Samia aweka kibindoni shahada ya tano ya heshima

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitunukiwa Udaktari wa Falsafa wa Heshima (Honoris Causa) kwenye Sekta ya Anga na Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga (Korean Aerospace University) Hee Young Hurr wa kwanza kulia, Jijini Seoul, Jamhuri ya Korea leo June 3, 2024. Wa kwanza kushoto ni Amidi wa Shule Kuu Soo Chang Hwang
Muktasari:
- Rais Samia ametunukiwa shahada hiyo leo Juni 3, 2024 jijini Seoul, Korea Kusini anakoendelea na ziara yake ya siku sita ambapo ameshiriki shughuli mbalimbali ikiwemo kushuhudia utiaji saini wa mikataba kati ya Korea Kusini na Tanzania.
Seoul. Rais Samia Suluhu Hassan ametunukiwa udaktari wa heshima (PhD) na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea (KAU) kutokana na mchango wake katika sekta ya usafiri wa anga.
Rais Samia ametunukiwa shahada hiyo leo Juni 3, 2024 jijini Seoul, Korea Kusini anakoendelea na ziara yake ya siku sita ambapo ameshiriki shughuli mbalimbali ikiwemo kushuhudia utiaji saini wa mikataba kati ya Korea Kusini na Tanzania.
Hiyo inakuwa shahada ya tano ya udaktari wa heshima kwa Rais Samia kutunukiwa tangu ameingia madarakani. Kwa mara ya kwanza alitunukiwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), baadaye akatunukiwa na vyuo vingine kama Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (Suza), Chuo Kikuu cha Jawahal Nehru cha India na Chuo Kikuu cha Antaria cha Uturuki.
Heshima hiyo kwa Rais Samia imetokana na mchango wake katika sekta ya usafiri wa anga nchini kutokana na hatua alizochukua hasa wakati na baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 kama vile kuongeza safari za ndege na ndege katika Shirika la Ndege la Air Tanzania.
Akizungumza leo Jumatatu Juni 3, 2024 baada ya kupewa udaktari wa heshima, Rais Samia ameshukuru na kupokea heshima hiyo aliyotunukiwa na chuo hicho na kueleza kwamba sekta ya usafiri wa anga imekuwa na umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Amesema ilikuwa ni muhimu kulihuisha Shirika la Ndege la Air Tanzania na tangu hatua hizo zilipoanza kuchukuliwa, mapato ya ATCL yameongezeka kutoka Sh33 bilioni mwaka 2016/17 hadi kufikia Dola za Marekani 308.4 bilioni mwaka 2023.
Amesema safari za ndege za kimataifa pia zimeongezeka kutoka 26 mwaka 2016/17 hadi kufikia 33 mwaka 2021 na hivyo kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini hadi kufikia karibu watalii milioni mbili wanaotembelea Tanzania.
“Ni muhimu kutambua kwamba waendeshaji wa ndani na wasafiri wamekuwa sehemu ya sekta hii kwani takwimu zinaonyesha pia idadi ya wasafiri imeongezeka kwa asilimia 25.6 kutoka abiria milioni tatu kabla a mlipuko wa Uviko-19 hadi abiria milioni 3.8 kufikia mwaka 2023,” amesema.
Rais Samia amesema mwaka 2006, Tanzania ilikuwa na ndege moja pekee, lakini hadi sasa ina ndege 14 za abiria pamoja na ndege moja ya mizigo. Pia, amesema imeweza kupanua masafa yake kutoka mataifa manne hadi kufikia mataifa 24.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea, Hee Young Hurr amesema chuo hicho kina historia ya miaka 72 na kwamba wamekuwa na ushirikiano na Tanzania hasa kwenye udhaminj wa masomo ya shahada ya umahiri.
"Utayari wa Rais Samia kushirikiana katika sekta ya anga. Leo ni mwanzo mzuri wa ushirikiano kati ya Tanzania na Korea. Uongozi wako unavutia na tumeamua kukutunukia shahada ya udaktari katika usimamizi wa usafiri wa anga," amesema Hurr.
Akizungumzia sababu za kumtunukia Rais Samia udaktari wa heshima, mwenyekiti wa bodi ya KAU, Amidi wa Shule Kuu, Soo Chang Hwang amesema kama kiongozi mwanamke, anatoa somo kubwa kwa vizazi vijavyo.
Amesema uongozi wake katika sekta ya anga ni wa kipekee na umekuwa na manufaa makubwa ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya ndege zinazotua nchini, kuongezeka kwa idadi ya ndege za ATCL pamoja na mapato.
"Kwa niaba ya bodi ya KAU, tunakupongeza na shahada hii ni ishara ya heshima kwako kwa kile unachokifanya na tunatarajia utaendelea kuwa na ushirikiano na Chuo chetu," amesema Hwang.