Prime
Dk Biteko atoa maelekezo utendaji wa Rea

Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameiagiza menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), kutumia muda mwingi kutekeleza kazi vijijini na mchache ofisini.
Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameiagiza menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), kutumia muda mwingi kutekeleza kazi vijijini na mchache ofisini.
Dk Biteko alisema hayo jijini hapa jana, alipofanya mazungumzo na menejimenti ya Rea katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati.
Alisema lengo ni kutaka waendelee kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.
“Najua mnafanya kazi kubwa ya kuandaa na kuratibu miradi mnayoitekeleza, lakini nawashauri nendeni vijijini na tumieni muda mwingi zaidi wa kazi vijijini ambako ndiko miradi yenu inatekelezwa ili muweze kuisimamia vizuri na kuhakikisha inatekelezwa kwa ufanisi,” alisema Waziri Biteko.
Hata hivyo, aliipongeza Rea kwa kazi nzuri inayofanya ya kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma ya nishati bora sawa na walioko mijini.
Aliitaka iendelee kuchapa kazi ili azma ya Serikali ya kuhakikisha kila mwananchi kijijini anatumia nishati bora ya umeme ifikiwe.
Awali, akiwasilisha taarifa za miradi inayotekelezwa kwa waziri huyo, Mkurugenzi Mkuu wa Rea, Hassan Saidy alisema mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuongeza hali ya upatikanaji umeme vijijini kutoka asilimia mbili wakati wakala huo unaanzishwa mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 69 mwaka 2020.
Saidy alisema mafanikio mengine ni kuwezesha upatikanaji wa huduma ya umeme katika makao makuu ya wilaya 26 zilizokuwa hazijafikiwa pamoja na kuanzisha mpango wa kupeleka umeme katika vijiji 12,318 vya Tanzania Bara.
“Hadi Agosti 31, mwaka huu, jumla ya vijiji 10,987 sawa na asilimia 89 ya vijiji vyote vimefikiwa na umeme na vilivyobaki vitakamilika kabla ya Juni 2024,” alisema Saidy.
Pia, alitaja mafanikio mengine kuwa ni kuviunganishia umeme vijiji na vitongoji 4,234 kwa kipindi cha miaka miwili kupitia miradi mbalimbali na kusaini mikataba ya miradi sita kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini ndani ya kipindi cha miezi 12.
“Pia, tumewezesha ujenzi wa miradi midogo 121, hivyo kuunganisha wateja 178,401 katika maeneo mbalimbali yaliyo mbali na gridi ya Taifa,” alisema Saidy.
Mengine ni kuanzisha mpango wa kuwezesha ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta vijijini, kuongezeka kwa uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha vifaa vya ujenzi wa miradi kutoka sita mwaka 2007 hadi 56 mwaka 2021.
Alisema viwanda hivyo huzalisha nguzo, nyaya, mita, mashineumba na viunganishi.
Saidy alimhakikishia Dk Biteko kuwa Rea itaendelea kujituma pamoja na kuleta ubunifu katika kuharakisha upatikanaji wa nishati bora maeneo ya vijijini.