Dk Biteko azindua bodi ya Tanesco akiagiza mambo sita

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akiwa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), muda mfupi baada ya kuizindua bodi hiyo leo.
Muktasari:
- Miongoni mwa maelekezo hayo ni kuendeleza na kusimamia miradi ya kimkakati ya uzalishaji na usambazaji wa umeme ili kuhakikisha huduma ya umeme inaimarika na kuwafikia Watanzania wengi zaidi nchini.
Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amezindua rasmi Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), huku akitoa maelekezo sita.
Miongoni mwa maelekezo hayo ni kuendeleza na kusimamia miradi ya kimkakati ya uzalishaji na usambazaji wa umeme ili kuhakikisha huduma ya umeme inaimarika na kuwafikia Watanzania wengi zaidi nchini.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu na kuhakikisha miradi ya umeme inatekelezwa kwa ufanisi ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Maelekezo mengine ni pamoja na kusimamia miradi mipya ukiwamo wa Mto Malagalasi mkoani Kigoma, kuendeleza vyanzo mseto vya umeme (umeme jua na joto ardhi), pia kusimamia na kuimarisha mtandao wa gridi ya Taifa ili mikoa isiyounganishwa ipate huduma hiyo.
Amewaeleza wajumbe hao wa bodi ya wakurugenzi kwamba wanapotekeleza majukumu yao, wanapaswa kukumbuka kuwa Watanzania wanahitaji umeme wa uhakika zaidi kuliko mambo mengine.
“Wananchi wakipata huduma bora ya umeme, hawatakuwa na shida nyinginezo, hivyo hili lazima mliwaze kila kukicha,” amesema.
Dk Biteko ameyasema hayo leo Jumapili, Septemba 15, 2024 alipokuwa akizindua rasmi bodi hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti, Dk Rhimo Nyansaho aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Desemba 19, 2023.
Wajumbe wa bodi hiyo ni pamoja na Dk Lucy Mboma, Isaack Chanji, Boma Raballa, Grace Joachim, Profesa Hellen Bandiho, Balozi Zuhura Bundala, Profesa Ninatubu Lema na Profesa Idris Kikula, ambao wote watatumikia kwa kipindi cha miaka mitatu.
"Bodi hii ninayoizindua leo inapaswa kuongeza idadi ya wateja wanaounganishwa na umeme, pamoja na kuendelea kuboresha huduma. Mtakumbuka kuwa wakati bodi hii inateuliwa, tulikuwa tunakabiliwa na changamoto za umeme.”
"Wakati naingia hali ya umeme haikuwa ya kuridhisha, lakini sasa baada ya miezi michache ya bodi hii kufanya kazi, nafurahi kuona mabadiliko mazuri katika upatikanaji wa umeme kwa Watanzania. Matatizo madogo yaliyosalia tutayashughulikia," amesema Dk Biteko.
Tahadhari kwa bodi mpya
Pamoja na mambo mengine, Dk Biteko ametoa tahadhari kwa wajumbe wa bodi hiyo, akisisitiza ingawa wote wana uzoefu, haitoshi kama hawataendelea kujifunza ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
"Wapeni nafasi menejimenti kuonyesha utaalamu wao, lakini msikubali jambo lolote lisilofaa kupita bila kulikagua. Muwe na uwezo wa kusimamia, lakini pia wasikilizeni," amesema.
Amesema baadhi ya taasisi, wajumbe wa bodi badala ya kuisimamia menejimenti, wanageuka kuwa madalali wa zabuni, jambo ambalo si sahihi. "Menejimenti inapata usumbufu, lakini Mungu ni shahidi, tangu bodi hii ianze kazi sijawahi kusikia dalili ya mjumbe kusukuma jambo lisilofaa," amesema.
Akiigeukia menejimenti, Dk Biteko amesema; "Menejimenti, fahamuni kwamba nikiletewa pendekezo kuhusu utendaji kazi wa mtu yeyote, nitaiamini bodi zaidi yenu, hivyo nendeni mkafanye kazi kwa bidii kwani Watanzania wanahitaji umeme."
Naye Mwenyekiti wa bodi hiyo, Dk Nyansaho, amesema wajumbe wa bodi hiyo wana utaalamu tofauti kama vile sheria, diplomasia, uhandisi, usimamizi wa ugavi, masoko na utawala.
Hata hivyo amesema licha ya changamoto za nishati hiyo kupungua, amemuhakikishia Dk Biteko kuwa bodi itahakikisha upatikanaji wa umeme nchini unaboreshwa zaidi.
Akizungumzia nafasi zinazokaimiwa, Dk Nyansaho amesema kuna wafanyakazi wengi wanaokaimu nafasi za menejimenti, jambo alilosema linaweza kuathiri ufanisi wao.
Hivyo, amesema bodi imeamua kusimamia suala hilo ili wale wenye sifa waongezewe nguvu kwa kuthibitishwa rasmi katika nafasi wanazozikaimu.