Dk Mpango aahidi ushirikiano na Mahakama ya Afrika

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango akiwa na Majaji wa mahakama ya Afrika ya Haki za Binaadamu na Watu leo Jumatatu, Februari 20, 2023 wakati wa uzinduzi wa mwaka wa shughuli za mahakama hiyo. Picha Mussa Juma
Muktasari:
- Mahakama hiyo ilianzishwa mwaka 2004 na Umoja wa Afrika (AU) kutokana na maazimio ya mwaka 1998, ikiwa na makao makuu yake jijini Arusha, hata hivyo imekuwa na changamoto ya baadhi ya nchi wanachama wa kutotekeleza hukumu zake.
Arusha. Wakati Tanzania ikiwa imejiondoa rasmi kwenye kipengele cha Mahakama ya ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) kinachoruhusu watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali kuishtaki Serikali, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema Serikali itaeandelea kushirikiana nayo kutetea haki za binaadamu.
Tanzania iliandika kusudio la kujitoa Novemba 21, 2020, katika ibara ya 34 (6) ya mahakama ya Afrika ya Haki za binadamu na watu, ambayo inaruhusu watu binafsi na asasi zisizo za kiserikali kuishtaki Serikali.
Akifungua mkutano wa 27 wa Chama cha Mawakili wa Afrika ya Mashariki (EALS) jijini Arusha Novemba 26, 2022 Rais Samia, alisema Tanzania imejiondoa kwa muda katika mahakama hiyo kutokana na changamoto ilizozibaini.
Hata hivyo, akizungumza leo Februari 20 katika hotuba ya ufunguzi wa mwaka wa mahakama hiyo, Dk Mpango amesema, Serikali ya Tanzania inatambua umuhimu wa mahakama hiyo na itaendelea kufanya nayo kazi ikiwepo kuhakikisha majaji na watumishi wengine wanaishi katika mazingira mazuri na salama jijini Arusha.
"Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza ajenda ya AU ya mwaka 2063 katika kuimarisha masuala ya haki za binaadamu na watu, demokrasia na uhuru wa kujieleza," amesema.
Amesema kumekuwepo na changamoto kadhaa katika utekelezwaji wa hukumu za mahakama hiyo na akashauri mahakama kuboresha mahusiano na mahakama za ndani ya nchi, ili kuondoa dhana kuwa mahakama hiyo kuingilia uhuru wa mahakama za ndani.
Awali Rais wa mahakama hiyo, Jaji Imani Aboud amesema mahakama hiyo, tangu imeanzisha miaka 16 iliyopita imeweza kutoa hukumu katika mashauri zaidi ya 200 ambayo yalifikishwa kutoka nchi mbali mbali.
Hata hivyo, alisema changamoto iliyopo ni baadhi ya nchi kutotekeleza baadhi ya hukumu ambazo zimekuwa zikitolewa na mahakama hiyo.
"Kwa mujibu wa mkataba wa AU ibara ya 30 nchi wanachama zinapaswa kuheshimu maamuzi ya mahakama hiyo na kueleza tayari kuna nchi zimeanza kuzitumia baadhi ya hukumu za mahakama hiyo katika kuboresha sheria zake," amesema.
Amesema kauli mbiu ya mwaka wa mahakama hiyo mwaka huu ni ‘Kuunganisha mifumo wa sheria za haki za binaadamu za kikanda na kimataifa katika mifumo ya kitaifa’ ikiwa na lengo ni kuimarisha masuala ya haki za binaadamu.
Alisema mahakama hiyo, itarajia kuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo wa mawakili, majaji na mahakimu juu ya masuala ya haki za binaadamu na watu.
Kwa upande wake Rais wa Mahakama ya Afrika ya Mashariki (EACJ), Jaji Nestor Kayobera amesema mahakama ya Afrika ya Mashariki itaendelea kufanyakazi kwa kushirikiana na mahakama hiyo ya Afrika ili kuimarisha haki za binaadamu.
Naye na Rais wa Bunge la Afrika, Fortune Charumbira amesema wabunge wa bunge hilo wana imani kubwa na mahakama hiyo na wataendelea kutoa ushirikiano ikiwepo kupitisha sheria kusaidsia upatikanaji wa haki, maendeleo na umoja.