Dk Biteko kuanza na hili Wizara ya Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko
Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema kazi iliyo mbele yake ni kuhakikisha huduma ya nishati inawafikia wananchi wote na kwamba pamoja na kazi nzuri iliyofanyika ya kuimarisha sekta ya nishati, bado kuna nafasi ya kufanya ili nishati ya uhakika ipatikane.
“Kama watu hawapati umeme, kama watu hawapati nishati wanayoihitaji, hata tukivaa suti za namna gani tunakuwa hatuna maana na tutakuwa tunasemwa kila siku, kiu yangu ni kuona tunafanya kazi kwa viwango ili huduma ya nishati iwafikie wananchi wote,” alisema Dk Biteko
Dk Biteko alisema hayo jana Jumatatu, Septemba 4, 2023 baada ya kupokewa rasmi na menejimenti na watumishi wa wizara ya nishati katika Ofisi za wizara hiyo zilizopo jijini Dodoma baada ya kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika nyadhifa hizo.
Alitumia fursa hiyo kumpongeza aliyekuwa waziri wa nishati, January Makamba (ambaye sasa ni waziri wa mambo ya nje) kwa juhudi alizofanya kuendeleza sekta na kuahidi utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati itaendelea ili kufanya nchi kuwa na nishati ya uhakika.
Pia, Dk Biteko aliongozana na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ambaye naye ameteuliwa na kuapishwa kuchukua nafasi ya Stephen Byabato aliyehamishiwa wizara ya mambo ya nje akishughulikia masuala ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa imani aliyompatia ili kuweza kuhudumia sekta ya nishati kama mbunge aliyetoka katika kundi la vijana na ameahidi uchapakazi, weledi na ufanisi katika kazi zake.
Kapinga alieleza kufarijika kwake kwa kurudi katika sekta ya nishati kwani tayari alishaanza kuwa na uzoefu nayo wakati akihudumu kama makamu mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya nishati na madini.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba aliwapongeza Dk Biteko na Judith kwa kuteuliwa kwao na kuwakaribisha viongozi hao katika wizara ya nishati na kueleza wafanyakazi watatoa ushirikiano kwa viongozi hao ili kuweza kutekeleza majukumu yao kazi kwa ufanisi mkubwa.