Madalali watorosha madini kubanwa

Muktasari:
Waziri wa Madini, Dotto Biteko ameagiza Tume ya Madini nchini kuanza kufuatilia madalali wanaonunua na kusafirisha madini ya dhahabu kabla ya kulipia leseni zao.
Chunya. Waziri wa Madini, Dotto Biteko ameagiza Tume ya Madini nchini kuanza kufuatilia madalali wanaonunua na kusafirisha madini ya dhahabu kabla ya kulipia leseni zao.
Alisema hivi sasa kumeibuka wimbi la utoroshaji wa madini kwa kutumia mifumo isiyo rasmi.
Waziri Biteko alitoa agizo hilo jana Wilayani Chunya, Mkoani Mbeya baada ya kutembelea migodi ya wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Sangambi, ambako alifanya mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi, wachimbaji na madalali wa madini.
“Wapo wenzenu wachache ambao wanajifanya vinara wa kuwafuata wachimbaji na kuwashawishi kununua madini pasipo kufuata taratibu na kutorosha kwa mifumo wanayoijua wao, sasa naagiza tume ya madini kuanza kazi haraka kuwachunguza mmoja baada ya mwingine na kujua kiwango cha madini wanayonunua kwenye soko,” alisema.
Alisema kitendo kinachofanywa na watu wachache kuiibia Serikali hakivumiliki, hivyo baada ya uchunguzi wapo watakaowajibishwa kwa mujibu wa sheria endapo watapatikana na hatia.
Mbunge wa Lupa Wilaya ya Chunya, Masache Kasaka aliiomba Serikali kupunguza utitiri wa tozo za kodi ili kuwasaidia wachimbaji wa madini kulipa kwa wakati na kuwatua mzigo ambao ni kilio chao kwa muda mrefu.
Awali, Meneja wa kampuni ya Imuma, Charles Mambo alisema kukatika kwa umeme mara kwa mara kumechangia kusimama kwa uzalishaji kutokana na gharama za uendeshaji kwa kutumia mafuta ya dizeli kuwa kubwa, ambapo kwa siku wanatumia lita 30 mpaka 35.
“Mheshimiwa Waziri, tunakwama kufikia malengo ya uzalishaji wa madini kufikia kilo 3,000 mpaka 4,000 na kuongeza ajira kutoka watu 32 mpaka 80,” alisema.