Dereva wa gari la mizigo mbaroni akisafirisha wahamiaji haramu

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Alex Mkama.
Morogoro. Jeshi la polisi mkoa wa Morogoro limewakamata na kuwashikilia wahamiaji haramu 18 waliokuwa wakisafiri kuelekea nchini Zambia kwa kutumia gari la mizigo mali ya kampuni ya Fredy Logistics ya jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama amemtaja dereva wa gari hilo lililokuwa likisafirisha wahamiaji haramu kuwa ni Mwinyijuma Panduka (39) mkazi wa Dar es Salaam na kwamba naye anashikiliwa na polisi.
Amesema kuwa wahamiaji hao haramu ambao sita ni raia wa Somalia na nane raia wa Ethiopia walikamatwa katika maeneo mbalimbali katika barabara ya Dar es Salaam na Iringa.
Kamanda Mkama amesema kuwa polisi walifanikiwa kuwakamata baada ya kupata taarifa na kufuatilia Kwa karibu gari hilo na kufanikiwa kuwapata wahamiaji hao.
"Awali tulikamata wahamiaji haramu wawili wakiwa kwenye gari hilo lakini baadaye tukapata taarifa kuwa dereva huyo aliwashusha wahamiaji wengine 12 eneo la sangasanga njia panda ya Mzumbe na pia eneo la mindu alikwishawashusha wahamiaji haramu wengine haramu wanne ambao wote tunawashikilia kwa mahojiano na taratibu nyingine za kisheria kutoka idara ya uhamiaji," amesema kamanda Mkama.