Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dk Biteko: Watumishi wa umma furukuteni ili uwepo wenu utambulike

Muktasari:

  • Amesema watumishi wengi hawataki kujishughulisha kwenye kazi zao ili watambulike badala yake wanasimama kwa kusubiri waelekezwe na viongozi wao, na bila kufanya hivyo huonekana kama hawako kazini.

Dodoma. Watumishi wa umma wametakiwa kusimama katika majukumu ili waweze kuonyesha umuhimu wao na jamii iwatambue, badala ya kusubiri wapewe sifa kupitia makaratasi.

Wito huo umetolewa leo Jumatano Mei 7,2025 na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko wakati akizungumza kwenye mkutano mkuu wa Chama Cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii (Codepata) unaoendelea jijini Dodoma.

Naibu Waziri Mkuu amesema watumishi wengi hawatekelezi majukumu yao kwa kujiamini badala yake wanasubiri kila jambo kuelekezwa na wakuu wao au wasimamizi wao katika idara wanazofanyia kazi, jambo ambalo ni aibu.

Dk Biteko amewaambia maofisa maendeleo ‘kufurukuta’ kila hatua wanayofanyia kazi na ndipo wataonekana kuliko kukaa kimya kila wakati wakisubiri kupangiwa majukumu yao,  ambayo wangeweza kuyafanya bila kusimamiwa.

“Kudai kwamba mpo lakini hamfurukuti haitawasaidia badala yake mtaendelea kupiga kelele kila wakati msifanikiwe, lazima mfurukute na mjitume hasa katika utumishi, tatizo tunapenda kufanya kazi kwa kusimamiwa,” amesema Dk Biteko.

Ametaka kila mtumishi kuwa na wivu na taaluma yake ili asimame kama mtumishi aliyewekwa kwa ajili ya kulisaidia Taifa, akisema ni dhambi kwa kuiacha taaluma nje na kufanya mambo yaliyo nje ya walichojifunza.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri amewapongeza maofisa maendeleo hao kwa kujitahidi kuwasajili wafanyabiashara ndogondogo 79,946 hadi kufikia Aprili 2025 pamoja na kuratibu masuala ya mikopo  ya asilimia 10, lakini akaomba wasikubali kuharibu taswira yao kutokana na mikopo hiyo.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Doroth Gwajima amesema mkutano huo uliojumuisha  maafisa kutoka nchi nzima ni wa 17 tangu kuanza kwa chama hicho 2001.

Dk Doroth amesema maofisa maendeleo ya jamii wanafanya kazi kubwa lakini kwenye mazingira magumu kutokana na upungufu wa vifaa ikiwemo ukosefu wa vyombo vya usafiri.

Dk Doroth amemuomba Dk Biteko kupeleka kilio cha wizara kuhusu upungufu wa kada hiyo muhimu kwenye soko la ajira, akisema ndiyo injini ya maendeleo mahali popote lakini wamekuwa hawapewi thamani yao.

Awali rais wa Codepata, Victor Kabuje aliomba Serikali kuwasaidia kwa kuendelea kuajiri wataalamu kuanzia ngazi ya vijiji na mitaa ili wawafikie watu wengi zaidi wanaohitaji huduma yao.

Kubeje ameomba Serikali iwasaidie upatikanaji wa vifaa na vitendea kazi na kuongezewa bajeti katika idara hiyo, kwani inafanya kazi kama sekta mtambuka kwa ajili ya kuwawezesha watu kupata huduma na mahitaji yao.