Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dhahabu ya Sh1.5 bilioni ilivyonaswa ikitoroshwa

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akionyesha aina ya madini yaliyokamatwa jijini Mbeya. Picha na Saddam Sadick

Muktasari:

  • Watu hao walimuomba mmiliki wa nyumba hiyo Vitus Sanga kuishi licha ya kuwa alikuwa anaikarabati ili ahamie. Inasemekana waliingia kabla ukarabati haujakamilika wakimweleza kuwa  kazi yao ni ununuzi wa mazao.

Mbeya. Watu 10 wakikamatwa kwa utoroshaji madini jijini Mbeya, Wizara ya Madini imevitaka vyombo vya usalama kumfuatilia na kumkamata kinara wa utoroshaji wa bidhaa hiyo ambaye alishafungiwa leseni.

  

Akizungumza leo Machi 19, 2024 jijini hapa, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Machi 16, mwaka huu watu 10 walikamatwa katika Mtaa wa Ilomba wakitorosha vipande 334 vya madini ya dhahabu vyenye uzito wa kilo 9.8 na thamani ya zaidi ya Sh1.5 bilioni.

Amesema maofisa madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi walifanya kazi nzuri, kwani iwapo madini hayo yangetoroshwa Serikali ingepoteza zaidi ya Sh144 milioni kama pato.

Mavunde amevitaka vyombo hivyo kumfuatilia na kumkamata kigogo na kinara wa utoroshaji madini na kumchukulia hatua.

"Hadi sasa wapo baadhi ya watu wasio na uzalendo wanaoiibia nchi kwa masilahi yao binafsi. Naomba vyombo vya dola imarisheni ulinzi kwenye mipaka lakini mfuatilie huyu kigogo mtorosha madini akamatwe haraka sana na mfumo wake wote," ameagiza.

Mavunde amesema, "hatuwezi kuhangaishwa na mtu mmoja ambaye alishafungiwa leseni, na simamisheni leseni kwa hawa wote waliohusika na mnyororo wao wote, wasijihusishe na shughuli zozote za madini."

Amemuagiza Kamishna wa Madini kuhakikisha wanaofungiwa leseni mkoa wowote, hawaruhusiwi kuendeleza shughuli eneo lingine nchini.

Mavunde ambaye pia ni mbunge wa Dodoma Mjini, ametangaza kuongoza operesheni maalumu za waliojimilikisha maeneo ya uchimbaji bila kuyaendeleza.

Amesema maeneo hayo wapewe wenye uhitaji wakiwamo wachimbaji wadogo.

"Wapo watu wanang'ang'ania maeneo makubwa lakini hawafanyi shughuli za uchimbaji, naenda kuongoza operesheni ya kusimamisha na kufuta leseni zao na kuwapa wachimbaji wadogo wenye uhitaji, suala la kodi kwenye madini tunaenda kulifanyia kazi," amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mbarak Batenga, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, amewataka wamiliki wa nyumba kabla ya kumpangisha mteja wajue taarifa zake.

"Tunaambiwa hapa kwamba hao waliokamatwa hawakuwa wazi kwa mwenye nyumba wakieleza ni wafanyabiashara wa mazao kumbe ni watorosha madini, hivyo naomba kila mmiliki wa nyumba apate taarifa za mpangaji wake ikiwamo kazi anayofanya," amesema.

Amesema, "hata viongozi wa Serikali za mitaa hakikisheni mnakuwa na orodha ya majina ya watu wenu kwenye mitaa, kila mmoja awe anafahamika taarifa zake ili kuondoa uhalifu kama huu na kuipa hasara Serikali, usalama unaanzia ngazi za chini," amesema Batenga.

Vitus Sanga, mmiliki wa nyumba walipokutwa watuhumiwa wa utoroshaji madini, amesema watu hao waliingia nyumbani hapo Desemba, 2023 wakimweleza shughuli zao ni wafanyabiashara wa mazao.

"Mimi shughuli zangu ni duka la vifaa vya ujenzi hapa Ilomba hii nyumba ndiyo nilikuwa naandaa kwa ajili ya kuishi, lakini waliniomba sana wakaingia kabla haijaisha ukarabati, waliniambia kazi yao ni ununuzi wa mazao," amesema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema kutokana na mafunzo waliyonayo waliwakamata watuhumiwa  waliokuwa wamejificha juu ya dari.

"Hatuwezi kueleza zaidi mbinu zetu, lakini kwa mafunzo ya kiintelijensia tuliwakamata licha ya kupanda kujificha juu ya dari. Tunatoa rai kwamba, hatutamfumbia macho yeyote kwa uhalifu wowote," amesema Kuzaga.