DC aagiza Takukuru kumchunguza DED Geita Mjini

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi

Geita. Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza safari ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi, aliyekwenda nchini China.

Uchunguzi huo unalenga kubaini iwapo safari hiyo ni kwa masilahi ya halmashauri au ni ya binafsi.

Pia ameagiza Takukuru kubaini iwapo matumizi ya safari hiyo yanatokana na fedha za halmashauri au binafsi na ikibainika kuwa ni za halmashauri zirejeshwe na zielekezwe kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani ambacho nafasi ya mkurugenzi ambaye ni katibu wa kikao ilikaimiwa na Lee Kyangalla, ambaye ni Ofisa Maliasili wa halmashauri hiyo, Magembe aliitahadharisha halmashauri kutokuwa kichaka kwa mkurugenzi kutumia fedha kwa matumizi binafsi.

“Nimeuliza hapa mkurugenzi yuko wapi naambiwa halmashauri mmemtuma kwenda kujifunza. Nashukuru mwenyekiti na madiwani kama mnaweza kumtuma kwenda China kujifunza, basi elimu atakayoipata ije iendeshe kweli halmashauri, lakini isiwe kichaka kwa sababu wewe ni mkurugenzi...” alisema.

Jitihada za kumpata Zahara hazikufanikiwa baada ya simu yake kutopatikana, hata ujumbe kupitia mtandao wa WhatsApp alioandikiwa na mwandishi ulionyesha kwamba ameusoma lakini hakujibu.

Hata hivyo, Kaimu Katibu tawala mkoa wa Geita, Herman Matemu akitoa ufafanuzi wa tuhuma hizo, alisema mkurugenzi huyo alisafiri kwa kibali kilichotolewa na ofisi yake na anapaswa kuripoti kazini Oktoba 30, 2023.

"Ni safari ya kikazi kwa kuwa shirika lililompeleka linafanya kazi Mkoa wa Geita na mkurugenzi alipata mwaliko na akaomba ruhusa na akakubaliwa na kupata vibali vyote vya Utumishi," alisema.

Kuhusu gharama za safari alisema hawezi kujua, huku akisema kuna uwezekano zikawa za shirika kwa kuwa, mkurugenzi hawezi kuchukua fedha za Serikali kugharimia, kwani sio iliyoandaa safari hiyo.
 

Awashukia madiwani

Mbali ya hilo, Magembe alimtaka mwenyekiti wa baraza hilo, Constantine Moradi na madiwani kutofanya vikao vya baraza kama mkurugenzi hayupo, kwa kuwa wanaoachwa kukaimu nafasi hiyo hawana mamlaka ya kufanya uamuzi.

“Kama mkurugenzi hayupo ahirisheni, wanaokaimu hawana uwezo wa maamuzi hata akitaka kufanya kwa utaalamu wake, anaogopa na hii inatokana na ninyi madiwani mmelegea, narudia tena madiwani mmelegea mnakubali kupelekwa tu,” alisema.

Alionyesha kukerwa na madiwani wanaopewa majibu mepesi na wataalamu na kupiga makofi, akisema wanasahau wapo kwenye baraza hilo kwa niaba ya wananchi na Chama cha Mapinduzi (CCM) kilichowapeleka ili wawaletee maendeleo.

“Inaniuma, tena inaniudhi kuona wataalamu wakiwapa majibu mepesi na pengine ya ovyo kwa kujificha kwenye kichaka eti majibu ya wataalamu nanyi mnapiga makofi, si sahihi,” alisema.

Magembe alisema pamoja na Serikali kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, utekelezaji umekuwa wa kusuasua, huku kukiwa na matumizi ya ovyo kwenye miradi, hali inayotokana na madiwani kukubali kuondolewa kwenye msingi.

“Sasa hivi kamati ya fedha inaitwa mkurugenzi akijisikia. Mnakaa miezi mitatu hadi minne bila kikao cha kamati ya fedha kama mmekubali hivyo, haya madudu lazima yaendelee. Mwenyekiti na kamati yako hii ni ‘alarm’ (kengele) mtafika mahali kikao cha baraza kitakaa baada ya mwaka mmoja,” alisema na kuongeza:

“Vikao vina kanuni na taratibu zake nikutake mkurugenzi; kanuni, tararibu na uendeshwaji wa halmashauri uzingatiwe kwa sababu tunaishi kwa kanuni.”
 

Walichosema madiwani

Mwenyekiti wa halmashauri, Morandi akifunga kiko hicho alisema madiwani wamesikia na kuelewa maagizo yaliyotolewa na kuahidi kuyafanyia kazi.
Diwani wa Kata ya Nyanguku, Elias Ngole akizungumzia maagizo ya Mkuu wa Wilaya, alisema mbali ya hayo, anaomba vyombo vya maamuzi kufuatilia, akidai halmashauri inaendeshwa kama genge na madiwani wamekuwa wakisema lakini hawasikilizwi.

“Mkuu wa wilaya ametusema sana, nasi tumekubali na tunashukuru kuona hata yeye ameona halmashauri inavyoendeshwa...” alisema.

Jambo hili tunaamini sasa litapata ufumbuzi maana tumepaza sauti hatusikilizwi,” alisema.

na kuongeza:
“Mimi ni mjumbe wa kamati ya fedha lakini hatuna taarifa na safari ya mkurugenzi, tumekuja hapa tunahoji tunaambiwa amesafiri kwenda China kikazi, si madiwani wala mwenyekiti mwenye taarifa.”