Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dowuta: Kuhamia DP Word au kubaki TPA ni mchakato shirikishi

Muktasari:

  • Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (Dowuta), wamezungumzia hatua ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ya kuwataka watumishi wanaotaka kwenda DP World kujiorodhesha majina yao kabla ya Machi 29, wakisema mchakato huo ni shirikishi.

Dar es Salaam.  Wakati Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), ikiwataka watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam wanaotaka kuajiriwa na Kampuni ya DP World kuorodhesha majina, Chama cha Wafanyakazi wa Shughuli za Meli na Bandari (Dowuta), kimesema mchakato huo una baraka zao.

Viongozi wa Dowuta wamesema kabla ya kufikia mchakato huo, walijengewa uwezo wao na wafanyakazi wenzao kuhusu suala hilo, ili kila mtumishi kufanya uamuzi sahihi wa kuendelea kubaki TPA au kwenda kufanya kazi DP World.

Juzi, katika tangazo lililotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa kwenda kwa watumishi wa bandari, limesema kutokana na makubaliano yanayohusisha usimamizi na uendeshaji wa maeneo tajwa, watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam wanapaswa kuchagua kati ya kubaki TPA au kusitisha mkataba wa ajira wa TPA na papo hapo kuajiriwa upya na kampuni ya DP World.

Viongozi wa Dowuta wameeleza hayo leo Jumamosi Machi 23, 2024 wakati wakizungumza na Mwananchi Digital lililotaka kujua wamepokea tangazo la Mbossa aliyesema katika mchakato wa uwekezaji bandari “hakuna mtu yeyote atakayepoteza kazi.”

“Elimu imetolewa kuanzia Machi 4 hadi 19 mwaka huu  kwa kuhusisha idara kwa idara, vitengo kwa vitengo na watu walielewa, yule asiyeelewa alipata fursa ya kueleweshwa kwa kina na ilianzishwa kliniki maalumu kwa ajili ya suala hili.”

 “Hili ni takwa la kiserikali, kinachotakiwa ni kufuata taratibu ambazo wafanyakazi wanatakiwa kuwa na uhakika na kile wanachokifanya,” amesema Muharami Manyara ambaye ni mwenyekiti wa Dowuta Taifa.

Manyara amesema hakuna changamoto kati ya TPA na Dowuta kuhusu suala hilo, isipokuwa vyombo vya habari vinawachanganya baadhi haviandiki ukweli uliopo, badala kila wanachoambiwa au kusikia wanakifanyia kazi.

Kwa mujibu wa Manyara, sio wafanyakazi wote wa TPA ndio watakaokwenda DP World na hakuna mtu atakayelazimishwa kwenda katika kampuni hiyo, isipokuwa kwa hiari na utashi wake hasa katika maeneo yanayotakiwa kukodishwa na kampuni hiyo.

“Mtu hawezi kwenda kusaini mkataba DP World kabla ya kuhakikishiwa uhalisia wa kule upoje, kinachofanyika lazima mtumishi aende kule na kuchukua mkataba anausoma karibu siku tatu akishirikiana na wanasheria au washauri wake kabla ya kutoka TPA.”

“Akiona panamfaa kwenda, anasaini mkataba wake, kisha anarudi TPA kusaini mkataba wa kuondoka na anapewa masilahi yake yote kulingana na mkataba wa hali bora uliopo sasa,” amesema Manyara.

Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Dowuta, Edesius Kinunda, hakuwa mbali na maelezo ya Manyara akisisitiza  mchakato huo umeshirikisha viongozi na wafanyakazi kuanzia mwanzo.

“Ndio maana hakuna mfanyakazi aliyepiga kelele mahali popote, kwa sababu kuna ushirikishwaji wa kutosha, hakuna kipengele ambacho menejimenti ya TPA wamefanya peke yao pasipo kujulisha Dowuta, hivyo watumishi wana hiari kubaki au kwenda DP World.

Machi 20, 2024, TPA ilitoa tangazo kwa watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam ikielezea mkataba walioingia na DP World ya Dubai unaohusu uendeshaji wa gati namba 0-3 na gati 4-7 kwa kipindi cha miaka 30.

Oktoba 22, 2023, TPA na DP World zilisaini mikataba mitatu mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Dodoma inayohusu uwekezaji na uendeshaji Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza ufanisi.

Kabla ya kutia saini mikataba hiyo, Serikali iliingia makubaliano na Serikali ya Dubai kuhusu uwekezaji huo (IGA). Mikataba hiyo ni wa nchi mwenyeji (HGA), wa ukodishaji na uendeshaji wa gati 4 – 7, na uendeshaji wa pamoja wa gati 0 – 3 kati ya TPA na DP World kwa shughuli za kibiashara na za kiserikali.

“Lengo la kutoa elimu ni kuwapa watumishi wote uelewa sahihi wa mabadiliko ya uendeshaji yanayoendelea Bandari ya Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine, elimu hiyo inahusisha mabadiliko ya uendeshaji wa bandari, utaratibu wa makabidhiano, mtumishi kusitisha mkataba na TPA na papo hapo kuajiriwa upya na kampuni ya DP World,” linaeleza tangazo hilo.

Imeelezwa elimu pia imejumuisha stahiki ambazo zitatolewa na TPA na kuajiriwa upya na Kampuni ya DP World.

Katika msisitizo imesema mtumishi anatakiwa kufanya hivyo kwa hiari bila kushurutishwa.


“Kwa msingi huo nawajulisha watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam makabidhiano kati ya TPA na Kampuni ya DP World yameanza kutekelezwa. Kwa kuwa hatua ya  utoaji elimu kwa watumishi limekamilika,”imeeleza sehemu ya  tangazo hilo.

Jana  Ijumaa Machi 22, 2024 Akizungumza na Mwananchi Digital Mbossa kupata ufafanuzi wa baadhi ya maswali, ikiwemo kama itatokea hakuna mtumishi hata mmoja atakayejitokeza itakuwaje? na je, kuna hakikisho la kwamba lazima wataajiriwa DP World?

Katika majibu yake, Mbossa amesema; “Hakuna mtumishi yeyote wa TPA ambaye atapoteza ajira yake. Lakini niseme tu mpaka sasa zaidi ya watumishi 70 wamekwishajitokeza.”

Amesema iwapo wasingejitokeza bado wangeendelea kuwa wafanyakazi wa TPA kwa kufanyakazi eneo la DP World na DP World atawalipa TPA mishahara yao ambayo wao (TPA) watawalipa wafanyakazi.

Mbossa amesema wao wana bandari nyingi, wanaweza kuwahamishia zingine.

“Ninachoweza kusisitiza na kuwatoa hofu watumishi, suala hili tunaenda nalo kwa umakini na kama nilivyosema, hakuna mtumishi yeyote wa TPA atakayepoteza ajira yake,” amesema na kuongeza;

“Na iwapo ikitokea watumishi wote wa TPA wakajitokeza kutaka kwenda kuajiriwa na DP World watalipwa stahiki zote, basi tutachukua jukumu la kuajiri watumishi wengine.”