Dira ya maendeleo ya 2025 imefikiwa kwa asilimia 65

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akizungumza na Watanzania wanaoishi Jamhuri ya Korea (Diaspora) kwenye Mkutano uliofanyika katika Hoteli ya JW Marriott Jijini Seoul tarehe 05 Juni, 2024
Muktasari:
- Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utekelezaji wa dira ya maendeleo ya mwaka 2025 umefanikiwa kwa kiasi kikubwa licha ya kwamba siyo kwa ukamilifu wake.
Seoul. Wakati serikali ikiendelea na mchakato wa kuandaa dira mpya ya maendeleo ya mwaka 2050, Rais Samia Suluhu Hassan amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 umefikia asilimia 65.
Amesema utekelezaji wa dira hiyo ungeweza kufikia asilimia 80 lakini haikuwezekana kwa sababu hawakuweza kuipima sekta isiyo rasmi licha ya kuwa na mchango.
Rais Samia alibainisha hayo jana Juni 5, 2024 jijini Seoul, Korea Kusini wakati akizungumza na Watanzania waishio nchini humo na kuwaeleza mambo kadhaa yanayoendelea nchini Tanzania na yale yanayofanywa na Serikali.
Amesema Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na utekelezaji wa dira ya maendeleo ya mwaka 2025 umefanikiwa kwa kiasi kikubwa licha ya kwamba siyo kwa ukamilifu wake.
"Utekelezaji wa dira iliyopita uko asilimia 65, tungeweza kufikia asilimia 80 lakini sekta isiyo rasmi hatukuweza kuipima. Kwa hiyo, tunajihesabu tumefanya vizuri kwenye dira iliyopita," alisema Rais Samia.
Rais Samia alibainisha kuwa Serikali imefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei hasa za vyakula ambapo sasa uko asilimia tatu na malengo yao ni kuwa usizidi asilimia tano, kiwango ambacho hakijafikiwa.
Alisema kuwa msimu wa mavuno ya chakula ndiyo kuna kelele za kupanda kwa bei za vyakula, lakini Serikali imechukua hatua kuhakikisha kwamba mfumuko wa bei haupandi kwa kiwango cha kuwaathiri wananchi.
"Uchumi wetu unakua kwa asilimia 5.2 kwa sasa, tuna tumaini huko mbele tutafika kwenye kiwango cha awali cha asilimia saba. Kwa ujumla tunaendelea vizuri," amesema Rais Samia akiwaeleza wanadiaspora hayo.
Kuhusu ununuzi wa mazao, Rais Samia amesema msimu uliopita Serikali ilinunua tani 380,000 za chakula huku lengo likiwa ni kufikisha tani 500,000 kwenye maghala ya Serikali. Alibainisha kwamba tayari Serikali imepata dili la kuuza chakula katika nchi za Zimbabwe na Zambia.
Rais Samia amewahakikishia diaspora kwamba Serikali iko tayari kufanya kazi na sekta binafsi, hivyo amewataka Watanzania hao waishio Korea kukumbuka nyumbani na kufanya uwekezaji wa kutosha kwa ajili yao na ndugu zao.
"Mwaka 2023, sekta ya ujenzi ilipokea Sh200 bilioni kutoka kwa diaspora, wengi wanajitahidi kuwekeza kwenye nyumba. Mjitahidi kuongeza uwekezaji wenu nyumbani," Rais Samia aliwaambia diaspora.
Alisisitiza kwamba sera mpya ya mambo ya nje imekamilika na diaspora wametambuliwa kwa sura mbili na haki zao zikibainishwa. Alisema kwenye Bunge hili, Serikali itapeleka bungeni miswada miwili ya marekebisho ya sheria ili iendane na haki za diaspora, sheria hizo ni Sheria ya Ardhi na Sheria ya Uhamiaji.
Akizungumzia uhusiano wa Tanzania na Korea, Rais Samia alisema umeimarika zaidi na sasa inanufaika na fungu ambalo inapata kutoka Korea Kusini tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
"Huko nyuma, shea ya Tanzania kutoka Korea ilikuwa Dola za Marekani 1 bilioni, lakini sasa tumepata Dola 2.5 bilioni. Hii ni hatua kubwa," alisema Rais Samia huku akishangiliwa na Watanzania waliohudhuria mkutano huo.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba alisema Korea Kusini imetenga Dola 10 bilioni (Sh26.2 trilioni) kwa ajili ya misaada duniani, kati ya hizo, tayari Tanzania imepokea Dola 2.5 bilioni (Sh6.7 trilioni)," alisema.
Alifafanua, "heshima ya nchi hujengwa na kiongozi wa nchi kwa mafanikio yake, haiba yake na maneno yake. Sifa za kiongozi wa nchi ina manufaa kwa nchi nzima.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wanadiaspora waishio Korea, Ally Hamad alisema mchango wa diaspora unaonekana kuwa mdogo kutokana na kukosekana kwa mifumo rahisi ya kifedha itakayowafanya wazitume nyumbani.
"Tunaomba tuwe na mifumo mizuri na rafiki itakayotuwezesha kutuma fedha nyumbani kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo," alisema mwenyekiti huyo wakati akiwasilisha risala ya Watanzania hao kwa Rais Samia.
Hata hivyo, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Mavura alisema benki ya NMB mwishoni mwa Juni 2024 itakwenda Korea ili kushughulikia jambo hilo. Ameongeza kuwa CRDB nao wameonyesha nia ya kutaka kushiriki kwenye jambo hilo.