CWT yaitega Serikali madai ya walimu

Mwalimu wa shule ya msingi akiwaelekeza wanafunzi wake. Picha na Maktaba
Muktasari:
Yasema haitaki kulumbana katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu
Dar es Salaam. Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimeitaka Serikali kutekeleza madai ya ahadi za walimu kama walivyokubaliana na chama hicho.
Miongoni mwa madai hayo, ni posho ya madaraka kwa wakuu wa shule, muundo wa madaraka, walimu kutopandishwa madaraja, madeni kutolipwa kwa wakati na nyongeza ndogo ya mishahara.
Rais wa chama hicho, Gratian Mukoba alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema CWT hakijakaa kimya kuhusu kuikumbusha Serikali kutekeleza wajibu wake.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Anne Kilango Malecela alipoulizwa suala hilo, alisema kila kitu kinakwenda sawa na kwamba hawawezi kugombana na walimu.
“Kwa kifupi ndiyo hivyo, tutahakikisha kila kitu kinakwenda sawa, ila naomba umtafute Waziri Dk Shukuru Kawambwa atakupa maelezo ya kina kwa sababu analijua vizuri suala hilo,” alisema Kilango.
Hata hivyo, alipotafuwa Dk Kawambwa kupitia simu ya kiganjani iliita bila kupokelewa.
“Tukikutana Agosti 28, Serikali ije na majibu ya madai yetu, siyo kutuambia mikakati mipya wakati madai ya nyuma hayajafanyiwa kazi.
“CWT haipendi kuishinikiza Serikali kutekeleza madai ya walimu katika kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu, bali itambue makubaliano yake na chama cha walimu,” alisema Mukoba.
Alisema kikao hicho kitakuwa cha kupokea taarifa juu ya utekezaji wa madai yao.
Mukoba alisema endapo Serikali haitokuja na majibu ya kueleweka ya changamoto hizo zinazowakabili walimu, matatizo hayo yatapelekwa kwenye vikao vya chama vinavyotarajiwa kufanyika mwisho wa mwezi huu kwa maelekezo zaidi.
Akizungumzia madai ya muundo mpya wa utumishi wa walimu, Mukoba alisema:
“Muundo huu unaohusu kuwaondoa walimu waliogota kwenye madaraja ya TGSTS E ambao wanapaswa kupandishwa hadi daraja TGSTS F, lakini hadi sasa Serikali haijatekeleza kama tulivyokubaliana,” alisema Mukoba.
Alisema Serikali na CWT kwa pamoja walikubaliana mwaka 2013 kupitishwa muundo huo uliotarajiwa kuanza kutumika Julai Mosi 2014.
Mukoba alisema zaidi ya walimu 38,000 mwaka 2014/15 bado hawajapandishwa madaraja licha ya kuwa na sifa.