Dk Biteko awataka wahitimu Mweka kuichukia rushwa

Askari wa Jeshi Usu, kutoka chuo cha Usimamizi wa wanyamapori, Mweka wakiwa kwenye gwaride wakati wa kilele cha maadhimisho ya Miaka 60 na mahafali ya 59 ya chuo hicho. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amewataka wahitimu wa chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Mweka kwenda kuyaishi maadili waliyoyapata vyuoni na kuchukia rushwa.
Moshi. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewataka wahitimu wa taaluma za uhifadhi na masuala ya utalii, kulinda rasilimali za Taifa na kuepuka kujitajirisha katikati ya umaskini wa Watanzania.
Amewataka watakaoajiriwa kwenye taasisi za umma na maeneo mengine kwenda kuyaishi maadili waliyoyapata vyuoni na kuchukia rushwa.
Wito huo ameutoa leo Novemba 25, 2023 alipokuwa akizungumza na wahitimu wa kozi za uhifadhi wa wanyamapori na utalii katika kilele cha maadhimisho ya miaka 60 na mahafali ya 59 ya chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Mweka mkoani Kilimanjaro.
"Tutendeeni wema kwa jambo moja, kayaishini maisha mliyofundishwa, nendeni mkachukie rushwa wale mtakaoajiriwa, msione fahari kujitajirisha katikati ya umaskini wa Watanzania.
"Wale mtakaopewa kazi ya kulinda maliasili nendeni mkazilinde kwa wivu mkubwa, kama mtalaumiwa kwa kulinda maliasili zetu, Mungu yupo atawalipa heri zake na mkawe walinzi wa taaluma zenu," amesisitiza Dk Biteko.
Amewataka watakaoajiriwa kwenda kuwaheshimu watakaowakuta kazini na kuacha ujuaji mwingi na kuamini Taifa linawategemea.
"Kajifunzeni kwa wale mtakaowakuta kazini, kitendo cha kuamini kuwa wewe unajua kuliko wengine kwa kweli ni kutokuelimika," amesema.
Wakati Dk Biteko akiwa chuoni hapo alishiriki kupanda mti wa kumbukukumbu na kuzindua mnara wa miaka 60 ya chuo hicho tangu kuanzishwa mwaka 1963.
Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho, Profesa Jaffary Kideghesho amesema wameendelea kuwa na ushirikiano na Serikali na mataifa mengine ambapo tangu kuanzishwa kwake kimetoa wahitimu 11,000 kutoka mataifa mbalimbali duniani.
"Mafunzo ya kwanza kwa ngazi ya Astashahada na Stashahada yalianza June 24, mwaka 1963 kwa wanafunzi 25 kutoka nchi tano za Afrika, Tanzania, Kenya, Uganda, Malawi na Cameroon na mpaka sasa chuo hiki kimetoa jumla ya wahitimu 11,000 kutoka mataifa mbalimbali,"amesema.
Ameongeza kuwa chuo hicho kimetoa wataalam mbalimbali wanaochangia kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya uhifadhi pamoja wanyamapori nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amekipongeza chuo hicho kwa ushirikiano mkubwa walionao katika jamii, na kuhakikisha maendeleo yanapatikana katika eneo linalokizunguka.