Dk Slaa, Mwabukusi na Mdude waitwa Polisi kuhojiwa

Muktasari:
- Mwanaharakati na wakili wa kujitegemea, Boniface Mwabukusi, Dk Wilbroad Slaa na Mdude Nyangali wameitwa Polisi kwa ajili kuhojiwa kwa kile kinachodaiwa kutaka kuendesha mkutano wa hadhara bila kibali.
Mbeya. Mwanaharakati na Mwanasheria wa kujitegemea, Boniface Mwabukusi na Dk Wilbroad Slaa wamelazimika kuhairisha mkutano wao na waandishi wa habari uliopangwa kufanyika FQ mtaa wa Forest mkoani Mbeya baada ya kupokea wito wa Jeshi la Polisi.
Mkutano huo ulipangwa kufanyika leo Jumatatu Oktoba 9, 2023.
Mwananchi Digital ilifika eneo hilo na kushuhudia Dk Slaa, Mwabukusi wakiwa wamejifungia ndani ya hoteli hiyo huku Jeshi la Polisi likiimarisha ulinzi katika eneo hilo.
Akizungumzia hali hiyo, wakili Philip Mwakilima anayewatetea wanaharakati hao, amesema kikao cha waandishi wa habari pamoja na wateja wake hakitofanyika tena baada ya madai ya kupokea wito kutoka kwa R.C.O.
"Kwa maana hiyo kikao chetu na waandishi wa habari hakitakuwapo tena kwa sababu wateja wameitwa kwa mahojiano, Dk Slaa tayari amefika hapa polisi na Mwabukusi na Mdude wameshapokea wito kwa mahojiano zaidi kufanya mkutano bila kibali " amesema Mwakilima.
Wakili huyo amesema kuwa baada ya mahojiano hayo wataelezea msimamo rasmi na mipango yao kutokana na ratiba walizokuwa nazo akiwaomba wananchi kuwa watulivu.
Ikumbukwe watatu hao walilazimika kuhairisha mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyika jana Oktoba 8, mwaka katika eneo la Busokelo, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya baada ya polisi kudaiwa kuuzuia.
Mwabukusi ambaye miezi michache iliyopita alifungua kesi ya kupinga mkataba wa uwekezaji wa bandari katika Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambayo baadaye ilitupiliwa mbali na kubariki mkataba huo.