Makonda aitaka Takukuru kuchunguza rushwa Muleba

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda akizungumza na wananchi wa Muleba aliposimama kuwasilimia akielekea Chato mkoani Geita.
Muktasari:
- Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda amekemea vitendo vya rushwa vinavyodaiwa kutwandwa wilayani Muleba Mkoa wa Kagera, akiwaahidi wananchi kuzungumza na Mkurugenzi mkuu wa Takukuru kutatua changamoto hiyo.
Kagera. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Paul Makonda amesema atauagiza uongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kutuma timu ya wataalamu wilayani Muleba mkoani hapa, kufuatilia vitendo vya rushwa vinavyolalamikiwa.
Amesema katika wilaya hiyo kuna harufu ya vitendo vya rushwa katika vitalu, ofisi za utumishi wa umma, polisi na maeneo mengine, lakini amewahakikishia wananchi kuwa atashughulikia kero hiyo.
Makonda ameeleza hayo leo Ijumaa Novemba 10, 2023 akizungumza na wananchi wa Muleba aliposimama kuwasilimia akiwa njiani kuelekea wilayani Chato mkoani Geita.
Kiongozi huyo huyo yupo katika ziara ya kuimarisha chama katika mikoa ya kanda ya ziwa.
"Nitaongea na mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, kuhakikisha kwamba rushwa sio sehemu ya wilaya ya Muleba," amesema Makonda.
Huku mvua ikinyesha kubwa Makonda amesema kwamba kabla ya kumaliza mkutano wake Chato atazungumza na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amueleza mpango wa maji kuhusu upatikanaji wa huduma hiyo wilayani Muleba.
Pia amewaagiza Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) wilayani humo kuhakikisha wanajenga na kuboresha barabara katika halmashauri, akisema kwa leo wana bahati mvua inanyesha.
"Kwa upande wa Tarura mna bahati na mvua leo, isingekuwa hivyo ningekula sahani moja nanyi, tunataka barabara zenye ubora," amesema Makonda huku akishangiliwa na wananchi waliojitokeza kumsalimia licha ya mvua kubwa kunyesha.
Katika hatua nyingine Makonda aliyewahi kuwa katibu wa chipukizi na hamasa wa chama hicho, amesema huu ndio wakati wa kuijenga CCM ili iwe mtetezi wa wananchi na maslahi ya wanyonge
Awali akimkaribisha Makonda katika eneo hilo Mbunge wa Muleba Kusini, Oscar Kikoyo amesema ndani ya miaka mitatu Serikali imefanya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na miundombinu.