DC Mbulu akemea jamii kujichukulia sheria mkononi

Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Kheri James (katikati) akizungumza na Mkurugenzi wa Mji wa Mbulu, Yefred Myenzi (kushoto) kwenye kikao na wakazi wa Kata ya Murray baada ya kutokea mauaji ya watu watatu. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
- Watu watatu wanaoishi Kata ya Murray Wilayani Mbulu Mkoani Manyara, wameuawa baada ya baadhi ya wananchi kujichukukia sheria mkononi na kufanya mauaji hayo.
Mbulu. Mkuu wa Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Kheri James ameitaka jamii ya eneo hilo kutojichukulia sheria mkononi, baada ya kundi la watu kuwaua wakazi watatu wa kata ya Murray.
James ameyasema hayo akizungumza na wakazi wa kata hiyo juu ya tukio la mauaji ya watu watatu yaliyosababishwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo.
Waliofariki ni Safari Awe (55) aliyepigwa na mtoto wa kaka yake Petro Baha (22) ambaye naye aliuawa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kwa kumuua baba yake mdogo.
Tukio lingine la la mauaji ni mtoto Tumaini Paul (10) mwanafunzi wa darasa la kwanza aliyeuawa na baba yake wa kufikia Petro John baada ya kutokea ugomvi wa familia. John anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za mauaji ya mtoto huyo.
Mkuu huyo wa wilaya ya Mbulu, amelaani vikali matendo ya watu kujichukulia sheria mkononi bila kufuata misingi ya utawala wa sheria, na kwama ni vema watoe taarifa kwenye vyombo vyenye dhamana ya usimamizi wa usalama na utoaji wa haki.
"Ni kosa kwa mtu au kikundi chochote kujichukulia mamlaka ya kutuhumu au kuhukumu bila kushirikisha mamlaka zinazo husika," amesema James.
Ametaja vyanzo vikuu vya matukio ya mauaji Mbulu ni migogoro ya ardhi, ukatili wa kijinsia, ulevi, wivu wa kimapenzi, ramli chonganishi na tamaa.
Hata hivyo, amewaomba viongozi wa dini, wa mila, vijiji na wananchi kwa ujumla, kuheshimu na kuhimizana umuhimu wa upendo, utii wa sheria na kuzingatia mafundisho ya dini kwenye nyumba za ibada.
"Nyenzo muhimu ya kutibu haya ni kupunguza na kumaliza visasi, chuki, tamaa na ukatili kwa miongoni mwa jamii inayoishi kwenye wilaya yetu ya Mbulu," amesema James.
Kwa upande wao, baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamebainisha kuwa wanywaji wa pombe za kienyeji ndiyo hujichukulia sheria mkononi mara baada ya kulewa.