Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mizani zakwamisha uuzaji pamba, wakulima hawaelewi

Wakulima wakiwa wameleta pamba yao kuuza katika ghala la kijiji cha Mwandoya lakini hawakufanikiwa kuuza kutokana na mzani wa kupimia pamba kutokuwepo. Picha na Samwel Mwanga

Muktasari:

  • Hatua hiyo imekuja baada ya malalamiko ya muda mrefu kuhusu mizani zinazodaiwa kupunja wakulima kwa makusudi, hivyo kusababisha mamlaka husika kuchukua mizani kwa ajili ya uchunguzi.

Simiyu. Wakulima wa pamba wilayani Meatu mkoani Simiyu, wamelalamikia kusitishwa kwa shughuli za ununuzi wa zao hilo hatua iliyozua sintofahamu na kilio miongoni mwa wananchi wa wilaya hiyo.

Hatua hiyo imekuja baada ya malalamiko ya muda mrefu kuhusu mizani zinazodaiwa kupunja wakulima kwa makusudi hivyo kupelekea Wakala wa Vipimo (WMA) kuchukua mizani kwa ajili ya uchunguzi.

Mwananchi digital leo Ijumaa Julai 4,2025 imezungumza na baadhi ya wakulima hao akiwemo, Mboje Madakila wa kijiji cha Mwabusalu wilayani humo ambaye amesema kuwa tangu jana hadi leo, hakuna taarifa rasmi iwapo mizani hiyo zitarejeshwa au kama italetwa mpya yenye ubora na usahihi.

"Tulifika sokoni tangu asubuhi kuuza pamba, lakini hakuna mnunuzi wote wanasema mizani zimeondolewa na hakuna maelekezo mengine hadi sasa," amesema.

Hollo Machibya ni mkulima wa Kijiji cha Lubiga amesema kuwa wakulima walio wengi wanategemea mauzo ya pamba kwa ajili ya kugharamia mahitaji ya familia na kulipa madeni, sasa wamebaki na wasiwasi na sintofahamu kubwa.

"Pamba ndilo zao linalotupatia fedha na tulio wengi tunaendesha maisha yetu kwa kutumia malipo ya fedha za pamba na wengine tulikopa mbolea na dawa kwa matarajio ya kulipa baada ya kuuza. Sasa haijulikani tunaanzia wapi," amesema.

Luhende Nyanza mkulima wa kijiji cha Mwandoya, amesema kuwa wilaya hiyo uchumi wake unategemea kilimo cha pamba, hitilafu katika mnyororo wa ununuzi si tu huathiri kipato cha mkulima mmojammoja bali mzunguko mzima wa fedha katika jamii.

“Serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania na mamlaka za upimaji wa vipimo kuhakikisha mizani sahihi na yenye ithibati inarejeshwa haraka ili kuondoa sintofahamu sokoni na kurejesha matumaini kwa wakulima,”amesema.


Kauli ya mkuu wa wilaya

Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Faudhia Ngatumbura akizungumza na Mwananchi digital amesema malalamiko ya wakulima kuibiwa kupitia mizani isiyo sahihi yameanza kufanyiwa kazi na tayari wataalamu wa ukaguzi wa mizani wamewasili wilayani humo, kwa ajili ya kufanya tathmini ya kitaalamu.

“Jana tumepokea wataalamu wa kukagua mizani ili kubaini kama kuna zilizochezewa kwa nia ya kuwaibia wakulima. Ukaguzi huu unafanywa kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi pamoja na Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), ili pale inapobidi, hatua zichukuliwe haraka dhidi ya wahusika,” amesema.

Pia, amesisitiza kuwa Serikali ya wilaya iko makini kufuatilia kila hatua katika ununuzi wa zao la pamba ili kuhakikisha wakulima wanapata haki yao na mazao yao yanauzwa kwa usawa.