Dk Slaa, Mwabukusi wahojiwa polisi, watoa msimamo

Muktasari:
- Dk Slaa, Mwabukusi na Mdude waliitwa tangu jana Jumatatu na Jeshi la Polisi mkoani Mbeya kwa ajili ya mahojiano na leo Jumanne wamehojiwa na wanatarajia kurudi baada ya siku 14.
Mbeya. Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limewaita na kuwahoji Dk Wilbroad Slaa, Boniface Mwabukusi na Mpaluka Nyagali (Mdude) kwa madai ya kufanya mkusanyiko bila kibali, huku watatu hao nao wakisisitiza msimamo wao wa kupigania maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa huo, Benjamin Kuzaga alipotafutwa kuelezea mahojiano na wanaharakati hao, amesema kwa sasa anaendelea na kikao akiahidi kulifafanua zaidi baadaye.
Akizungumza na Mwananchi jijini hapa leo Oktoba 10, Dk Slaa amesema baada ya kuhojiwa na polisi hajakutwa na hatia yoyote licha ya kupewa siku 14 kurudi kwa ajili ya mahojiano mengine akieleza kuwa hali hiyo haiwakatishi tamaa kuendelea kupigania maslahi ya nchi.
Amesema licha ya kutokuwa na chama kama alivyotangaza mwaka 2015, lakini bado anaendelea na siasa akieleza kuwa mkakati wao ni kuendelea kupigania kile wanachokiamini.
“Hii ni mara yangu ya 22 nakamatwa na Polisi lakini nakuwa sina hatia, leo nimehojiwa tena nikaambiwa nimefanya kusanyiko lisilo na kibali lakini sisi tulialikwa na chama kilichokuwa na mkutano kule Kandete wakadai kuna muziki ulipigwa wa chama cha kisiasa.
“Hatukati tamaa licha ya wao kutaka kutupunguza kasi, tunajiandaa na maandamano Novemba 9 tutakayozindua rasmi jijini Mbeya tukihitaji katiba mpya na kupinga uwekezaji bandari,” amesema Dk Slaa.
Kwa upande wake Mwabukusi amesema wametekeleza wito wa Polisi baada ya kuwapo kwenye mkutano wa NCCR Mageuzi na kwamba bado msimamo wao ni uleule kuhakikisha wananchi wanapata haki zao na kupinga kile kinachowaminya.
“Tunataka katiba mpya, haki ya umiliki wa ardhi kwa wazawa na uwekezaji mbovu wa bandari, yakitekelezwa haya sisi tutatulia, niwaombe wananchi kutokata tamaa na lazima kieleweke,” amesema mwanasheria huyo wa kujitegemea.
Pia wamesema Novemba 9 wanatarajia kufanya uzinduzi wa maandamano ya kudai katiba mpya, haki ya umiliki wa ardhi kwa wazawa na kupinga makubaliano ya uwekezaji wa bandari.
Hii ni mara ya pili kwa wanaharakati hao kukamatwa ndani ya mwaka huu, ambapo Agosti 12 walikamatwa na Polisi kwa nyakati tofauti na kufikishwa Mbeya, kabla ya kuachiliwa baada ya kukaa mahabusu kwa wiki moja.
Kwa upande mwingine, CCM Mkoa wa Mbeya imesema haitakubali kuona mkoa huo unakuwa kitovu cha mipango kupinga juhudi za serikali kuleta kimaendeleo.
Hayo yameelezwa leo na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mbeya, Charles Mwakipesile akisema mkoa huo umekuwa na baraka nyingi kwa kupewa miradi mingi ya maendeleo ikiwamo mradi wa njia nne na ule wa maji Mto Kiwira.
“Kama kuna mtu anaona wivu atafute sehemu nyingine akafanyie maandamano, Rais Samia Suluhu Hassan ameruhusu uhuru lakini wapo baadhi wanautumia vibaya, hivyo CCM Mbeya haitakubali kupoteza sifa yake.