Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yaja na mfumo wa kudhibiti matumizi ya mafuta

Muktasari:

  • Katika kudhibiti mianya ya upotevu wa raslimali za umma, Serikali imetengeneza Mfumo wa Kieletroni wa Kuratibu Ununuzi wa Mafuta Serikalini, ujulikanao kama (GIMIS), ambao utatunza taarifa za matumizi ya mafuta kwa kila taasisi.

Dodoma. Serikali imesema matumizi sahihi na salama ya mifumo ya kieletroniki Serikalini, yatakuwa ni suluhisho la kudumu la kuziba mianya ya upotevu wa rasilimali za umma ikiwemo mapato yatokanayo na vyanzo mbalimbali nchini.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba, leo Jumapili Oktoba 22, 2023 wakati akipokea na kuzindua Mfumo wa Kieletroni wa Kuratibu Ununuzi wa Mafuta Serikalini, ujulikanao kama (GIMIS), kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene.

Amesema matumizi ya mifumo imara ya kielektroniki yanasaidia kuondoa mianya ya upotevu wa rasilimali za Serikali na kudhibiti watumishi wasio waadilifu, kwakuwa malipo yote ya Serikali yatalipwa kupitia njia sahihi na salama katika taasisi husika.

“Tukifanya kazi kupitia mifumo ya kielektroniki tunapunguza makosa mengi ya kibinadamu, hivyo matumizi sahihi ya mifumo hii yatatuwezesha kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wetu ikiwa ni pamoja na eneo la ukusanyaji wa mapato mbalimbali ya serikali,”amesema.

Dk Mwigulu amesema mfumo wa GIMIS unatumiwa na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA), ambapo kwa sasa  majukumu yote ya Wakala yanatekelezwa kupitia  mfumo huo ambao umesaida kurahisisha na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aidha, Dk Mwigulu aliielekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kuhakikisha inaunganisha mfumo wa Manunuzi Kielektroni (NeST) na mfumo wa GIMIS kwa kuwa, mfumo huo unatumiwa na wizara, mashirika ya umma, wakala, Ofisi za mikoa na halmashauri za wilaya nchini katika kupata huduma za GPSA.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema lengo la mfumo huo ni kurahisisha utendaji kazi wa Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).

Amesema kurahisisha huku ni katika uuzaji wa mafuta Serikalini ili kuweka uwazi na kutunza kumbukumbu za matumizi ya mafuta katika kila taasisi ya umma.

Amesema hadi sasa zaidi ya taasisi nunuzi 7070 zinatumia mfumo huo ambapo, taarifa za matumizi ya mafuta kwa kila taasisi zinatunzwa katika mfumo huo.

Amesema mfumo huo utasaidia katika uandaaji na usimamizi wa mipango ya bajeti ya ofisi pamoja na udhibiti wa matumizi sahihi ya mafuta kwa taasisi za umma.

“Lengo la mfumo huu ni kuhakikisha matumizi sahihi ya mafuta kwa taasisi za umma na kuokoa fedha zilizokuwa zikipotea kutokana na kutokuwepo kwa kumbukumbu sahihi za matumizi ya mafuta”, amesema.

Aliongeza kupitia mfumo huo, Serikali inaweza kufahamu kiasi cha mafuta yaliyotumika na yaliyobaki, magari yaliyopatiwa mafuta, muda, mahali na tarehe.

Simbachawene amesema kwa kufanya hivyo kutawezesha taasisi husika kuweza kudhibiti matumizi ya mafuta ikiwa ni pamoja na kuondoa udanganyifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu.

Aidha, katika utekelezaji wa agizo la Rais Dk Samia Suluhu Hassan la kuunganisha mifumo ya TEHAMA Serikalini, Simbachawene alisema mfumo huo umeunganishwa kwenye mfumo mkuu wa Serikali wa kuwezesha mifumo kubadilishana taarifa (GovESB).