Serikali yawatoa wananchi hofu upatikanaji mafuta

Muktasari:
- Serikali imeendelea kuwatoa hofu wananchi juu ya upatikanaji wa bidhaa ya mafuta nchini huku akiesema Serikali kupitia Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) inaendelea kuingiza mafuta kwa mujibu wa taratibu na mikataba iliyowekwa.
Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema ripoti ya hali ya utoshelevu wa mafuta nchini kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, unaridhisha huku akisema Serikali kupitia Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), inaendelea kuingiza mafuta kwa mujibu wa taratibu na mikataba iliyowekwa.Dk Biteko amesema hayo, Oktoba 19, 2023 jijini Dodoma wakati Wizara ya Nishati ilipokuwa ikitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu hali ya uagizaji wa mafuta nchini pamoja na upatikanaji wa fedha za kigeni"Ujazo wa mafuta yaliyokuwepo nchini kwa ajili ya matumizi ya ndani mwishoni mwa mwezi Septemba, 2023 yalikuwa ni jumla ya lita 248,815,232 ikiwa ni lita 136, 532,747 za dizeli, lita 93,305, 815 za petroli na lita 18,978, 670 za mafuta ya ndege na taa" amesema Dk Biteko.Amesema mafuta yaliyokuwepo katika maghala na yale yaliyokuwa katika hatua za upakuaji, wastani wake kila wakati kumekuwa na ziada ya mafuta isiyopungua siku 15 kwa dizeli na petroli wakati ambapo kwa mafuta ya ndege ziada huzidi siku 30.Kuhusu suala la upatikanaji wa fedha za kigeni nchini, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema kuwa, sababu za uhaba wa fedha za kigeni umechangiwa na athari za uviko-19.“Mdororo wa kiuchuni uliosababishwa na kufungwa kwa baadhi ya shughuli za uchumi kama vile China, na athari za Vita ya Ukraine na Urusi na hivyo kusababisha ongezeko la bei katika soko la dunia,” amesema na kuongeza;“Mabadiliko ya tabia ya nchi na ongezeko la riba nchini Marekani na hivyo kusababisha mahitaji makubwa ya fedha ya kigeni hususani Dola za Marekani.”Amesema, Tanzania imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na upungufu huo ikiwa ni kuziagiza wizara kuunda timu ya wataalamu kufanya upembuzi wa kina kuhusu changamoto hiyo na kuziagiza taasisi kufanya uchambuzi wa maeneo mengine yenye matumizi makubwa ya fedha za kigeni.Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba akitoa majumuisho kwa kamati amesema kuwa miongoni mwa hatua ambazo zimechukuliwa kwa ajili ya kuboresha hali ya upatikanaji wa mafuta ni kuanza kutumia eneo la kushushia mafuta la TIPER ili kupunguza muda wa kushusha mafuta.Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kupitia kwa Mwenyekiti wake, Daniel Sillo wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa mafuta nchini kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2023 hadi Sasa na kuwatoa hofu wananchi kuhusu kukosekana kwa bidhaa hiyo nchini.