Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nzengo: Nguvu ya mshikamano Kanda ya Ziwa

Muktasari:

  • Nzengo si tu desturi, ni ishara ya mshikamano, uzalendo wa kijamii na moyo wa kusaidiana.

Mwanza. Katika miji na vijiji vya mikoa ya Kanda ya Ziwa, sauti ya kilio au yowe inaposikika kuashiria tatizo, ikiwamo taarifa za kifo, mfumo wa kijamii uitwao nzengo huchukua nafasi yake.

Wanajamii hukusanyika eneo husika, wanawake kwa wanaume, vijana wa kike na wa kiume, kuhakikisha wanatoa msaada kwa lililotokea.

Iwapo ni msiba, kinamama wataingia jikoni, wanaume watashughulikia uchimbaji wa kaburi. Si hivyo tu, wanajamii watatoa michango ya fedha, vyakula, huku wengine wakijitolea hata magari kwa ajili ya shughuli za msiba.

Nzengo si tu desturi, ni ishara ya mshikamano, uzalendo wa kijamii na moyo wa kusaidiana. Jamii hujitoa kumfuta machozi mfiwa kwa pamoja.

Si kanuni iliyoandikwa, lakini ina nguvu kuliko sheria yoyote ya mtaani. Kila mmoja ana nafasi yake mchango wa pesa, chakula, nguvu kazi au hata uwepo wa kimwili, vyote ni muhimu.

Hata hivyo, kadri siku zinavyosonga, mambo nayo yanabadilika, baadhi wakijikuta wanatengwa na wana nzengo.

Daudi Mtemi, mkazi wa Kijiji cha Dutwa, wilayani Bariadi, mkoani Simiyu, anasimulia alivyotengwa mwaka jana alipofiwa na mama yake mzazi.

“Mwaka jana nilimpoteza mama yangu, hakuja hata mtu mmoja kutoka nzengo. Nilikuja kugundua kuwa nilikuwa nikikaidi michango na kushindwa kuhudhuria misiba ya wengine. Nilijifunza kwa uchungu,” anasema.

Anasema alitozwa faini ya Sh200,000 iliyoambatana na ununuzi wa sululu mbili, majembe matatu na sufuria kubwa mbili, ndipo wana nzengo walipokubali kushiriki mazishi.

Si yeye pekee, Gabriel John, mwalimu wa Shule ya Msingi Longalonigha iliyopo wilayani Meatu, mkoani Simiyu, alionja adha hiyo kwa kutokushiriki shughuli za kijamii.

“Nilikuwa najiona nina shughuli nyingi, sikuona umuhimu wa kushiriki misiba ya wenzangu, lakini baada ya kushindwa kupata msaada nilipofikwa na msiba, nilijifunza. Sasa siwezi kukosa kuchangia wala kuhudhuria,” anasema.

Kwa upande wake, Dorice John (jina si halisi), mkazi wa Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga, anasema wana nzengo walisusia kula msibani nyumbani kwake.

“Nilitengwa na nzengo kwa sababu sikuwa nakula kwenye misiba. Siku nilipopoteza mwanangu, walifanya kila kitu lakini hawakula. Nilijisikia vibaya sana, nikaomba msamaha lakini wapi. Baadaye uongozi ulinitoza faini,” anasema.

Mkazi wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki, wilayani Ilemela, mkoani Mwanza, Jackline Ferdinand, anasimulia kisa cha mkazi wa mtaa huo aliyekuwa hashirikiani na wenzake, ambaye alipopata tatizo la kuvamiwa na wezi, hakuna aliyetoka kumsaidia, hivyo akabadili mtazamo wake.

"Nzengo siyo kwenye misiba tu, hata matatizo mengine inasaidia. Ni vizuri jamii isidharau, hususani wapangaji," anasema na kuongeza:

"Kama mtu ameishi kwa muda mrefu katika mtaa huu lakini kila yanapotokea matatizo au changamoto hashiriki, anapofikwa na msiba atalipishwa kwanza faini ya Sh70,000. Nzengo haitampa huduma yoyote isipokuwa ya kuzika," anasema.

Mkazi wa Mtaa wa Morembe, Manispaa ya Musoma, Helena Wambura, anasema nzengo si ya kupuuza kwani ina msaada mkubwa mtu anapopata shida.

“Huwezi kubeba msiba mwenyewe hasa kwa watu kama sisi wenye kipato cha chini, hivyo ushiriki wa wenzako ni muhimu ili ufanikishe jambo. Mchango wa Sh2,000 ni mdogo ila ni mkubwa pale ambapo wana mtaa wote wanakuchangia," anasema.

"Msiba unatokea ghafla, mtu huwezi kujipanga, kwa hiyo uwepo wa huduma za wana nzengo zinaleta unafuu na faraja kwa mlengwa," anasema Joyce Martin, mkazi wa Manispaa ya Musoma.


Kwa nini masharti

Baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa wanasema masharti yamewekwa kwa lengo la kuwajibishana na kuimarisha mshikamano.

George Nyagawa, Mwenyekiti wa nzengo ya Majengo, mjini Maswa, anasema wameweka masharti mtaani ili kila mmoja awajibike.

"Tunaweka masharti ili kila mtu awajibike. Si sawa baadhi ya watu wafurahie msaada bila wao kujitolea. Mtu akikaidi, inabidi aelezwe wazi kuwa hatasaidiwa," anasema.

Janeth Mbwelwa, Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwabuzo, wilayani Meatu, anasema utaratibu wa nzengo unasaidia, hasa vijijini, kwa kuwa Serikali haiingilii uamuzi wa wana nzengo ilimradi hawavunji sheria wala haki za binadamu.

Kulwa Charles, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bugwandege, Kata ya Ibadakuli, mkoani Shinyanga, anasema nzengo ina masharti yaliyopitishwa na wakazi wa eneo husika, hivyo anayekwenda kinyume hulazimika kulipa michango ya nyuma na faini kabla ya kurejeshwa.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Bondeni, Manispaa ya Musoma, Amani Joel, anasema mtaa huo una kamati maalumu inayoshughulikia misiba na hakuna aliyewahi kutengwa, lakini kwa wanaokwepa ushiriki, kamati hutoa onyo au kutoza faini.

"Kamati huratibu ushiriki wa kila mwana mtaa. Michango ni kati ya Sh1,000 hadi Sh2,000," anasema.


Imeandikwa na Saada Amir, Samwel Mwanga, Beldina Nyakeke na Hellen Mdinda