Dk Biteko: Watanzania wanataka mafuta yapatikane kirahisi

Muktasari:
- Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 27, 2023, alipotembelea gati la kupokelea mafuta (KOJ), wilayani Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo pia panajengwa mita mpya za kupimia uingiaji wa mafuta (Flow meter), ambazo zinasimamiwa na Mamlaka ya Bandari (TPA).
Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameitaka Kampuni ya kuhifadhi mafuta nchini (Tiper), kurahisisha upatikanaji wa mafuta nchini ili shughuli za kiuchumi zisisimame.
Biteko ameyasema hayo leo Oktoba 27, 2023, alipotembelea gati la kupokelea mafuta (KOJ), wilayani Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo pia panajengwa mita mpya za kupimia uingiaji wa mafuta (Flow meter), ambazo zinasimamiwa na Mamlaka ya Bandari (TPA).
Wakati sekta ndogo ya mafuta ikiwa imegubikwa kile kinachoita “siasa nyingi,” Dk Biteko amesema Watanzania nahitaji bidhaa hiyo ipatikane kwa kirahisi na bei wanayoimudu.
Mwezi Julai mwaka huu, wananchi katika mikoa kadhaa ikiwemo Arush, Rukwa, Njombe na Tabora walikuwa wanalalamika kuadimika kwa bidhaa hiyo kiasi cha kutumia muda mwingi kujipanga foleni ili kununua, huku baadhi ya vituo vinavyouza bidhaa hiyo vikisema Imeisha.
Jambo hilo lilisababisha Serikali kuingilia kati ambapo, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), ilivifungia vituo kadhaa vya mafuta kwa miezi sita, baada ya kubainika vilificha bidhaa hiyo.
“Wananchi wapate mafuta kwa urahisi lakini pia kwa bei rafiki sio kunakuwa na ucheleweshwaji wa kupata mafuta kwa sababu zilizo ndani ya uwezo wetu," amesema Dk Biteko.
Aidha, Dk Biteko ameridhishwa na utaratibu wa upokeaji na upakuaji mafuta kuwa unaendelea vizuri huku akisisitiza changamoto chache zilizopo zinaendelea kushugulikiwa na TPA.
Akizungumzia kuhusu Tiper, Naibu Waziri Mkuu amesema imeanza kupokea mafuta na wameonyesha uwezo mkubwa wa kusambaza bidhaa hiyo nchini, huku akibainisha kuwa ujenzi wa matenki mapya ya kuhifadhia mafuta katika eneo hilo, utaongeza ufanisi, na kupunguza gharama za kusubiri ambazo huchangia kupanda kwa bei ya nishati hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tiper, Mohamed Mohamed ameahidi kuwa kampuni yake itaendelea kuboresha miundombinu ya kupokea na kusambaza mafuta ili kuongeza ufanisi zaidi.
Katika ziara hiyo, Dk Biteko aliambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba, Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Halima Bulembo, Meneja wa Bandari Dar es Salaam, Mrisho Mrisho, maofisa wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), na Wataalam kutoka Wizara ya Nishati.