Mavunde awapa salamu watorosha madini

Muktasari:
- Waziri wa Madini Antony Mavunde amekutana na Chama cha Mabroka wa Madini Tanzania (Chammata) na kuwaomba ushirikiano wao katika suala zima la kuzuia utoroshaji wa raslimali hiyo.
Dodoma. Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema kuanzia sasa mtu yeyote atakayetiwa hatiani kwa kosa la kutoroshaji madini atafutiwa leseni zake zote na kufungiwa kufanya shughuli hizo nchini Tanzania.
Mavunde ameyasema hayo Oktoba 19, 2023 wakati akizungumza na wanachama wa Chama cha Mabroka wa Madini Tanzania (Chammata).
Amesema mahakama ikitoa hukumu na kubainisha kweli mtu amehusika na kosa la utoroshaji wa madini atafuta leseni na kuwafungia (black list) kutofanya biashara ya madini tena nchini.
“Utatafuta kazi nyingine ya kufanya kama ulikuwa na kipaji cha kuimba utakwenda huko. Nakwambia kuwa hutafanya biashara ya madini tena nchini. Ndugu yangu usitake kuingia katika huu mnyororo (utoroshaji madini),” amesema.
Mavunde ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM) amesema mnyororo huo wanakwenda kufuatilia na kuukomesha hadi mwisho.
Amewataka mabroka hao kuisaidia nchi yao katika kukabiliana na utoroshaji wa madini ili kuwezesha kupatikana kwa fedha zitakazotumika kwenye shughuli za maendeleo.
Amesema inawezekana ikawa sababu kubwa ya utoroshaji wa madini ni sera, sheria, mikakati na mipango yao Serikalini, milango yake iko wazi waende wakamweleze ili aweze kushughulikia.
“Ukija kuniambia ukiondoa kodi madini yatakuja sokoni, sasa unishauri siyo unatorosha. Njoo uniambie,” amesema.
Mwenyekiti wa Chammata, Jeremia Kituyo ametaja miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na kuwa na idadi kubwa ya leseni ambazo huwagharimu fedha nyingi kuzilipia na hivyo kuomba suala hilo kuangaliwa upya.
“Changamoto nyingine baadhi ya madini kuzuiwa kuuzwa katika masoko yaliyoanzishwa na Serikali kihalali. Kuzuia madini ya Tanzanite kuuzwa katika mikoa mingine tofauti na Mererani imesababisha masoko mengine kudorora hasa soko la kimataifa la Arusha,” amesema.
Amesema madini ya Tanzanite hayana bei kubwa kuliko aina nyingine ya madini ya vito lakini yamekuwa yakililiwa na wafanyabiashara kwa sababu ni kama chumvi kwenye biashara hiyo.
Aidha, Kituyo ameahidi kuwa watatoa taarifa sahihi na wakati sahihi kabla ya utoroshaji wa madini ili kudhibiti uhalifu huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Dodoma, Ali Hamad Amour amesema wanakabiliwa na ukosefu wa umeme kwenye mgodi wa Chamkoroma mkoani Dodoma na kwamba wamefuatilia utatuzi wa changamoto hiyo kwa muda mrefu bila mafanikio.
“Mgodi ule umekuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa nafikiri mnafahamu. Kwa mazingira tunayokabiliana nayo gharama za mafuta zimekuwa ni kubwa mno na uchakavu wa mashine umekuwa ni mkubwa,”amesema.