CWT Walia uhaba wa nyumba za walimu

Muktasari:
- Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeeleza kuwa bado kuna uhaba wa nyumba za walimu nchini licha ya mafanikio mengi yaliyofanywa na Serikali.
Dodoma. Chama cha Walimu Tanzania (CWT) kimeeleza kuwa bado kuna uhaba wa nyumba za walimu nchini licha ya mafanikio mengi yaliyofanywa na Serikali.
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu rais wa CWT, Dinah Masamani wakati akizungumza mafanikio yaliyopatikana kwa walimu nchini.
Masamani amesema changamoto za uhaba wa nyumba za walimu ni kubwa hivyo ipo haja kwa Serikali kulitazamana kwa jicho pevu jambo hilo.
Hata hivyo amepongeza kuwa katika bajeti zimetengwa Sh55.57 milioni kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu 809 hivyo akaomba fedha hizo zipelekwe kwa wakati kwani zitabeba familia nyingi.
Amesema ndani ya CWT kuna vitu vingi ambavyo wanaweza kujivunia katika kipindi kifupi ikiwemo malipo ya malimbikizo ya madeni na upandishwaji wa madarakani.
“Lakini tatizo bado lipo kwenye nyumba za walimu, huko tuna changamoto kubwa hasa kwa maeneo ya vijijini, tunaomba Serikali itazame jambo hilo kwa jicho pevu,” amesema Masamani.