamke kuonekana kuwa na shida.
"Mbegu za kiume zinachukuliwa na yai linatolewa zaidi ya moja kwa kutumia ‘ultra sound’. Kuna vifaa vinatumika kuunganisha vitu hivyo na vikishaungana baada ya muda inachaguliwa moja iliyoonekana kuwa sawa anaingiziwa mwanamke kwenye kizazi ikishika mimba inaendelea kama kawaida, "ameeleza.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, vitu wanavyoviangalia kabla ya mwanamke kupandikizwa ujauzito ni kama ana uvimbe kwenye kizazi au uwepo wa maji kwenye mirija ya uzazi, matatizo ambayo hupaswa kutibiwa kwanza kabla ya kuanza kwa upandikizaji.
Kwa wanaume, daktari huyo amesema wanaangalia utoshelevu wa mbegu zake na endapo itagundulika ana mbegu chache zaidi, teknolojia ya juu zaidi hutumika, lakini kama hana mbegu kabisa jambo hilo kwake litakuwa gumu kutekelezeka.