Dawa za kienyeji zatajwa kupoteza usikivu

Muuguzi Ruth Ng'wananogu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita (kushoto) akimpima uwezo wa kusikia mgonjwa aliyefika hospitalini hapo akisumbuliwa na tatizo hilo juzi. Picha na Rehema Matowo.
Muktasari:
- Hospitali ya Mkoa wa Geita hupokea wagonjwa saba mpaka 10 kwa mwezi wakisumbuliwa na magonjwa ya sikio, lakini hufika wakiwa wamechelewa hadi kupoteza usikivu.
Geita. Matumizi ya tiba za kienyeji, kuchelewa kufika kituo cha afya na kujinunulia dawa famasi bila kupata ushauri wa daktari wa magonjwa yahusuyo masikio, vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia watu kupoteza usikivu.
Hayo yameelezwa na daktari bingwa wa magonjwa ya sikio, pua na koo kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, Brian Kimario katika mahojiano maalumu na Mwananchi Digital jana Machi 19, 2024.
Amesema changamoto kubwa iliyopo ni jamii kutokuwa na uelewa juu ya afya ya masikio, hivyo kuwafanya wenye matatizo hayo wachelewe kufika hospitali kupata matibabu.
Hospitali ya Mkoa wa Geita hupokea wagonjwa saba hadi 10 kwa mwezi wakisumbuliwa na magonjwa ya sikio na hufika wakiwa wamechelewa hadi kupata tatizo la usikivu.
“Jamii haina uelewa wa afya ya masikio na usikivu na hii husababisha wengi kuchelewa kwenda hospitali wanapopata tatizo. Badala yake wanaenda kununua dawa kwenye maduka ya dawa bila ushauri wa wataalamu,” amesema Dk Kimario.
“Wakati mwingine unakuta hapaswi kutumia dawa ya kutumbukiza ndani, akienda duka la dawa anapewa hiyo au wengine wanatumia dawa za kienyeji na mwisho wa siku madhara yanakuwa makubwa, yanasababisha kushindwa kusikia.”
Dk Kimario amezitaja sababu nyingine zinazochangia mtu kupata tatizo la kusikia kuwa ni kukaa kwenye kelele kubwa bila kuvaa vikinga sauti, mathalani wale wanaofanya kazi viwandani, kwenye mitambo na kumbi za starehe.
Amesema sababu nyingine ni matumizi ya baadhi ya dawa za kuweka kwenye masikio na nyingine za kunywa zisipotumiwa vizuri pamoja na baadhi ya wazee ambao umri wao huchangia wakose usikivu.
Vilevile, Dk KImario ametaja homa ya uti wa mgongo, ajali na ugonjwa wa manjano kwa watoto, kuwa ni sababu nyingine zinazochangia tatizo la usikivu.
Hali ikoje nchini?
Kwa mujibu wa Dk Kimario hakuna utafiti wa jumla uliofanywa kwa wananchi wote, bali uliofanywa kwenye makundi maalumu, wakiwemo wanaofanya kazi kwenye viwanda vya nguo ambao asilimia 58 ya wafanyakazi hao walikuwa wamepata tatizo la usikivu.
Amesema pia utafiti umefanywa kwa wagonjwa wa kisukari ambao asilimia 23 walibainika kuwa na tatizo, huku asilimia 27 ya wafanyakazi kwenye migodi mikubwa nao wakiathirika.
Akizungumzia changamoto kwa wachimbaji wadogo, Dk Kimario amesema hakuna utafiti uliofanyika kubaini ukubwa wa tatizo kwa kada hiyo, lakini akasema kutokana na uelewa mdogo wa elimu ya afya ya sikio, wengi hawafiki hospitali.
Amesema kwa mkoa wa Geita wanaofika kupata huduma wengi ni wanafunzi, ambao nao hufika wakiwa wamechelewa zaidi ya miaka mitano tangu wapate tatizo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) iliyotolewa hivi karibuni, hadi kufikia 2050 karibu watu bilioni 2.5 wanatarajiwa kuwa na kiwango fulani cha kupoteza uwezo wa kusikia na watu 700 milioni watahitaji matibabu ili waweze kusikia.
Takwimu zinaonyesha pia zaidi ya vijana bilioni moja wenye umri kati ya miaka 12-35, wako hatarini kupoteza uwezo wa kusikia kutokana na usikilizaji usio salama wa sauti za juu.
Nini kifanyike
Ili kukabiliana na changamoto ya kukosa usikivu ushauri umetolewa kwa watu wanaofanya kazi viwandani na migodini kuvaa vikinga sauti mara zote wawapo kazini ili kuepuka sauti kubwa zenye athari kwao.
Vijana pia wanashauriwa kuepuka matumizi ya ‘earphone‘na pale wanapolazimika kuzitumia iwe kwa muda mfupi .
Kwa upande wa wajawazito wanashauriwa kuwahi kliniki wanapobaini wana ujauzito, pamoja na kuhakikisha watoto wanaozaliwa wanapata chanjo zote ili kuepuka uziwi unaoweza kuchangiwa na magonjwa ya surua na polio.
Pia wazazi wanashauriwa kutowapiga watoto makofi kwenye maeneo ya sikio na kutotumia pamba za masikio kutoa uchafu kwa kuwa zinachangia kusogeza uchafu ndani na kusababisha sikio kuziba na uwezekano wa kusababisha uziwi.
Kuchelewa hospitali
Veronica William, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mgusu mjini Geita ambaye ameishi na tatizo la kutosikia vizuri kwa zaidi ya miaka mitano, amesema akiwa shule ya msingi aligundua sikio la kulia halisikii lakini hakuwahi kupelekwa hospitali kupata matibabu.
“Ilikuwa hata nikiitwa kama nimegeuka siwezi kusikia. Kuna wakati napigwa wakisema nina kiburi, lakini ukweli nakuwa sisikii hadi nilipoingia sekondari walimu ndio walinisaidia kusema nyumbani kuwa mimi nina tatizo la usikivu,” amesema Veronica.
Amesema mbali na changamoto ya kuonekana mwenye kiburi, Veronica amesema yeye kama mwanafunzi changamoto kubwa ni akiwa darasani, ni ngumu kusikia vizuri, hali inayochangia asifanye vizuri darasani.
Naye Agness Joseph mwanafunzi wa shule ya Sekondari Kasamwa anasema, “ilitokea tu nikawa sisikii vizuri nikiwa darasa la saba, nikapelekwa hospitali ikaonekana uchafu umeziba. Nilipewa vipamba vya kutoa uchafu bahati mbaya siku moja pamba ikabaki ndani na ndio hapo nikapoteza tena usikivu kabisa, sasa niko kidato cha nne na sikio langu moja halisikii,” amesema.
Akizungumzia changamoto ya mtoto wake kutosikia vizuri, Gloria Milinga, mkazi wa Mgusu amesema awali hakujua tatizo la mwanae kwa kuwa hakuwahi kusema anaumwa sikio.
Amesema sikio hilo halikuwahi kutoa usaha lakini ilitokea akiitwa haitiki na akitumwa haendi, jambo lililomfanya amwadhibu mara kwa mara, akidhani ana utovu wa nidhamu.
“Hili tatizo tumeligundua mwaka juzi baada ya mtoto kwenda sekondari…Wakati mwingine unampiga analia kuwa hajasikia, ila sikujua kama anasema kweli maana hajawahi kusema anaumwa sikio,” amesema
Mwalimu wa watoto wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Sekondari Kasamwa, Yasumta Paul amesema wanawagundua watoto wenye changamoto kutokana na wao kushindwa kuchangamana mapema na wenzao na pia kushindwa kujibu maswali darasani.
“Wenye matatizo ya usikivu na macho wanapokua darasani wanakuwa na matatizo mengi, wasiosikia vizuri tunawashauri wakae mbele na walimu wanawatambua na kuwasaidia.
Mary Venancy, Ofisa Elimu Maalumu Sekondari wa Halmashauri ya Mji wa Geita amesema kutokana na changamoto hiyo wameanza kuwabaini wenye matatizo ili wapatiwe msaada wa vifaa.
Amesema hadi sasa wanafunzi 40 wamebainika kuwa na changamoto ya kusikia inayowanyima uhuru wa kujifunza.
“Hawa ambao hawasikii Serikali inawasaiidia kupata vifaa, hivyo tukijua ukubwa wa tatizo na idadi, tunaweza kuwasaidia wakapata vifaa, wale ambao tatizo lao linatibika wanatibiwa.”
Utafiti wa WHO unaonyesha zaidi ya watu 400 milioni duniani kote wanahitaji msaada wa kuwezeshwa kusikia na kati yao ni asilimia 20 pekee wenye uwezo wa kupata vifaa hivyo kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha pamoja na rasilimali watu.